Kongamano la vijana kitaifa kufanyika Moshi
KONGAMANO la
Vijana Wakatoliki wa Sekondari na ngazi ya cheti (TYCS) linatarajiwa kufanyika
katika Jimbo Katoliki Moshi, ambapo zaidi ya vijana 2000 kutoka majimbo
katoliki nchini wanatarajiwa kushiriki.
Taarifa
iliyotolewa na Mratibu wa Vijana Taifa katika Baraza la Maaskofu Katoliki
Tanzania (TEC), Padri Liberatus Kadio inaeleza kuwa kongamano hilo
litafunguliwa Aprili 13 katika Sekondari ya Marangu, ambapo Askofu wa Jimbo
Katoliki Bukoba na Mwenyekiti wa Idara ya Utume wa Walei (TEC) Mhashamu
Desderius Rwoma ataongoza Misa Takatifu ya ufunguzi huo.
Aidha
Padri Kadio ameeleza kuwa Kongamano hilo litafanyika kuanzia Aprili 12 hadi 18
mwaka huu, huku akitumia fursa hiyo kuwakumbusha vijana wote kujitokeza zaidi
na kutoa taarifa za ushiriki kupitia walezi wao.
“Dhamira
itakayoongoza kongamano ni kutoka Isaya 6:8 ‘Unitume mimi Bwana’. Tumeichagua
kwa kuzingatia kuwa kazi ya Chama cha Kitume TYCS ni kumuinjilisha kijana
mwenyewe, na kuwainjilisha wenzake katika mazingira ya shule. Kaulimbiu yetu
itakuwa ni ‘Jubilei ya miaka 150 ya uinjilishaji Tanzania Bara: Furaha ya
Injili kwa wana TYCS” amesema Padri Kadio.
Akielezea
lengo la kufanya kongamano hilo Padri Kadio amesema kuwa wanakusudia kuwaweka
pamoja vijana ili wafahamiane na waweze kujifunza kwa pamoja. Aidha
amezungumzia kukithiri kwa mmomonyoko wa maadili katika ulimwengu wa leo, na
kusema kuwa kongamano hilo linakusudia kuwajengea vijana uelewa katika kufuata
misingi ya imani na jamii ili waweze kuwa mfano wa kuigwa na jamii
inayowazunguka.
“Mwongozo
wao unasisitiza katika kuona, kuamua na kutenda. Tunawajengea vijana uwezo wa
kumuinjilisha Kristo kwa kuwasaidia vijana wenzao kuona mambo sahihi, kuamua na
hatimaye kutenda. Kila mwana TYCS apeleke furaha kwa wengine, ndiyo maana
tunawalea kiroho, kimaadili na kusisitiza katika elimu bora,” ameongeza.
Baadhi ya
mada zitakazotolewa na wawezeshaji mbalimbali ni pamoja na ‘Miaka 150 ya
Uinjilishaji Tanzania Bara na uinjilishaji mpya’ itakayotolewa na Katibu Mkuu
wa TEC Padri Raymond Saba, ‘Vyama vya Kitume na mwana TYCS: Changamoto na
maswali yenye utata yanayowakabili wana TYCS’ itakayotolewa na Padri Titus
Amigu.
Kongamano
hilo linatarajiwa kuhitimishwa Aprili 17 ambapo Misa ya kufunga itaongozwa na
Askofu Isaac Amani wa Jimbo Katoliki Moshi, huku maaskofu wote wakipewa mwaliko
wa kushiriki kongamano hilo.
Comments
Post a Comment