“Hakuna mafuta mbadala ya krisma”
ASKOFU wa
Jimbo Katoliki Iringa Mhashamu Tarcisius Ngalalekumtwa amewataka waamini
kuwaombea mapadri na hasa katika kipindi hiki ambacho wanaadhimisha miaka 100
tokea wapatikane mapadri wa kwanza Tanzania Bara, ili waweze kuishi katika Roho
ya kweli isiyo na uroho na pia kuutendea haki ukuhani kwa kumuakisi Yesu katika
yote.
Mhashamu
Ngalakumtwa ameyasema hayo mwishoni mwa juma katika misa ya kubariki mafuta
(Krisma) ya wagonjwa,wakatekumeni na kuyaweka wakfu mafuta ya Krisma, misa
ambayo imefanyika katika Kanisa Kuu la kiaskofu la Moyo Mtakatifu wa Yesu
Parokia ya Kihesa.
Amesema
kwamba ikiwa makuhani hao watafanya vile anavyotaka Roho Mtakatifu, wanamfanya
Kristo atende kama zama hizo na siyo kuhani kumzamisha muamini katika giza.
“Siyo mie
kuhani nakuzamisha kwenye giza, nashindwa kuwasaidia wale wenye mioyo mizito
hapana, natakiwa niwapatie tumaini jipya, na waliokata tamaa niwaelekeze kwamba
kabla hajafa hujaumbika,” amesema Mhashamu Ngalalekumtwa.
Aidha
Mhashamu Ngalalekumtwa amekemea baadhi ya waamini wanaosema kwamba kuna mafuta
kutoka sehemu fulani au ya Mama Bikira Maria na amesema kuwa huo ni upotoshaji
mkubwa.
“Hakuna
mafuta yanayotumika katika liturujia zaidi ya haya, huo ni upuuzi mtupu na
uhuni, mnakufuru huo ni utapeli wa kiroho.
Tutayaweka
wakfu mafuta ya Krisma ambayo yanatumika kwa sakramenti mbalimbali na matumizi
mengine kama kuitakatifuza altare, ubatizo, kipaimara, wanapakwa pia mapadri na
maaskofu, tutabariki mafuta ya wagonjwa na mafuta ya wakatekumeni.” Ameonya
Aidha
katika misa hiyo ambapo makuhani hao walirudia viapo vyao, Mhashamu
Ngalalekumtwa amesema kwamba, makuhani wanajazwa Roho kuwasaidia waamini
sakramenti ya kiroho wanashirikishwa kazi hiyo nzito na takatifu, hivyo waamini
wanapaswa kuwaombea.
“Tumekusanyika
kuadhimisha karama zetu na pia kurudia viapo vyetu mbele ya Mungu na Kanisa,
tunatoa sadaka za kiroho kwa Mungu, daraja hili lina hadhi na majukumu ya
kipeke,” Amefafanua
Misa hiyo
imehudhuriwa na mapadri 70 kutoka jimboni Iringa, watawa wa kike na kiume
pamoja na waamini wenye mapenzi mema.
Comments
Post a Comment