‘Wanaovaa rozari bila kusali wanakufuru’
θ Wamo wasanii, waamini na wanaoning’iniza kwenye magari
WAAMINI nchini
wametakiwa kutumia vizuri visakramenti ikiwemo Rozari Takatifu ili waweze
kuimarika kiimani. Rai hiyo imetolewa kwa nyakati tofauti na Askofu wa Jimbo
Katoliki Bukoba Mhashamu Desderius Rwoma na Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu
Katoliki Tanzania Padri Raymo nd Saba, ambapo wote wamekemea tabia ya watu
kuvaa rozari bila kusali.
Akiongoza
Misa Takatifu ya ufunguzi wa Kongamano la TYCS Kitaifa Askofu Rwoma amesema
kuwa rozari siyo pambo la kuvaliwa au kuwekwa ndani, bali inamtaka muumini
kuitumia kwa kusali na kuimarika kiroho.
Aidha Askofu
Rwoma amekemea tabia ya wasanii kuvaa rozari katika kazi zao huku matendo
wanayofanya katika nyimbo zao au filamu kutoendana na uwepo wa rozari hizo.
“Unakuta
wasanii wanavaa rozari kwenye nyimbo zao lakini yanayotendeka humo hayafanani
kabisa. Tumieni visakramenti hivi vizuri, mnaovaa rozari mkumbuke kwamba siyo
pambo hilo. Rozari iwasaidie kumpenda Bikira Maria na kuimarika kiimani” ameasa
Askofu Rwoma.
Kwa upande
wake Padri Raymond Saba amesema kuwa kitendo cha kuvaa rozari bila kusali au
kuning’iniza kwenye magari bila kusali ni ushirikina. Amewaasa waamini kusali
rozari kila siku siyo kusali kwa kibiashara, yaani kusali wakati wa shida
pekee.
“Kama unavaa
rozari au unatundika kwenye gari bila kusali, huo ni ushirikina. Rozari kazi
yake ni kusali kila siku, siyo kusali kibiashara yaani kusali kwa nipe nikupe,
kusali pale tu unapokua na shida. Daima mdumu katika kusali rozari” ameeleza
Padri Saba.
Mwezi Mei na
Oktoba kila mwaka waamini wakatoliki wanaalikwa kusali rozari kwa ajili ya nia
mbalimbali, lakini daima sala ya rozari inapaswa kusaliwa kila siku na kila
wakati.
Asante sana Baba Padri Raymond Saba na Baba Askofu Rwamo.
ReplyDelete