Maaskofu Dodoma walaani mauaji, ubakaji na utekaji nchini

UMOJA wa madhehebu ya kikristo mkoa wa Dodoma umewataka watanzania kuunganisha nguvu zao za pamoja za kiroho na kimwili na serikali, ili vitendo vya kikatili vinavyotokea viweze kukomeshwa vikiwemo vile vya mauaji, utekaji na ubakaji wa watoto wa kike na mauaji ya vikongwe.
Aidha umoja huo pia umelaani na kukemea vikali vitendo ambavyo vimetokea hivi karibuni vya mauaji ya askari wa jeshi la polisi wanane, na kuwaomba watanzania kuungana na serikali ili wale wote waliohusika waweze kukamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya dola.
Kauli hiyo ya umoja huo imetolewa hivi karibuni  na Askofu Dr Damasi Mukasa alipokuwa akizungumza na waamini wa madhehebu mbalimbali ya dini kwenye viwanja vya Kanisa Kuu la kiinjili Kilutheli Tanzania (KKKT) Usharika wa Dodoma mjini.
Akizungumza na waamini hao, amewataka watanzania kuungana kwa pamoja na serikali katika kufichua maovu yanayojitokeza kwenye maeneo mbalimbali kama vile ya mauaji ambayo hivi karibuni Taifa limewapoteza askari wake ambao wameuawa na majambazi wilayani Kibiti mkoani Pwani.
Amesema serikali peke yake kamwe haiwezi kuwabaini wanaofanya vitendo ambavyo ni kinyume na katiba yetu ya nchi, bali ni pale watanzania watakapoungana kwa pamoja katika kuwafichua watu hao.
Aidha amewataka watanzania kuungana kwa pamoja katika kuliombea taifa na viongozi wa nchi ili waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi na kwa maslahi ya kila mwananchi.
“Kama tulivyokuwa tukiomba kwa Mungu kwa ajili ya kutupatia viongozi kutoka kwake, hivyo hivyo tunatakiwa nguvu ile ile pia tuwaombee hao viongozi waliochaguliwa ili waweze kufanya shughuli zao za kimaendeleo kwa maslahi ya watanzania wote na si vinginevyo,”amesema.
Naye Askofu wa Dayosisi ya kati Kanisa la Anglikana Dr Dickson Chilongani ameutaka Umoja wa madhehebu mkoani humo kuhakikisha wanawaunganisha waamini wao na kuwa kitu kimoja, ili changamoto zinazojitokeza ziweze kutatuliwa kwa pamoja.
Amesema wakiungana kwa pamoja bila kujali dini zao wataweza kuisaidia serikali katika kutatua changamoto kadhaa kama vile suala la mauaji, ubakaji na utekaji kwa kuzipata taarifa zitakazosaidia kuwabaini wahalifu wanaoichafua amani iliyopo.
“Ni imani yangu sisi kama viongozi wa dini, waamini pamoja na serikali yenyewe tukiwa kitu kimoja tunaweza kuondoa changamoto hizi zinazojitokeza kwa kuwa tutakuwa tayari kuhakikisha wahusika wanakamatwa na vyombo vya dola bila pingamizi lolote,”amesema.
Kwa upande wake Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Dodoma Mhashamu Beatus Kinyaiya amewataka wananchi wa mkoa wa Dodoma kuwa tayari kupokea fursa zitakazoletwa katika kipindi hiki ambacho serikali imeamua kuhamishia makao yake hapa Dodoma.
Akizungumza kwa niaba yake, Padri Onesmo Wissi amesema kuwa hakuna sababu ya kuzikataa fursa zitakazoletwa kwa kuwa wakifanya hivyo ni sawasawa na kupinga maendeleo ambayo yanahitaji kwa hivi sasa mkoani hapa.
“Hapo zamani wakati mkoa huu wa Dodoma unatawaliwa na watemi kwenye maeneo mbalimbali, baadhi yao walikuwa wakipinga maendeleo ambayo yalikuwa yakiletwa na wageni kwa hofu ya kudharauliwa madaraka yao, suala ambalo lilisababisha kutokuwepo kwa maendeleo hayo kama vile ya ujenzi wa shule na hospitali,”amesema.


Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI