Geita waandaa Hija ya Miaka 100 ya Upadri

Jimbo Katoliki Geita linatarajia kuhitimisha Jubilei ya miaka 100 ya Upadri Kijimbo kwa Hija ya aina yake itakayoambatana na Misa Takatifu itakayoongozwa na Askofu wa Jimbo hilo Mhashamu Flavian Kassala katika Parokia ya Nyantakubwa kwenye eneo lenye masalia ya Mmisionari wa kwanza.

Akitangaza tukio hilo hivi karibuni, Mwenyekiti wa Kamati ya Hija, Padri George Nkombolwa amesema pamoja na kwamba maadhimisho ya kuenzi miaka 100 ya upadri Tanzania Bara kijimbo yamepewa uzito mkubwa kwa sababu mmoja wa mapadri wanne wa kwanza wazalendo, (Pd. Angelo Mwilabure) alitokea Jimboni Geita katika Parokia ya Kome-Nyakasasa, Jimbo pia lina Misioni Kongwe iliyoanzishwa miaka ya 1880 na mapadri wa Shirika la White Fathers, ambapo mmoja wao, Padri Mfaransa "Combarieu"alizikwa na masalia yake yanasadikika kuwepo maeneo hayo.

Padri Nkombolwa ambaye pia ni Paroko wa Parokia ya Nyantakubwa amesema uwepo wa Misioni Kongwe kupita zote kwa upande wa Kusini mwa ziwa Victoria, iliyojulikana kama "Misioni ya Mranda" eneo liitwalo Nyamatongo (kwa sasa) karibu na kivuko cha Kamanga, ni uthibitisho tosha kuwa Jimbo Katoliki Geita ni miongoni mwa maeneo yaliyowahi kupata huduma ya mapadri.

"Ni fahari kuwa tunao mlango wa imani ndani ya Jimbo Katoliki Geita katika Parokia iitwayo Nyantakubwa ambapo Wamisionari wa Afrika walifika kwa mara ya kwanza miaka ya 1887 na kuanzisha Parokia ya kwanza kabisa eneo la Mranda (Nyamatongo Ziwani), na baada ya kutoelewana na Mtemi Rwoma wa Karumo waliondoka na kuacha wamesimika Msalaba Mkubwa uliopafanya mahali hapo kwa miaka mingi kujulikana kama "Nyamatongo Msalabani", amesema Padri George.

Amesema Parokia zote za Jimbo hilo wameamua kufanya Hija hapo Msalabani (Misioni iliyopotea ya Mranda) kama sehemu ya kuienzi Jubilei ya Miaka 100 ya kupata mapadri wazalendo, sababu eneo hilo lilionja huduma ya mapadri kwa mara ya kwanza kabisa katika ukanda wa Kusini mwa Ziwa Victoria, na kuacha hapo msalaba na mawe na hivyo imependeza kuwa eneo la Hija.

Kanisa Katoliki Tanzania mwaka huu 2017 linatimiza miaka 100 tangu kuwapata mapadri wa kwanza waafrika waliosoma huko seminarini Rubya na Kajunguti na kuhitimu mafunzo ya Upadri mwaka 1917 huko Jimboni Bukoba, ambao ni mapadri Wilibard Mupapi na Oscar Kyakaraba wa Bukoba, Celestine Kipanda wa Ukerewe na Angelo Mwilabure wa Geita.

Awali akitangaza rasmi kuzinduliwa kwa maadhimisho ya miaka 100 ya Upadri siku ya Misa ya Kubariki Mafuta, Katibu wa Kamati ya Hija, Padri Gelard Singu amesema waamini wa Geita waliwatolea mapadri na Baba Askofu fedha zaidi ya Tsh milioni 20 kama ishara ya kuenzi huduma ya upadri.

Padri Singu amesema kuwa hitimisho la hija kijimbo litaambatana na Matembezi ya Msalaba hadi parokiani Nyantakubwa, semina mbalimbali za uinjilishaji, Ibada ya kitubio, nyimbo za sifa, maigizo ya kuja kwa wamisionari na kesho yake Misa Takatifu eneo la Nyamatongo Msalabani, alipozikwa padri Comparieu.


Maadhimisho kitaifa ya uzinduzi wa Jubilei hii yalifanyika huko Seminarini Rubya kwa Misa Takatifu iliyoongozwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Mwanza Mhashamu Yuda Tadei Ruwa'ichi, na kuhudhuriwa na maelfu ya waamini kutoka majimbo mbalimbali, mapadri na watawa huku kilele kikiwa ni tarehe 15/08/2017 Jimbo Kuu Dodoma.


Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU