Kongamano la vijana kitaifa kufanyika Moshi

KONGAMANO la Vijana Wakatoliki wa Sekondari na ngazi ya cheti (TYCS) linatarajiwa kufanyika katika Jimbo Katoliki Moshi, ambapo zaidi ya vijana 2000 kutoka majimbo katoliki nchini wanatarajiwa kushiriki.
Taarifa iliyotolewa na Mratibu wa Vijana Taifa katika Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Liberatus Kadio inaeleza kuwa kongamano hilo litafunguliwa Aprili 13 katika Sekondari ya Marangu, ambapo Askofu wa Jimbo Katoliki Bukoba na Mwenyekiti wa Idara ya Utume wa Walei (TEC) Mhashamu Desderius Rwoma ataongoza Misa Takatifu ya ufunguzi huo.
Aidha Padri Kadio ameeleza kuwa Kongamano hilo litafanyika kuanzia Aprili 12 hadi 18 mwaka huu, huku akitumia fursa hiyo kuwakumbusha vijana wote kujitokeza zaidi na kutoa taarifa za ushiriki kupitia walezi wao.
“Dhamira itakayoongoza kongamano ni kutoka Isaya 6:8 ‘Unitume mimi Bwana’. Tumeichagua kwa kuzingatia kuwa kazi ya Chama cha Kitume TYCS ni kumuinjilisha kijana mwenyewe, na kuwainjilisha wenzake katika mazingira ya shule. Kaulimbiu yetu itakuwa ni ‘Jubilei ya miaka 150 ya uinjilishaji Tanzania Bara: Furaha ya Injili kwa wana TYCS” amesema Padri Kadio.
Akielezea lengo la kufanya kongamano hilo Padri Kadio amesema kuwa wanakusudia kuwaweka pamoja vijana ili wafahamiane na waweze kujifunza kwa pamoja. Aidha amezungumzia kukithiri kwa mmomonyoko wa maadili katika ulimwengu wa leo, na kusema kuwa kongamano hilo linakusudia kuwajengea vijana uelewa katika kufuata misingi ya imani na jamii ili waweze kuwa mfano wa kuigwa na jamii inayowazunguka.
“Mwongozo wao unasisitiza katika kuona, kuamua na kutenda. Tunawajengea vijana uwezo wa kumuinjilisha Kristo kwa kuwasaidia vijana wenzao kuona mambo sahihi, kuamua na hatimaye kutenda. Kila mwana TYCS apeleke furaha kwa wengine, ndiyo maana tunawalea kiroho, kimaadili na kusisitiza katika elimu bora,” ameongeza.
Baadhi ya mada zitakazotolewa na wawezeshaji mbalimbali ni pamoja na ‘Miaka 150 ya Uinjilishaji Tanzania Bara na uinjilishaji mpya’ itakayotolewa na Katibu Mkuu wa TEC Padri Raymond Saba, ‘Vyama vya Kitume na mwana TYCS: Changamoto na maswali yenye utata yanayowakabili wana TYCS’ itakayotolewa na Padri Titus Amigu.
Kongamano hilo linatarajiwa kuhitimishwa Aprili 17 ambapo Misa ya kufunga itaongozwa na Askofu Isaac Amani wa Jimbo Katoliki Moshi, huku maaskofu wote wakipewa mwaliko wa kushiriki kongamano hilo.


Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU