Mitandao isiwatenge na Mungu-Askofu Mstaafu awaonya vijana
MWENYEKITI wa jukwaa la Kikristo Tanzania, mkoani
Mbeya, Askofu mstaafu John Mwela, amewaonya vijana wa kitanzania kuwa matumizi
ya mitandao ya kijamii na kukua kwa sayansi na teknolojia kusiwatenganishe na
Mungu.
Askofu Mwela ameyasema hayo wakati
akikabidhi misaada mbalimbali ya vyakula, nguo na mahitaji muhimu ikiwemo
vifaa vya shule vilivyochangwa na wasamaria wema wa kikristo na kiislamu
jijijini Mbeya na kuwasilishwa kwa Shirika lisilo la kiserikali la Sauti
ya Mama Afrika(SAMAFO) akisema kuwa mitandao ya kijamii imekuwa ikiwaondolea
vijana walio wengi hofu ya Mungu na kuiga matendo yasiyompendeza Mungu.
Ametoa wito kwa shirika la Sauti ya Mama Afrika
kuendelea kutoa elimu kwa jamii hasa vijana na familia
majumbani kuwa wasimsahau Mungu kwani kwa sasa hali imekuwa ni mbaya kwa vijana
walio wengi wamefikia hatua ya kuona kwamba Mungu yupo katika
mitandao wanayoperuzi.
Askofu Mwela amesema kwa sasa
dunia ni kama kijiji hivyo vijana wanaona Mungu wao yupo katika
mitandao ya kijamii na simu hali inayosababisha dunia kwa sasa
kughubikwa na dhuluma, uhalifu, matumizi
hovyo ya silaha na vitendo vya utekaji, hivyo amewaombea kwa Mwenyezi
Mungu awasaidie ili wanapofundisha katika program zao wawakumbushe
vijana athari na faida ya mitandao.
“Utandawazi umetandaa kila mahali, kwa hiyo
wanawake mnalo jukumu kubwa kwa vijana kuwafahamisha kuwa matumizi ya
mitandao ya kijamii yasiwasahaulishe Mungu wao na yasiwaondolee kutokuwa na
hofu na Mungu wao kwani kwa sasa hofu haipo, wanaona Mungu hayupo,”
amesema.
“Pengine dunia ilivyo sasa katika
mtikisiko wa hali ya kiuchumi, kiutamaduni, kisiasa, kijamii na hali
mbalimbali, tungeisikiliza sauti ya Mama pengine yasingetokea yanayotokea, kwa
hiyo Sauti ya Mama Afrika ni msemo mzuri sana. Katika Biblia unaikuta sauti
ya Mama Maria kwa mwanawe Yesu iliposikilizwa kilifanyika kitu cha uponyaji,” amefafanua.
Mwenyekiti huyu ameendelea kufafanua kuwa
Sauti ya mama ikisikilizwa katika jamii uponyaji mkubwa unaweza kutokea
akiwasihi waendelee na msimamo na utamaduni wa kuwatembelea yatima na
wahitaji.
Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika lisilo la
kiserikali la Sauti ya Mama Afrika (SAMAFO), Bi.Tabitha Bughali ameiomba Serikali
ya Mkoa wa Mbeya kupitia idara ya ardhi kuwapatia uwanja ili waweze
kujenga nyumba ya amani kwa ajili ya kuwafanyia ushauri nasaha vijana na
kuwasaidia kisheria wanawake wanaofanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Hata hivyo baadhi ya watoto yatima
wanaolelewa katika kituo cha mafunzo na malezi cha Msamaria Mwema kilichopo
kitongoji cha Idiga, Kata ya Songwe viwandani mkoani Mbeya, Emmy Immanuel na
Daniel Richard wametoa angalizo kwa watoto yatima nchini kutokubali
kushawishika na makundi yasiyompendeza Mungu huku mtoto Sharo Edson akiomba
wasamaria wema kuwajengea wigo na kuimarisha ulinzi katika kituo chao.
Comments
Post a Comment