Kadinali Pengo aonya waamini wavivu
Askofu
Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es salaam Mwadhama Palycarp Kadinali
Pengo amewaonya watu mbalimbali wanao watumikisha wenzao katika kufanya kazi
kwa manufaa yao huku wao wakiwa mawestarehe.
Kadinali
Pengo amesema hayo katika Ibada ya Misa Takatifu ya Mtakatifu Yoseph
iliyoandaliwa na wanaume wa katoliki (UWAKA) na kufanyika katika viwanja vya
hija Pugu Dar es salaam.
“Wapo watu
ambao wamekuwa wakiwatumikisha wenzao kazi ili hali wao wameketi bila hofu
yoyote na wakiwa wamesahau sauti ya Mwenyezi Mungu anamtaka kila mmoja kutafuta
chakula chake kwa jasho.
Mwenyezi
Mungu aliwaambia wazazi wetu kuwa kwa jasho lao watapata chakula, hivyo kila
mmoja wetu afanye kazi bila kumtumikisha mwenzake huku tukiendelea kujifunza
kwa Mtakatifu Yoseph ambaye licha ya kupewa jukumu la kumtunza Mungu aliendelea
na kazi yake ya useremala na pengine tungejiuliza kwa nini hakukaa raha
mstarehe badala yake aliendelea na kazi yake,” ameeleza.
Ameongeza
kuwa Mtakatifu Yoseph alipopewa jukumu la ulinzi wa mtoto Yesu angeweza kuomba
kwa Mwenyezi Mungu amfanyie kitu ili maisha yao ndani ya familia yawe mazuri na
aachane na shughuli za useremala.
Lakini hakufanya hivyo bali anatufundisha
kufikiria wengine kwanza kwa kuona ni lipi la manufaa kwao kama Yesu alivyoacha
yote na kuwatazama vipofu, viwete, na wakoma kwa kuwapa tumaini ya kutembea
tena na kuona tena.
Amesema kila
mtu anapaswa ajifunze kupitia kwa mtakatifu Yoseph kufanya kazi hata ile
inayodharauliwa kwenye jumuiya ya watu ili itupatie riziki na kuwasaidia
wengine wasioweza kufanya kazi.
Aidha
Kadinali Pengo amewataka wanaume Katoliki kufanya kazi na kushirikiana kwa
pamoja huku wakiisikia sauti ya Mungu kwa majitoleo ya hali na mali katika
kukijenga kituo cha Hija Pugu ili kiwe eneo bora Afrika Mashariki kwa watu
kufika na kuja kufanya Hija.
Wakati huo
huo Padri Raymond Mbaula anayehudumu katika Seminari ya Visiga na Paroko
Msaidizi wa Parokia ya Mlandizi kwa pamoja wamewaongoza wanakwaya wa Mtakatifu
Yoseph Kigango cha Visiga katika kusherekea somo wa kwaya hiyo sherehe
zilizofanyika kigangoni hapo na kuhudhuriwa na kwaya mbalimbali ikiwemo kwaya
ya Gabriel Malaika Mkuu kutoka Parokia ya Roho Mtakatifu Segerea sanjari na
kwaya za Kristo Mfalme, Mtakatifu Maria na Mtakatifu Sesilia zote kutoka
Parokia ya Mlandizi.
Comments
Post a Comment