Mfuko wa Graca Machel kuinua elimu Musoma
Na Veronica Modest,
Musoma.
SERIKALI Mkoani Mara
imewaondoa hofu walimu wanaotarajia kufundisha watoto walio nje ya mfumo wa
shule kwa ongezeko la vipindi vingi vya darasani katika mradi wa Graca Machel Trust
(GMT) ambao unatekelezwa kwa kushirikiana na Jimbo Katoliki Musoma.
Akizungumza kwenye hafla
ya kufunga mafunzo ya walimu 432 yaliyofanyika kwa muda wa mwezi mzima katika
kituo cha ufundi cha St Anthony na Chuo cha Maendeleo ya Jamii cha Buhare,
kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Bw.Method Mkoba amesema kuwa walimu hao
hawana budi kuondoa wasiwasi wa kuwa na majukumu makubwa wakati wa kuwafundisha
watoto hao, kwa kuwa tayari serikali imekwishaweka mfumo mzuri utakaowasaidia
walimu hao kusimamia majukumu yao bila tatizo.
Mkoba amesema kuwa
Serikali Mkoani hapa imeandaa mikataba ya kazi ambayo itawasaidia walimu hao
katika kusimamia majukumu yao hasa kwa upande wa vipindi vya darasani, ambavyo
awali walikuwa wanafundisha na sasa wameongezewa tena darasa jingine la MEMKWA,
ili kuwapunguzia mzigo mkubwa na kwamba walimu wote watakuwa chini ya mwalimu
mkuu wa shule husika.
Wakizungumza kwa nyakati
tofauti na gazeti hili, baadhi ya walimu walioshiriki mafunzo hayo wamesema
kuwa, wanakuwa na hofu hasa upande wa vipindi vya darasani ambavyo sasa
vimeongozeka kwa kuwa awali wengine walikuwa na vipindi vitano kwa siku
sawa na vipindi 25 kwa wiki, hivyo huenda darasa moja likakosa vipindi na hata
watoto kufeli somo la mwalimu husika, kwa kuwa mwalimu huyo huenda akajikita
zaidi upande wa darasa moja na kushindwa kumudu darasa jingine kwa wakati muafaka.
Mmoja wa walimu kutoka
wilaya ya Butiama (jina tunalihifadhi) amesema kuwa Bi.Graca Machel ana lengo
zuri la kuwasaidia watoto walio nje ya mfumo wa shule, hivyo ili mradi huu
uweze kufanikiwa zaidi, kwanza yawepo
mazingira rafiki ya kuwafundisha watoto kutokana na ukweli kwamba kuna
wengine walikuwa tayari wamekwishaolewa wakiwa na umri mdogo na sasa wanataka
kurudi shuleni, wengine wanahitaji muda mrefu wa kuelimishwa hasa kwa kwenda
taratibu ili wote waelewe, hivyo itawalazimu walimu hao kutumia muda mwingi
zaidi katika madarasa hayo ya MEMKWA kuliko kufundisha darasa la kawaida.
Kaimu Afisa Elimu Mkoa
wa Mara Elisonguo Mshiu amewaambia walimu walioshiriki mafunzo hayo ya MEMKWA
kuwa wameaminiwa na Serikali, hivyo waende wakafikishe kile walichojifunza
katika jamii, kwa kufuata maadili ya utumishi wa Umma na hivyo kuleta matokeo
chanya kwa watoto hao watakaokwenda kuwafundisha walio nje ya mfumo wa shule.
Comments
Post a Comment