Watoto walemavu na wazee waendelea kunyanyapaliwa
MOROGORO, Serikali
imeshauriwa kusaidia kujenga vituo vya afya katika vituo vya kulelea
watoto wenye ulemavu mbalimbali kutokana na kunyanyapaliwa na baadhi ya
wahudumu wa vituo vya afya vya umma wanapokwenda kupata huduma ya
matibabu.
Mkurugenzi wa Kituo cha Amani Centre
kilichopo Mkoani Morogoro Padri Beatus Sewando, amebainisha hayo wakati
akieleza changamoto mbalimbali zinazowakabili watoto wenye ulemavu hususani
wanapoenda kupatiwa huduma za afya katika vituo vya afya.
Padri Sewando amesema kuna baadhi ya
wahudumu wa afya katika hospitali za umma ambao hutoa huduma mbaya kwa watoto
wenye ulemavu hasa kutowasikiliza kwa wakati kiasi cha kusababisha vifo vya
watoto hao.
“Tunapokwenda kwenye hospitali za umma
baadhi ya wahudumu wanawanyanyapaa mkishasema kwamba huyu ni mlemavu na
wanapoona matendo anayoyatenda, huduma zinakuwa mbaya zaidi na inasababisha
baadhi ya watoto kupoteza maisha, endapo wangepatiwa huduma kwa wakati
wangepona,” amesema Padri Sewando.
Aidha amefafanua kuwa watoto wenye
ulemavu wanapofika katika hospitali hasa za umma hupokelewa tofauti na wale
wasiokuwa na ulemavu, kiasi cha wasimamizi na walezi wa watoto hao kujisikia
vibaya kwa mapokezi hayo na kuona wazi kuwa watoto hao wananyanyapaliwa.
Pamoja
na hayo, Mkurugenzi huyo amesema kuwa kulingana na sera ya afya wazee na
watu wenye ulemavu hupata matibabu bure, lakini imekuwa ni tofauti kwa watoto
watoto hao hali inayowalazimu baadhi ya watu wenye mapenzi mema kuwakatia
baadhi ya watoto hao bima za afya.
“Hili suala linapaswa kufuatiliwa na
serikali yenyewe kama wametamka kitu waweke ufuatiliaji waone ile bure
inafanyika kweli?, kwasababu malalamishi tunayasikia hata kwenye vyombo vya habari hata kwa wazee ambao wanatakiwa
watibiwe bure sijaona wazee wanaoridhika kiasi cha kuamini anapata huduma bure,
akienda pale mzee ataandikiwa lakini dawa hamna hivyo kama serikali ina nia ya
dhati kuwahudumia wazee na wenye ulemavu ifanye mpango kuwe na fungu na akiba
maalumu ya dawa kwa ajili yao na kuwapa kipaumbele,” amesema Padri Sewando.
Hata hivyo amesema kuwa ana imani na serikali
ya awamu ya tano kuwa itatekeleza na kusimamia vyema suala la huduma za afya
kwa wazee na walemavu kwa sababu kwa muda mrefu imekuwa kinyume na utekelezaji
wa sera husika.
Wakati huohuo Padri Sewando amewaomba
wahudumu wa afya kuwa na huruma na watoto walemavu na wazee kwa kuwajali na
kuwapatia huduma sawasawa na wengine, kwani hawakupenda kuzaliwa walemavu na
uzee haukwepeki na kuwapa huduma stahiki bila manung’uniko ni Baraka pia.
Na Josephine Burton, Morogoro
Comments
Post a Comment