Ask. Kinyaiya:Acheni kuwatafuta masangoma wakati ninyi ni wakristo
ASkofu Mkuu wa
Jimbo Kuu Katoliki Dodoma Mhashamu
Beatus Kinyaiya, amewaonya baadhi ya waamini wenye tabia ya kwenda kwa waganga
wa kienyeji kupeleka matatizo yao.
Amewataka kuachana na imani hiyo mara moja.
Ametoa kauli
hiyo kwenye Ibada ya Misa Takatifu
alipokuwa anatoa Sakramenti Takatifu ya Kipaimara kwa vijana 82 wa Parokia ya Bikira Maria
Msaada wa Wakristo Kizota Jimboni
Dodoma.
Askofu
Kinyaiya amesema kwa kufanya hivyo muumini anakengeuka na hawezi kuishika imani
yake vilivyo kwani atakuwa unatangatanga kiimani.
“Tafadhalini
sana ndugu zangu tuachane na imani hizo kwa wale wanaokwenda kwa waganga wa
kienyeji, Yesu ndiye kila kitu,”amesema Askofu Mkuu Kinyaiya.
Askofu
Kinyaiya, amewaasa vijana waliopokea sakramenti ya kipaimara kuwa askari hodari
wa Yesu Kristo kwa kuilinda na kuitetea imani yao.
Aidha
amewataka vijana hao kuwa waaminifu na wajiandae kupokea masakramenti mengine
yaliyobaki ya ndoa na utawa/ Upadri kwa wale watakaokuwa na wito huo.
Akitoa
tafakari ya somo la kwanza kutoka katika kitabu cha mwanzo Askofu Mkuu Beatus
Kinyaiya amesema, Mungu aliona mahangaiko ya utupu wa mwanadamu ndio maana
alimleta mwanae Yesu Kristo kuja kutusitiri.
Askofu
Kinyaiya amekaza na kusema kwa mazingira ya kawaida na ya kimaumbile utupu haukubaliki, hivyo kutokana na dhambi
walizozitenda Adam na Eva bustani ya
Edeni walijikuta wapo utupu na kuanza kuhangaika kujisitiri.
“Wapendwa Taifa la Mungu ninawaombeni
mumkabidhi Mwenyezi Mungu maisha yenu jumla kwani tukimkabidhi hakuna
kitakachotuyumbisha katika maisha ya hapa duniani,” Askofu Kinyaiya amesema.
Katika hatua nyingine amewataka waamini wa Jimbo Kuu
Katoliki Dodoma kuhakikisha kuwa wananunua Biblia Takatifu na kuzisoma kwani
kupitia Maandiko Matakatifu yaliyopo katika Biblia hizo wataweza kujua habari
njema za wokovu.
“Nawaombeni mnunue biblia na mtenge muda wa
kuwashirikisha watoto wenu neno la Mungu” ameongeza Askofu Kinyaiya.
Aidha
amehitimisha homilia yake kwa kuwakemea wale wote wenye tabia ya kudanganyika
na mafundisho ya baadhi ya watu wa imani nyingine kwamba watakapokwenda
kuombewa na wao watapata ajira, uponyaji, watabarikiwa katika shughuli zao, na
wengine hata kuwarubuni kuwauzia maji ya baraka .
Comments
Post a Comment