Askofu Mkude aiasa jamii kujitegemea

MOROGORO, Jamii imetakiwa kuwa na moyo wa kujitoa kwa hiyari ili kuchangia huduma mbalimbali na kuonyesha nia yakutatua tatizo badala ya kusubiri kushurutishwa au lifanywe na serikali wakati jamii husika ina uwezo wa kulitatua ikiwa na dhamira.
Hayo ameyasema Askofu wa Jimbo Katoliki Morogoro Mhashamu Telesphor  Mkude alipokuwa akihubiri katika parokia teule ya Mtakatifu Josephine Bakita wa Shirika la Stigimatine iliyo Nanenane, ibada iliyoambatana na harambee ya kuchangia ujenzi wa nyumba ya Padri.
Askofu Mkude amesema jamii inapaswa kujitoa na siyo kusubiri ifanyiwe kila kitu ikiwa watu kwa utashi waliopewa na Mungu wana uwezo wa kusimama na kufanya pasipo kutegemea nguvu ya mtu mwingine iwainue.
“Jamii inapaswa kujitoa na siyo kusubiria kufanyiwa kila kitu, ikiwa sisi wenyewe tuna uwezo wa kusimama na kufanya pasipo kutegemea nguvu ya mtu mwingine aje atuinue, kwa kufanya hivyo ni kushusha ule utashi ambao Mungu ametupatia na kujiona wanyonge tusioweza kufanya chochote,” amesema Askofu Mkude.
Amesisitiza kuwa jamii inapaswa kutumia kile kidogo ambacho wanacho kwa kuanza kutatua kero ambayo inawakabili ili wanapokwama na kuomba kusaidiwa atakae wasaidia atoe msaada kwa moyo kwakuwa ameona juhudi binafsi.
“Tunatakiwa tutumie kile kidogo ambacho tunacho kwa kuanza kutatua kero ambayo inatukabili ili tunapokwama na kuomba kusaidiwa atakae tusaidia awe na nia nzuri kwakuwa ameona dhamira, juhudi na kujitoa kwetu kwa hiyari ili kutatua kero ambayo inatukabili,” amesema Askofu Mkude.
Wakati huo huo amesisitiza kuwa, kila mmoja atoe kile anachoona ni jiwe katika maisha ambalo linasababisha uzito ili kuifanya vyema kazi ya Mungu pasipo mikwamo.

 “Kila mmoja wetu aondoe jiwe lililopo mbele yako, liwe ni jiwe la uchoyo , ubinafsi na mawe mengine ili tuifanye kazi ya Mungu kwa imani isiyo na mawaa na matendo,” amesema Askofu Mkude.

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI