TAARIFA KWA UMMA:TAMKO LA BARAZA LA MAASKOFU KATOLIKI JUU YA KONGAMANO LA EKARISTI TAKATIFU JIMBO KUU MWANZA JUNE 9-11-2016



TAMKO RASMI LA KONGAMANO LA EKARISTI TAKATIFU JIMBO KUU MWANZA 2016



Sisi Maaskofu, Mapadre, Watawa na Waamini wote Kutoka majimbo Katoliki Tanzania, tuliokutana katika viwanja vya  Bikira Maria Malkia wa Kawekamo kwa madhumuni ya kuadhimisha Kongamano la tatu (3) la Ekaristi Takatifu Kitaifa (Juni 8 mpaka 11 mwaka  2016). Kwa taswira nzuri mithili  ya ile  ya  kugeuka sura kwa  Bwana wetu Yesu Kristo pale mlimani  Tabor, na mithili ya wanafunzi wa Emaus waliomtambua Yesu katika kuumega mkate, tunapenda kuinua shukrani yetu kwa Mungu anayetupatia mwanae kuwa chakula cha safari yetu kuuelekea ufalme aliotuhaidia.

Baada ya kusali na kutafakari kwa kina juu ya neema na Baraka  ziletwazo na Ekaristi Takatifu, tunauhakika kwamba Roho Mtakatifu anatutuma sasa, kwenda kumtangaza na kumshuhudia Yesu wa Ekaristi Takatifu. Tukiongozwa na kauli mbiu “Kristo ndani Yenu Tumaini Letu la Utukufu, tumeitafakari Ekaristi kwanza kama;

Mkate wa Uumbaji: Ekaristi Takatifu, ikiwa inaishi na kuleta uhai hukutana nasi tunaoipokea, na yenyewe inakuwa ukamilifu kabisa wa fumbo la Pasaka ambalo ni msingi wa kweli na ni kichocheo cha Uongofu binafsi. Hili fumbo linatuimarisha sisi katika imani. Ni katika ekaristi kila kiumbe kinapata uhai, furaha ya kweli, na Ekaristi Takatifu inatuhimiza kuutunza uumbaji kama shukrani yetu kwa Mungu aliyeumba mbingu na dunia na vitu vyote vinavyoonekana na visivyoonekana.

 

Mkate kwa Utukufu: Ekaristi Takatifu ni ushuhuda wetu sisi waamini wakatoliki kuhusu, mateso,kifo na ufufuko wa Bwana wetu ambaye ametuachia ukumbusho wa mateso yake na fursa ya kumpokea yeye katika fumbo la Ekaristi.

Ekaristi Takatifu ni chanzo cha wito na matumaini yetu ya utukufu,pia ni mkate wetu wa matumaini kwa vile hutupatia nguvu ya kuishi kwa kutoa shukrani na furaha ijapokuwa maisha yetu hukabiliwa na changamoto nyingi.Pamoja na changamoto hizo, katika Sakramenti ya  Ekaristi Takatifu, Mungu anakuwa pamoja nasi,anatuokoa, anatutawala na kututakatifuza.

Ekaristi Takatifu kwa hiyo itujengee ari ya kutulia na kutafakari safari ya maisha yetu na humo tuchote nguvu za kuendelea mbele kwa uthabiti wa maisha.

Mkate wa mazungumzano: Ekaristi Takatifu   ni kiunganishi kati ya Mungu na uumbaji,:Mungu na watu, :watu kwa watu. Kwa muktadha huo  Ekaristi Takatifu inatupa nguvu  ya mazungumzano ndani yetu,katika familia,jumuia ndogondogo  na inatusukuma kuwa wahudumu wa Ekaristi katika kanisa, tukijenga misingi ya ekumenia, tukijenga misingi ya mahusiano na dini mbalimbali tamaduni mbalimbali na ulimwengu mzima. Ekaristi Takatifu siku zote itusaidie  tusiishi kinadharia  bali tuishi matendo ya injili  kila siku kama kanisa la mwanzao  “…na siku zote kwa moyo mmoja walidumu ndani ya hekalu, wakimega mkate nyumba kwa nyumba na kushiriki chakula chao kwa furaha na kwa moyo mweupe Mdo. 2:46”



Mkate kwa misioni: Baada ya kuvuviwa na kuhuhishwa na Ekaristi Takatifu katika viwanja vya Bikira Maria Malkia wa Kawekamo  tunaalikwa kuwa wamisionari wakristo wanaotumwa katika majimbo yetu na Tanzania kwa  ujumla kuwa Mkate unaomegwa kwa ajili ya kuiletea uhai Dunia inayomeguka. Katika umisioni huo sisi sote tuliokuwepo hapa tunalo jukumu la kimisionari; ni dhahiri kwamba kongamano la Ekaristi Takatifu  la kitaifa la mwaka 2016 ni wito wa kimisionari kwetu sote kwa sababu kama tulivyotafakarishwa Ekaristi yetu ni chemichemi ya msamaha kitubio. Kama tulivyotafakarishwa Ekaristi ni msingi wa kujenga familia; ni msingi wa namna ya kumpokea Bikira Maria kama mama wa Ekaristi na kutufundisha. Hivyo Ekaristi yetu ni chemchemi  na lengo la umisionari wa kanisa.

Umisionari kwa nafsi zetu, kwa familia zetu, kwa wasiomjua Kristo bado, kwa wanaoteswa na kuteseka, kwa wanyonge, na kwa wasio na matumaini; umisionari wa kujitakatifuza katika Sakramenti ya Upatanisho, na umisionari kupitia vyama vyetu vya kitume.  



Mwisho kwa Mama Mbarikiwa, Mama wa Ekaristi, tunalikabidhi kanisa zima nchini Tanzania, tunaweka chini ya ulinzi wake.

Ee Mama mwenye kulilinda kila jimbo, kila parokia na kila familia , tufundishe kuipokea, kuiishi, kuitetea na kuishuhudia Ekaristi Takatifu kila tutakapokuwa. Tunamuomba Mama yetu Malkia wa Kawekamo, alilinde jiji la Mwanza na watu wake, na alilinde Taifa zima la Tanzania ili amani, haki, upendo, heshima kwa hadhi na utu vidumu na kutawalahapa na nchini kote.



 KRISTO  NDANI YENU,TUMAINI LETU LA UTUKUFU

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU