Kongamano la Utoto Mtakatifu (Haki na Amani) kufanyika Juni Zanzibar
Kongamano la utoto Mtakatifu-Watoto wa Haki
na Amani linatarajiwa kufanyika Jimboni Zanzibar kuanzia tarehe 8-11 Juni mwaka
huu.
Hayo yamesemwa na Askofu wa Jimbo Katoliki Zanzibar Mhashamu
Augustine N.Shao C.S.Sp hivi karibuni ambapo amewaalika waaamini kuwaandaa
watoto kwa ajili ya Kongamano hilo.
Askofu Shao amesema Kongamano hili ni sehemu ya Umisionari
wa Watoto kwa watoto wenzao wa Zanzibar
na wakristo kwa ujumla.
Katika Kongamano hilo watoto wataonesha vipawa vyao katika
kumsifu Mungu, kushirikishana zawadi walizojaliwa na Mwenyezi Mungu katika
michezo, sala na kufurahia kwa pamoja kama familia.
Askofu Shao ameomba waamini waungane na watoto hao katika
kusali na kuiombea Dunia amani ambayo ni lazima ianzie kwenye familia na kuwa
na umoja.
Kauli mbiu ya kongamano hilo ni “UPENDO NA MSAMAHA UHAI WA
FAMILIA” ambayo imejikita katika kutafakari nguvu ya msalaba na Neno la Mungu.
“Kristo amekuja ili tuwe na uhai tena tuwe nao kamili” (Jn.10:10)
Wakati huohuo, Paroko wa parokia ya Mjini
Unguja, Jimbo Katoliki Zanzibar Padri Richard Haki akishirikiana na Padri Mathias
C.S.Sp, wamewaomba waamini wakristo kuwachangia chochote watoto wa Haki
na Amani ili kuweza kufanikisha Kongamano hilo.
Amesema kongamano hilo litawakusanya watoto kutoka
Tanzania Bara na visiwani, hivyo wawe na muamko wa kuwachangia watoto hao kwa
sababu ni neema kwa Zanzibar kupata nafasi ya kuandaa Kongamano hilo.
Hata hivyo Padri Haki amesema kuwa ndani ya
sherehe hizo kutakuwepo na masomo tofauti tofauti ya kumjenga mtoto kiakili hususani
katika masuala ya Imani.
Padri Haki amewasihi wazazi na vijana
kuwachangia watoto hao ili kufanikisha zoezi hilo la sherehe ya watoto wa Haki
na Amani itakayofanyika mwezi wa sita katika viwanja vya shule ya Francis Maria
Libermann Zanzibar.
Naye Padri Padri Mathias akinukuu injili ya Mathayo
7:7 kuwa “ombeni nanyi
mtapewa tafuteni nanyi mtapata” kuwasihi waamini kujitoa kwa kutoa
michango na majitoleo yao kwa wakati.
Katika harambee iliyofanyika ndani ya muda mfupi
baada ya ibada ya Misa ya Jumapili ya pili ya Pasaka, zilipatikana fedha za
kitanzania shilingi 404,000 kutoka kwa waamini wa Kanisa la Minara Miwili.
Mapadri hao waliwashukuru waamini kwa mchango
wao walioutoa kwa ajili ya watoto wa haki na amani.
Misa ya Ufunguzi wa Kongamano hilo itaadhimishwa tarehe 9
Juni na Askofu Augustine Shao na
kutakuwa na mada mbalimbali za majiundo katika Imani na kuzidi kutambua upendo
wa Mungu kwetu.
Kongamano hilo la
Kanda za Mashariki na Kati linajumuisha majimbo 9 pamoja na Zanzibar yenyewe.
Majimbo ya Kanda ya Mashariki ni Jimbo Kuu Dar Es Salaam, Jimbo Katoliki Tanga, Jimbo Katoliki Morogoro, Jimbo Katoliki Ifakara, Jimbo Katoliki
Mahenge na Jimbo Katoliki Zanzibar. Majimbo
ya Kanda ya Kati ni Jimbo Kuu Dodoma, Jimbo Katoliki Singida na Jimbo Katoliki
Kondoa.
Jimbo Katoliki Zanzibar linalojumuisha Visiwa vya Unguja na
Pemba, lina Parokia zipatazo 8 na 1 tarajiwa.
Comments
Post a Comment