Jamii Manyoni yaaswa kuwathamini watoto yatima

MRATIBU wa kituo cha kulelea watoto yatima cha Manyoni Orphans Sponsorship Association (MOSA) kilichopo wilayani Manyoni mkoani Singida Bi.Mahewa Mowo ametoa wito kwa jamii kuwajali na kujitolea kuwapenda watoto yatima.

Mratibu huyo ametoa kauli hiyo hivi karibuni kituoni hapo alipotembelewa na gazeti hili na kufanya mahojiano maalumu yenye lengo la kuikumbusha jamii juu ya watoto yatima.

Hata hivyo mratibu huyo amesema kuwa jamii inajisahau na kuutupa utu wa mtoto yatima huku baadhi yao wakitendewa vitendo viovu na walezi wao ikiwa ni pamoja na kuwanyima haki ya kupata elimu.

"Jamii imejisahau sana na kuutupa utu wa mtoto yatima ,tafadhali tusiwatenge ili wasijione wapweke, tupo kwa ajili yao," amesema.

Pamoja na hayo Bi.Mowo amesema mtoto yatima ni mtoto wa jamii na hivyo jamii inapaswa kumwangalia kwa ukaribu ili kutimiza mapenzi ya Mwenyezi Mungu ya kumpenda jirani yako kama nafsi yako.

“Watoto yatima ni wa jamii nzima, hatupaswi kuwabagua wala kuwanyanyasa kwani wamezaliwa na ndugu zetu na hivyo ni wajibu wetu kuwapenda na kuwajali na kuongeza ukaribu wa kuwa nao  kwa kipindi chote kigumu wanachopitia cha kuishi bila wazazi wao,” amesema.

Mbali na hayo amesisitiza kuwa serikali pia inapaswa kushirikiana kwa ukaribu na jamii ili kuvumbua waovu wanaowanyanyasa yatima na kwamba imefika wakati jamii nzima kuacha ukimya wa kuwafumbia macho watu wanaowatendea vitendo vibaya watoto hao.

Ameyataja baadhi ya maovu wanayofanyiwa watoto yatima kuwa ni pamoja na kubakwa, kulawitiwa na wakati mwingne kubaguliwa kielimu na kukosa huduma za afya pamoja na kukumbwa na tatizo la ndoa za utotoni.


Comments

Post a Comment

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU