Chuki na dharau vitalibomoa taifa
ASKOFU Jemsi Almasi wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Masasi amewataka
watanzania kuondoa chuki na dharau ambazo zinasababisha mauaji na hofu kwa
jamii.
Ameyasema hivi karibuni katika mahubiri yake ya Misa ya Pasaka
iliyofanyika katika Kanisa la Mtakatifu Edward mjini Lindi.
Amesema katika kuadhimisha sikukuu ya Pasaka ya ufufuo wa Bwana Yesu
Kristo ambaye alifuta hati ya mashitaka ya dhambi kwa wanadamu ili watu
wamrudie Mungu wao, lakini kwa sasa ni tofauti kwani wanadamu wameanza
ukengeufu.
Askofu Almasi amesisitiza kuwa taifa la Tanzania lilijengewa misingi ya
uvumilivu, utii na upendo ambapo kila mtanzania alifanya kazi kila kona ya nchi
bila hofu kwa vile alijiamini kuwa watanzania wote walikuwa ni ndugu.
“Kwa sasa taifa hili limeanza kuingiwa na hofu ya maisha, kila mtu amekuwa
hana amani ya kufanya kazi ya kuleta maendeleo jambo ambalo litarudisha nyuma
jitihada za kufikia maisha bora,”amesema Almasi
Askofu huyo amesema matatizo
yote yanatokana na chuki na visasi ambapo jambo hili linawasababishia
watanzania kutoaminiana hivyo kukosa upendo, uvumilifu na utii jambo ambalo
litalibomoa taifa ambalo ni teule.
“Taifa la Tanzania linasafiri kwa nguvu za Mungu kwa kuwa watu wake
walikwisha futiwa mashitaka na waasisi wetu, hivyo tuheshimu uhuru wa kila raia
kwani ana haki sawa na wewe,”amesema Askofu huyo
Ameongeza kuwa kila kiongozi wa serikali katika taifa hili anao wajibu wa
kuheshimu msingi wa katiba ya nchi, katiba ya kila dini, maana ndio misingi ya
uongozi ambayo inaondoa chuki na visasi.
“Hata Yesu alimwambia Petro rudisha upanga halani, kwani ukifanya hivyo
watu wote wataangamia kwa upanga, hivyo basi
sisi tuseme turudishe mitutu yetu ya bunduki ghalani kwani tumeanza
kuangamia kwa mtutu jambo linaloleta hofu kubwa kwa maisha yetu.”
Amehitimisha kuwa utii na upendo ndio silaha pekee ya mafanikio ya amani
ya taifa linalohitaji maendeleo kwa wananchi wake.
Comments
Post a Comment