TEC yawataka watunzi wa nyimbo za Kanisa kuzingatia miongozo ya Kanisa
KANISA Katoliki nchini limezidi kuwasisitiza watungaji na
waimbaji wa muziki wa Kikatoliki kuzingatia misingi na miongozo ya Kanisa hilo
badala kuiga mitindo na mahadhi ya
madhehebu mengine.
Rai hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Idara ya
Liturujia ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Mhashamu Salutaris
Libena, katika mahojiano maalum na
KIONGOZI, muda mfupi baada ya kufunga mkutano wa mwaka wa Liturujia Taifa,
uliofanyika jijini Dar es Salaam na kuwashirikisha wajumbe wa Kamati ya Muziki
kutoka Kanda za Kanisa Katoliki nchini, Waratibu wa Liturujia wa Majimbo,
Walimu wa Liturujia katika Seminari Kuu na baadhi ya vyuo vya Makatekista
nchini.
Amesema kuwa kama inavyosisitizwa kwenye Katiba ya
Utume wa Kwaya Katoliki Tanzania (UKWAKATA), mtindo uimbaji ukiwemo utoaji wa
sauti katika muziki Mtakatifu wa Kanisa hilo, haunabudi kuwa wa kiasili au
kibantu na siyo wa kuiga mahadhi ya nje ama ya madhehebu mengine.
“Waimbaji waepuke kuwa kikundi cha burudani kwa
kufuata matendo na mkao wa waamini wote katika maadhimisho ya Liturujia…nyimbo
zenye mahadhi ya kidunia zisitumike katika maadhimisho ya Kiluturujia kwani
hazifadhili dhana ya kuimba vizuri ni kusali mara mbili,” alisisitiza.
Mintarafu
mkutano huo ulioandaliwa na ofisi ya Idara ya Liturujia ya TEC, Mhahsamu
Libena alisema ulilenga kujadili na
kuangalia maendeleo ya Liturujia katika majimbo ya Kanisa Katoliki nchini
pamoja na kupata mrejesho wa utunzi na uimbaji wa muziki Mtakatifu, kwa
kuzingatia Katiba ya UKWAKATA ambayo ilianza kutumika rasmi Desemba 2 mwaka
jana yaani Jumapili ya kwanza ya Majirio.
Alisema kutokana na mrejesho uliotolewa na washiriki
wa mkutano huo kutoka majimbo mbalimbali, unaonesha kuwa waliofuata katiba hiyo
kikamilifu imeleta mafaniko hasa kwa kuwapata wanakwaya sahihi wanaofuata
kanuni na misingi ya Kanisa Katoliki hasa suala la ushiriki wa jumuiya
ndogondogo za Kikiristo.
“UKWAKATA katika ukurasa wake wa 40 ina fomu maalum
inayomtaka mwanakwaya kujaza na ina vipengele mbalimbali kikiwemo kile cha
kufahamika jumuiya anakotoka… kwa kweli waliyoizingatia kikamilifu wameonesha
mafanikio makubwa, “ alisema.
Hata hivyo alikiri kuwa baadhi ya vipengele vya
Katiba hiyo havijafahamika vilivyo, hivyo akatoa rai kwa waratibu wa Liturujia
majimboni kutoa elimu na ufafanuzi kwa wadau wa muziki Mtakatifu wakiwemo
watunzi na wanakwaya ili viweze kueleweka.
Sanjari na hayo, Mhashamu Libena ambaye pia ni Askofu
wa Jimbo Katoliki la Ifakara alisema, licha ya Kanisa Katoliki kuheshimu
Teknolojia ya Mawasiliano, lakini katu halitaruhusu waamini wake kutumia simu
za mikononi na vifaa vingine vya namna
hiyo, kama sehemu ya kufanyia rejea wakati wa Misa na Ibada Takatifu.
“Tunaendelea kutumia Biblia Takatifu na maandiko
mengine yaliyochapishwa kwa kuidhinishwa na Kanisa ambayo tayari yamo katika
maandishi yaliyochapishwa… siyo kuruhusu simu, ipad na vifaa vingine vya namna
hiyo,” amesema.
Akizungumzia msimamo wa Kanisa hilo, Bw. Benjamin
Mshana mwamini wa Parokia Katoliki ya Kibwegere Jimbo Kuu Katoliki Dar es
Salaam, ameunga mkono msimamo huo wa Kanisa kwa kile alichoeleza kuwa kuruhusu
matumizi ya simu wakati wa Misa ni sawa na kumruhusu shetani ambaye bila shaka
atawafanya waamini hao wakose utulivu wakati wa adhimisho la Misa Takatifu
“Unakuta mtu anafungua simu na
anakutana na ujumbe, ni wazi kwamba shetani naye atachukua nafasi yake kwani
hawezi kuacha kusoma ujumbe huo na tayari utulivu wake kanisani unakuwa wa
mashaka,” amesema Bw. Benjamin.
Comments
Post a Comment