Ask. Nyaisonga: Kanisa litumie vyombo vya habari kuinjilisha
WAUMINI wa Kanisa Katoliki wamealikwa
kuhubiri habari njema kupitia teknolojia mpya ya mawasiliano .
Teknolojia ya sasa mathalani redio,
runinga, mitandao ya kijamii ambapo watu wa kizazi hiki wamehamia humo ndiyo
nyenzo pekee muhimu inayoweza
kutumika kufikisha ujumbe wa Injili.
Hayo yameelezwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki
Mbeya,Mhashamu Gervas Nyaisonga katika homilia yake wakati wa adhimisho la Ibada ya Misa Takatifu
ya uzinduzi wa harambee ya mbio za Mama
Maria(Mariathon ) ambapo Radio Maria Tanzania ilifanya uzinduzi huo kijimbo Mei 5 mwaka huu katika Kanisa la Mtakatifu Patrick,Parokia ya
Vwawa,Mbozi.
Kwa
Mujibu wa Mwakilishi wa Radio Maria Jimbo Kuu Katoliki Mbeya,Thobias Mihale
lengo ya harambee hiyo ni kukusanya
Sh.Mil.35 kwa mwezi mei,ambapo katika
uzinduzi huo zaidi ya Sh.Mil.2.3
taslimu zilipatikana baada ya kuchangwa na waumini pamoja na marafiki wa Radio Maria jimboni humo.
Askofu Nyaisonga amewaalika waamini kutumia nafasi ya kutafakari sababu
ya kupewa kila mmoja kipawa kwa
makusudi yake na kuwasihi waweze
kuvitumia kadri ya mapenzi yake mwenyezi Mungu kwa ajili ya kutangaza na kueneza
habari njema.
“Kila mmoja wetu ameumbwa na kupewa karama yake ili tuweze kutangaza habari njema ya Mungu na watakaoamini waweze
kubatizwa ili waweze kupata uzima wa
milele na kwamba hilo ndiyo kusudio la juu ama wito mkuu wa
kuwafanya watu wote waweze kupata wongofu kupitia habari njema,”amefafanua Askofu Mkuu Nyaisonga.
Amesema kuwa tendo la uenezaji wa habari
njema linakwenda kwa nyakati ambazo
katika zama zilizopita wamisionari
waliweza kutumia karama zao kupita
kuhubiri habari njema kwa wayahudi na mataifa kwa kutumia usafiri wa mnyama aina ya Punda uliowawezesha kusafiri umbali mrefu kutoka sehemu moja kwenda
nyingine.
Nyakati zetu ni tofauti. Tutake tusitake
teknolojia ya habari na mawasiliano
ndiyo nyenzo ya sasa hatuwezi
kurudi kwenye zile zama za kusafiri kwa kutumia punda walivyofanya
wamisionari miaka 150 iliyopita
kuwafikia watu na waliwafikia wachache
lakini sasa wanatakiwa wafikiwe
wengi kwa wakati,” amefafanua zaidi
Askofu Mkuu Nyaisonga.
Ni
nyenzo ambayo inawafikia walio
wengi kwa muda mfupi na muda
muafaka kile ambacho unachokiamini,
unachokipenda kiweze kufikiwa na kupokelewa na wengi kipate mashabiki wengi kama vilivyo vilabu
vikubwa nchini Tanzania Simba na Yanga ambavyo vimekuwa vikipata na kupendwa
na mashabiki wengi ni lazima kuwe na
nyenzo na nyenzo ni hizo haitoshi tu
tukigawa na kuuza vitabu na misalaba,kwanza sisi hatuna desturi ya kusoma vitabu,”
Amesema Mhashamu Askofu Mkuu Nyaisonga.
“Lazima habari njema itangazwe,yatolewe
mafundisho,waamini waijue Katekisimu…habari njema itangaze ili watu iwachome
kwenye dhamiri zao kama wale wazee wa makuhani…itangazwe wasikie hata
wasipokusikia leo watasikia kesho na kesho kutwa ndiyo maana wanakwaya wanaendelea kuimba
kesho na keshokutwa na namna nzuri wasikie kwenye radio,wasikie kwenye nyenzo
nyingine wasome kwenye magazeti ,wasikie kwenye vyombo vingine.
Leo tupo hapa wapo wagonjwa mahospitalini na majumbani,wazee na wasio
jiweza kufika hapa ,walioshindwa kuja
hapa kwa sababu mbalimbali wasikilize kwenye
Radio neno la mungu,mimi siwezi kwenda sokoni kuhubiri lakini wapo nitakaowatuma kwenda kutangaza
kupitia karama zao kwa kutumia nyenzo
kama vyombo vya habari.
Kwa hiyo wakatoliki ndugu zangu tuna
wajibu wa kushuhudia
tunachoamini…kutokutangaza maana yake
hata imani yenyewe ina dosari. Tuna wajibu wa kusimama kidete na kusema kwamba ,ninaamini kwamba huyu aliyechinjwa,huyu ambaye ni pasaka yake ninaishangilia ,huyu aliyechinjwa
anastahili uweza na nguvu hakuna muweza
mwingine, hakuna mwenye nguvu mwingine
,ni huyu huyu anastahili uweza na nguvu
na ndiye atakayenipa nguvu mimi ,”amesisitiza Askofu Mkuu Nyaisonga.
Comments
Post a Comment