Askofu Kassala: Muishini Mungu kwa vitendo

WAAMINI wametakiwa kuitumia Pasaka kufungua njia mpya ya kumfuata Kristo kwa matendo mema ambayo ndiyo yampasayo kila Mkristo kwani wakibaki katika maneno tu ukristu wao unakuwa wa mashaka.
Maneno hayo yamesemwa na Askofu wa Jimbo Katoliki Geita Mhashamu Flavian Kassala wakati wa misa ya Pasaka iliyofanyika katika Kanisa la Bikira Maria wa Fatima lililopo Geita mjini.
Askofu Kassala amesema kwa muda wote ambao waamini hao walikuwa katika Mafungo matakatifu ya Kwaresima ni vyema yawageuze na kuwaondolea madhaifu mbalimbali ya kiroho ili kila muumini ajitahidi kuishi katika mwenendo mwema wa kumwelekea Kristo aliyeshinda mauti.
Aidha amewahimiza waamini hao kuyatambua madhaifu yao ya kiroho na kuyakabidhi kwa Kristo ili yageuzwe kwa neema za Mungu na kuwa imara katika kumtumikia Mungu maana kumtumikia mungu bila kuhitaji msaada wake ni kujidanganya.
Amesema kila muumini anapaswa kujua kuwa mafumbo matakatifu ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo ni safari iliyoongozwa na utii hadi mauti, hivyo akawahimiza waaamini hao kuwa watii kwa Kristo aliyekubali kufa kifo cha aibu kwa ajili ya kuwakomboa wote.
“Ndugu tuongozwe na utii tunapomtafakari Kristo mfufuka, tutii bila kujibakiza kwa kuuishi mwenendo mwema wa kumpendeza Mungu ambaye kila mmoja anaona thamani ya sadaka yake takatifu ya kutufia msalabani ili tukombolewe kutoka katika utumwa wa dhambi,” amesema
Amehimiza wanafamilia hasa baba na mama kuishi kwa kuheshimiana ili kuzifanya familia zao kuwa chanzo kikuu cha amani, kwa kufanya hivyo watakuwa wanatoa somo zuri kwa watoto wa familia zao kuonja upendo na hivyo kuzifanya familia hizo kuwa Kanisa dogo la sala.
Amesisiza pia waamini hao kujisomea neno la Mungu ambalo alisema ni nuru angavu kwa kila mwenye kulisoma na kuliishi, ambapo amesema kichwa kilicho wazi ni karakana ya shetani ambayo huitumia kutengeneza uovu mwingi.
Katika hatua nyingine Askofu Kassala ameungana na viongozi wengine wa dini na watu mbalimbali nchini kukemea mauaji ya Askari Polisi 8 hivi karibuni wakiwa kazini akisema kitendo hicho hakikubaliki hata kidogo kwa nchi yenye amani kama Tanzania.


Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU