Papa Francisko ametuachia zawadi ya Injili ya furaha na matumaini!

Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili jioni tarehe 2 Aprili 2017 amehitimisha hija yake ya kichungaji Jimbo Katoliki Carpi, Italia kwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, kuzungumza na wakleri, watawa na majandokasisi na hatimaye kutembelea eneo la Mirandola ambalo liliathiriwa vibaya sana na tetemeko la ardhi kunako mwaka 2012. Askofu Francesco Cavina wa Jimbo Katoliki Carpi anamshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko aliyewaonjesha furaha ya kweli kwa neno na matumaini ya kuweza kusonga mbele licha ya makovu makubwa yaliyoachwa na tetemeko la ardhi.
Askofu Cavina anasema katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema, mahubiri ya Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Ibada ya Misa Takatifu mbele ya bahari ya watu kutoka ndani na nje ya Jimbo la Carpi, yalikuwa ni utenzi wa Injili ya maisha yanayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu; ambaye pia ni chemchemi ya matumaini; maneno aliyoyazungumza wakati akiwa mbele ya Kanisa kuu la Mirandola, ambalo bado halijaguswa ili kufanyiwa ukarabati mkubwa.
Hii imekuwa ni hija ya kichungaji iliyomwezesha Baba Mtakatifu kukutana, kusalimiana na kuzungumza na umati mkubwa wa watu wenye mapenzi mema; ziara ambao imeacha chapa ya kudumu katika akili na mioyo ya watu wa Mungu Carpi na Mirandola. Watu wengi wameridhika na uwepo wa Baba Mtakatifu Francisko miongoni mwao! Licha ya kutembelea na kujionea mwenyewe uharibu mkubwa uliofanywa na tetemeko la ardhi huko Mirandola, Baba Mtakatifu pia amepata nafasi ya kukutana na kuzungumza na wagonjwa, walemavu na wazee; amana na utajiri mkubwa wa maisha na utume wa Kanisa na jamii katika ujumla wake.
Baba Mtakatifu amepata nafasi ya kukutana na kuzungumza kwa faragha na wakleri, watawa na majandokasisi wa Jimbo Katoliki la Carpi, Italia. Mazungumzo haya yamefanyika katika hali ya amani na utulivu; upendo na mshikamano kwa kukazia kwa namna ya pekee kabisa mafungamano ya kijamii sanjari na umoja wa Kanisa.Wakleri na watawa wamezungumza kwa uwazi yale yaliyokuwa moyoni mwao na Baba Mtakatifu akawajibu kwa ufasahaa kama Baba na Mchungaji mwema.
Ni matumaini ya Askofu Francesco Cavina kwamba, ziara ya kichungaji ya Baba Mtakatifu itaweza kuzaa matunda kwa wakati wake, hasa zaidi kwa kudumisha mafungamano ya kijamii; umoja, upendo na mshikamano katika maisha na utume wa Kanisa. Tetemeko la ardhi limekuwa ni kosa lenye heri kwani limesababisha kwa kiasi kikubwa umoja na mshikamano kati ya wananchi wa Carpi na Mirandola. Furaha na matumaini ni matunda makubwa yatakayoendelea kufanyiwa kazi na familia ya Mungu Carpi na Mirandola.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI