Mkatoliki anayepokea rushwa anaikana imani yake-Ask. Kassala amesema
MAkamu wa Rais Baraza la
Maaskofu Katoliki Tanzania, Askofu Flavian Kassala amewataka waamini wa Kanisa
Katoliki kuiishi imani yao inayomtaka mkristo kuwajibika kwa uadilifu,
kuichukia dhambi yakiwemo masuala ya rushwa.
Amesema hayo wakati wa adhimisho la Misa Takatifu ya Jumapili ya 6 ya
Pasaka katika Kanisa Kuu la Kiaskofu la Watakatifu wote la Jimbo Katoliki
Mtwara
Ametaja baadhi ya mambo ambayo yamekuwa kikwazo katika imani ikiwemo, rushwa, udini,ukabila na umaeneo
ambayo vyote hivyo vimekuwa sababu ya mateso kwa wanadamu wengi katika nyakati
hizi na matokeo yake ni kushuka kwa imani miongoni mwa waamini.
“Haiwezekani jana umepokea rushwa kwa mtu mmoja na leo umekaa karibu
naye kanisani halafu wakati wa kutakiana amani mnashikana mikono ya amani!,”
amesema Askofu Kassala
Kufuatia hali hiyo amewataka waamini kote nchi kuishi kwa kuzingatia
imani yao inayokataza rushwa, chuki, ubaguzi wa dini, rangi, kabila, maeneo nk.
“Imani yetu inasisitiza upendo, msamaha, amani, huruma, uwajibikaji
wenye uadilifu nk,” amesema.
Aidha Kassala amewashukuru waamini na wananchi wa mkoa wa Mtwara kwa
moyo wao wa upendo na shukrani kwa Mungu kwa kujituma katika maandalizi na
kufanikisha maziko ya Marehemu Askofu Mstaafu Gabriel Mmole ambayo yalifanyika
Mei 22 mwaka 2019 jimboni humo.
Amewataka wanamtwara kuendeleza ushirikiano na mshikamano kama
walivyofanya wakati wa msiba wa Marehemu Askofu Mmole.
“Maaskofu wamefurahishwa na maandalizi walioyakuta wakati wa maziko ya
Askofu Mmole na imeonyesha namna wanajimbo kwa kushirikiana na viongozi wa Kanisa
wanavyofanya kazi kwa pamoja na huo ni ukomavu wa iamani,”amesema Askofu
Kassala ambaye pia ni Askofu wa Jimbo Katoliki Geita.
Kwa upande wake mwenyekiti wa halmashauri walei jimbo la Mtwara Paul
werema amewashukuru waamini wote kwa namna walivyojitokeza kwa zaidi ya wiki
mbili katika maandalizi na hatimaye kufanikisha maziko ya marehemu Askofu
Mmole..
Werema amesisitiza kuendelea na umoja katika mambo mbalimbali ya furaha
na huzuni kwa kuwa ni umoja pekee ndio utasaidia kufanikisha kila jambo jimboni
humo.
Hata hivyo mwenyekiti huyo amewataka wanajimbo kuwa tayari kwaajili ya
kupokea ugeni wa kongamono la wawata
kutoka majimbo ya kusini, ambalo litafanyika Mtwara mwezi juni na amewaomba
akinamama wote kushirikiana katika kufanikisha shughuli hiyo.
Comments
Post a Comment