Geita waandaa Hija ya Miaka 100 ya Upadri
Jimbo Katoliki Geita linatarajia kuhitimisha
Jubilei ya miaka 100 ya Upadri Kijimbo kwa Hija ya aina yake itakayoambatana na
Misa Takatifu itakayoongozwa na Askofu wa Jimbo hilo Mhashamu Flavian
Kassala katika Parokia ya Nyantakubwa kwenye eneo lenye masalia ya
Mmisionari wa kwanza.
Akitangaza tukio hilo hivi karibuni, Mwenyekiti
wa Kamati ya Hija, Padri George Nkombolwa amesema pamoja na kwamba maadhimisho
ya kuenzi miaka 100 ya upadri Tanzania Bara kijimbo yamepewa uzito mkubwa kwa
sababu mmoja wa mapadri wanne wa kwanza wazalendo, (Pd. Angelo Mwilabure)
alitokea Jimboni Geita katika Parokia ya Kome-Nyakasasa, Jimbo pia lina Misioni
Kongwe iliyoanzishwa miaka ya 1880 na mapadri wa Shirika la White Fathers,
ambapo mmoja wao, Padri Mfaransa "Combarieu"alizikwa na masalia yake
yanasadikika kuwepo maeneo hayo.
Padri Nkombolwa ambaye pia ni Paroko wa Parokia
ya Nyantakubwa amesema uwepo wa Misioni Kongwe kupita zote kwa upande wa Kusini
mwa ziwa Victoria, iliyojulikana kama "Misioni ya
Mranda" eneo liitwalo Nyamatongo (kwa sasa) karibu na kivuko cha
Kamanga, ni uthibitisho tosha kuwa Jimbo Katoliki Geita ni miongoni mwa maeneo
yaliyowahi kupata huduma ya mapadri.
"Ni fahari kuwa tunao mlango wa
imani ndani ya Jimbo Katoliki Geita katika Parokia iitwayo
Nyantakubwa ambapo Wamisionari wa Afrika walifika kwa mara ya
kwanza miaka ya 1887 na kuanzisha Parokia ya kwanza kabisa eneo la
Mranda (Nyamatongo Ziwani), na baada ya kutoelewana na Mtemi Rwoma wa Karumo
waliondoka na kuacha wamesimika Msalaba Mkubwa uliopafanya mahali hapo kwa
miaka mingi kujulikana kama "Nyamatongo Msalabani", amesema Padri
George.
Amesema Parokia zote za Jimbo hilo wameamua
kufanya Hija hapo Msalabani (Misioni iliyopotea ya Mranda) kama sehemu ya
kuienzi Jubilei ya Miaka 100 ya kupata mapadri wazalendo, sababu eneo hilo
lilionja huduma ya mapadri kwa mara ya kwanza kabisa katika ukanda wa Kusini
mwa Ziwa Victoria, na kuacha hapo msalaba na mawe na hivyo imependeza kuwa eneo
la Hija.
Kanisa Katoliki Tanzania mwaka huu 2017
linatimiza miaka 100 tangu kuwapata mapadri wa kwanza waafrika waliosoma huko
seminarini Rubya na Kajunguti na kuhitimu mafunzo ya Upadri mwaka 1917 huko Jimboni
Bukoba, ambao ni mapadri Wilibard Mupapi na Oscar Kyakaraba wa Bukoba, Celestine
Kipanda wa Ukerewe na Angelo Mwilabure wa Geita.
Awali akitangaza rasmi kuzinduliwa kwa maadhimisho
ya miaka 100 ya Upadri siku ya Misa ya Kubariki Mafuta, Katibu wa Kamati ya
Hija, Padri Gelard Singu amesema waamini wa Geita waliwatolea mapadri na Baba
Askofu fedha zaidi ya Tsh milioni 20 kama ishara ya kuenzi huduma
ya upadri.
Padri Singu amesema kuwa hitimisho la hija
kijimbo litaambatana na Matembezi ya Msalaba hadi parokiani Nyantakubwa, semina
mbalimbali za uinjilishaji, Ibada ya kitubio, nyimbo za sifa, maigizo ya kuja
kwa wamisionari na kesho yake Misa Takatifu eneo la Nyamatongo Msalabani,
alipozikwa padri Comparieu.
Maadhimisho kitaifa ya uzinduzi wa Jubilei hii
yalifanyika huko Seminarini Rubya kwa Misa Takatifu iliyoongozwa na Askofu Mkuu
wa Jimbo Kuu Mwanza Mhashamu Yuda Tadei Ruwa'ichi, na kuhudhuriwa na maelfu ya
waamini kutoka majimbo mbalimbali, mapadri na watawa huku kilele kikiwa ni
tarehe 15/08/2017 Jimbo Kuu Dodoma.
Comments
Post a Comment