Upotoshaji wa Padri kuoa watolewa ufafanuzi
BAADA ya
mitandao ya kijamii pamoja na baadhi ya vyombo mbalimbali vya habari kupotosha
kuwa Kanisa Katoliki limemfungisha ndoa padri wake, imefafanuliwa kuwa, Padri
akiomba kuondolewa upadri wake anaruhusiwa kuoa.
Askofu
Msaidizi wa Jimbo Katoliki Bukoba Mhashamu Methodius Kilaini ameeleza
kuwa,katika wito wa Upadri katika Kanisa Katoliki , mapadri hawaoi na hiyo ni
sheria ama nidhamu ya Kanisa siyo ya Mungu hivyo Papa ana uwezo wa kuitengua.
“Katika
Kanisa Katoliki Padri ni kasisi, ni kuhani anayetolea sadaka altareni. Kutokana
na nidhamu ya Kanisa Padri haruhusiwi kuoa lakini pale anaposhindwa kuendelea
na wito wake ama anapoonekana kwamba anashindwa kuuishi upadri wake anaruhusiwa
kuomba kuacha na anaruhusiwa kulingana na taratibu za Kanisa.
Mapadri
ambao mitandao ya kijamii pamoja na vyombo vya habari vinazungumzia siyo
mapadri walishafuata taratibu zote na kupata kibali kutoka kwa Baba Mtakatifu
kuwa wamefunguliwa na upadri wao umeondolewa hivyo wana uhuru wa kuoa kwani
wamefanywa walei si mapadri.
Padri
akishavuliwa upadri haitwi tena Padri wala hawezi kutoa huduma kama padri, ana
haki za kuishi ulei wake. Kulingana na taratibu za imani ya Kanisa Katoliki
mlei anafunga ndoa aishi na mume ama mke wake kwa uhalali na kuweka maagano yao
mbele ya Mungu na hapo hakuna kosa.
Tatizo ni
tafsiri ya wanahabari kukuza mambo na kusema padri wa Kanisa Katoliki kaoa
wakati alishaondolewa upadri.
Dr Wilbroad Slaa alikuwa Padri wetu tena
Katibu Mkuu wa TEC ambaye nilimrithi lakini aliacha upadri kulingana na
taratibu za Kanisa akaoa, huyu mwingine Kalugendo naye vilevile alifuata
taratibu yupo huru na wako sahihi.
Hakuna
aibu Kanisa Katoliki iliyopata wala halijakosea. Tuna taratibu zetu ni mambo tu
ya kuelewa,” amesema Askofu Kilaini.
Kwa upande
wake Padri Stefano Kaombe aliyefungisha ndoa hiyo katika Kanisa la Mtakatifu
Petro Osterbay amesema kuwa, vyombo vya habari haviko sahihi kusema Padri wa
Kanisa Katoliki ameoa kwani Kanisa likishamaliza taratibu zake za kumfanya
padri mlei yaani kumuondolea ukasisi wake linamuondolea hadhi yake ya upadri.
“Kuna
kuondolewa hadhi ya upadri na kufunguliwa kifungo cha useja. Mtu anaweza
kufanywa mlei lakini kifungo cha useja kikabaki au unaweza kufunguliwa vyote.
Bw.
Privatus Kalugendo alifunguliwa vyote Septemba 14 mwaka 2008 kwa hati ya Papa
yenye Protokali No.4182/08.
Hivyo Bw.
Kalugendo alikuwa huru tokea siku hiyo kufunga ndoa kwani hakuwa padri na
hakufungwa useja,” ameeleza.
Comments
Post a Comment