Papa: Tunafanyia uchunguzi kashfa ndani ya Kanisa
BAba Mtakatifu
Francisko katika mahojiano maalum na Kituo cha Televisheni cha Taifa nchini
Mexico hivi karibuni pamoja na mambo mengine amezungumzia mauaji ya wanawake
ndani ya familia, ukarimu kwa wakimbizi na wahamiaji; uhusiano kati ya siasa na
uchumi; madhara ya biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya pamoja na
kashfa ya nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo.
Hii ni
sehemu ya tafakari ya kina kuhusu hali halisi ya kimataifa sanjari na maisha na
utume wa Kanisa kadiri anavyoufahamu Baba Mtakatifu Fransisko.
Kuhusu
shutuma za kashfa mbali mbali zinazoendelea kujitokeza ndani ya Kanisa, Baba
Mtakatifu amesema kuwa, wanazifanyia kazi na kwamba, si kila kitu lazima
kitolewe hadharani. Lazima uchunguzi ufanyike na kujiridhisha.
Pia Kanisa
lina nidhamu ya kuendesha kashfa na kwamba halifanyii kazi story za mitandao na
maneno ya kuambiwa. Lazima lifanye uchunguzi wa kina.
Jambo la
msingi ni watu kuwa na uvumilivu, ili kutoa nafasi kwa viongozi wa Kanisa
kufanya uchunguzi wa kina na matokeo kutolewa kwa wakati.
Aidha
amefafanua kuwa pale viongozi wa Kanisa wanapopatikana na hatia, hatua za
kisheria na kinidhamu zinachukuliwa mara moja.
Wakati mwingine, Kanisa linalazimika kukaa
kimya kama alivyofanya Yesu na hapo ni mwanzo wa watu kuchunguza dhamiri zao
ili hatimaye, kuibuka na majibu muafaka.
Mkutano wa Kanisa kuhusu ulinzi wa watoto
wadogo umekuwa na mafanikio makubwa na wengi wameridhishwa na jinsi mambo
yalivyoendeshwa.
Itakumbukwa
kwamba, hivi karibuni, Baba Mtakatifu Francisko katika Barua binafsi “Motu
proprio” ijulikanayo kama “Vos estis lux mundi” yaani “Ninyi ni nuru ya
ulimwengu”: Sheria mpya kwa ajili ya Kanisa Katoliki dhidi ya nyanyaso za
kijinsia; anabainisha sheria, kanuni na
taratibu mpya zinazopaswa kutekelezwa pale kunapojitokeza shutuma za nyanyaso
za kijinsia ndani ya Kanisa.
Maaskofu
mahalia pamoja na wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume wanapaswa
kuwajibika barabara. Kanisa litaendelea kuwa ni Mama na Mwalimu kwa kukazia
toba na wongofu wa ndani, ili watoto wake waweze kuchuchumilia utakatifu wa
maisha.
Pia Papa
Fransisko amesema kuwa, Kanisa litaendelea kuwa ni sauti ya maskini na
Sakramenti ya Wokovu kwa watu wa Mataifa.
Kanisa
litaendelea kuhamasisha ukarimu kwa wakimbizi na wahamiaji sehemu mbali mbali
za dunia kwa kutambua kwamba, leo hii Bahari ya Mediterrania imegeuka kuwa ni
kaburi lisiliokuwa na alama. Mambo makuu manne yanayozingatiwa na Kanisa kwa
ajili ya huduma kwa wakimbizi na wahamiaji ni: kuwapokea, kuwalinda,
kuwaendeleza na kuwashirikisha. Wakimbizi na wahamiaji wakiheshimiwa na
kuthaminiwa wanaweza pia kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya nchi
wahisani anasema Baba Mtakatifu Francisko. Kanisa litaendelea kuenzi Injili ya
uhai dhidi ya utamaduni wa kifo unaofumbatwa katika sera za utoaji mimba, kifo
laini au “Eutanasia”.
Baba
Mtakatifu anakaza kusema si kwamba, Kanisa linahalalisha matendo yao ambayo ni
kinyume cha mpango wa Mungu. Mafundisho msingi ya Mama Kanisa kuhusu ndoa na
familia ni kama yanavyofafanuliwa kwenye Katekesimu ya Kanisa Katoliki ma Wosia
wa Kitume: Furaha ya Upendo ndani ya familia ”Amoris Laetitia” ni habari njema
kwa familia ya Mungu. Katika maisha na utume wake, ataendelea kusimama kidete
kulinda, kutetea na kudumisha Mafundisho ya Kanisa bila kupepesapepesa macho!
Hakuna ndoa ya watu wa jinsia moja!
Comments
Post a Comment