Wazazi warithisheni watoto elimu-Askofu Nyaisonga asisitiza
WAAMINI wa Kanisa Katoliki wametakiwa kuwaendeleza watoto wao katika
elimu ikiwemo na wao wenyewe
kujiendeleza katika fani mbalimbali ili
waweze kujiajiri kupitia mafunzo
mbalimbali waweze kujitegemea.
Elimu ndiyo hazina pekee na urithi mkubwa kwa familia na jamii kwa
ujumla katika maisha ya sasa na ya baadaye.
Ushauri huo
umetolewa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Mbeya,Mhashamu Gervas
Nyaisonga wakati wa homilia yake katika adhimisho la Ibada ya Misa
Takatifu iliyofanyika katika Kanisa la
Mtakatifu Francisco wa Asiz, Kigango cha Mkwajuni,Parokia ya Mwambani,jimboni
humo.
Walioshiriki
ibada hiyo licha ya waamini wa parokia hiyo, walishiriki pia Wafanyakazi wa
Hospitali ya Mwambani inayomilikiwa na Jimbo Kuu Katoliki la Mbeya, iliyopo
katika Kigango hicho ambako Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Mbeya Mhashamu
Gervas Nyaiaonga alifanya ziara ya kutembelea Hospitali hiyo.
Katika
Homilia yake Askofu Nyaisonga amesema elimu ni hazina kubwa na msingi wa
maendeleo katika familia, jamii na taifa kwa ujumla.
“Wazazi na
walezi wasomesheni watoto wetu kwani katika maendeleo ya sayansi na teknolojia
ni muhimu sana,lakini pia nanyi mkipata
nafasi mjiendeleze kielimu na katika
fani mbalimbali,” amefafanua Askofu Nyaisonga.
Aidha ametoa
wito kwa madaktari, wauguzi na wafanyakazi wa fani mbalimbali katika
Hospitali ya Mwambani kuwahudumia wagonjwa kwa upendo,huruma na unyenyekevu
kadri ya weledi wao bila kujali tofauti za kiimani.
Amesema kazi
waliyoichagua ni wito na utume wa kujitoa
kuwahudumia wagonjwa na wahitaji mbalimbali, hivyo wanapaswa kufuata
nyayo za Muuguzi mwanzilishi Florence Nightingale.
“Muwe watu
wa huruma kwa wagonjwa,muwe wapole,wakarimu na wanyenyekevu na lugha
itakayoweza kuwatia moyo wagonjwa,” amefafanua.
Hata hivyo
amewakumbusha waamini na wakristo umuhimu wa kusali na kumuomba
Mungu katika maisha yao ya kila siku ili aweze kuwafundisha,kuwaongoza na
kuwasaidia katika maisha.
Hospitali ya Mwambani iliyopo makao makuu ya Wilaya ya Songwe,mkoani songwe inamilikiwa na Kanisa Katoliki Jimbo Kuu
Katoliki Mbeya kwa kushirikiana na Serikali.
Comments
Post a Comment