Askofu Kassala kutoa rehema kamili kwa wanahija Geita
Askofu wa Jimbo
Katoliki Geita Mhashamu Flavian Kassala amesema atatoa Rehema Kamili “Indulgensia” kwa wanahija watakaohiji katika
Kituo cha Hija cha Nyamatongo Parokiani Nyantakubwa jimboni humo.
|
Akizungumza
katika Misa Takatifu ya Ushemasi wa Frateli Albert Warioba wa Jimbo Katoliki
Geita, Askofu Kassala amesema anatumia uwezo wake aliopewa na Baba Mtakatifu
kutoa rehema kamili kwa baadhi ya wanahija watakaokidhi vigezo Juni 15 mwaka huu vikiwemo kufanya
majuto kamili, kuungama dhambi na kupokea Ekaristi Takatifu na kusali kwa ajili
ya nia za Baba Mtakatifu.
Kituo hicho
kilizunduliwa rasmi mwaka 2017 katika kuadhimisha miaka 100 ya Upadri Tanzania
ambapo Waamini wa Jimbo la Geita walichagua kituo cha Nyamatongo kwa kuwa juu
ya Kilima hicho alifariki Padri Pierre Combarieu na kuzikwa hapo mwaka 1881
baada ya jaribio la kuanzisha Misheni (Parokia) mahali hapo kukwama.
Miongoni mwa
vivutio vinavyochochea mwamko wa kiimani katika Kilima hicho ni Msalaba mkubwa
ulioachwa hapo na wamisionari tangu mwaka 1881 na kaburi la padri huyo
lisiloonekana mahali hapo.
Wenyeji wa
eneo hilo akiwemo mjukuu halisi wa Mtemi Rwoma aliyewapa wamisionari wa
Kifaransa wa shirika la White Fathers ardhi hiyo ambaye bado yupo hapo jina
lake Gabriel Rwoma amesisitiza kuwa eneo liliheshimiwa lisivamiwe na mtu yeyote
mbali ya kuachanizwa kwa zaidi ya miaka 138.
kwa tamko
lake la kuanza kutoka rehema kamili ambayo ni msamaha kamili wa adhabu za
dhambi zote mtu alizotenda kila mwaka kwa washiriki wa hija watakaokidhi
vigezo, Askofu Kassala ameipandisha hadhi hija ya mwaka huu ambapo mamia ya
mahujaji wanategemewa kushiriki, wakiwemo wanakwaya ambao hufanya mashindano ya
nyimbo na kuchangamsha tukio zima.
Hija hiyo ya
Kijimbo iliyoidhinishwa na Askofu Kassala muda mfupi tu baada ya kusimikwa Jimboni
Geita imezidi kuchukua umaarufu baada ya waamini kutoka parokia zote za Jimbo
hilo na baadhi kutoka Jimbo Kuu Katoliki Mwanza kukubali kumiminika kwa wingi
kushudia maajabu ya kilima hicho kila mwaka kwa kusali Misa takatifu, kupata
semina za kiroho, kitubio na mafungo.
Wakizungumza
kwa nafasi tofauti waamini wa Jimbo Katoliki Geita wameahidi kushiriki hija
hiyo kwa wingi ijapokuwa baadhi wamekiri hawakuwahi kufahamu nini maana ya
rehema kamili na hivyo kuwaomba mapadri watoe elimu ya kutosha wakati wa
mahubiri Kanisani ili waamini walewe zaidi jambo hilo.
Comments
Post a Comment