SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU NA JUBILEI YA MAPADRI




Tunaadhimisha Jubilei maalum ya Mwaka wa Huruma ya Mungu ambayo ilizinduliwa rasmi na Papa Fransisko mwaka jana Desemba 8 Sherehe ya Bikira Maria Imakulata. Katika ratiba maalum aliyoiweka Papa Fransisko katika maadhimisho hayo ni pamoja na tarehe ya Jubilei ya Mapadri tarehe 1-3 Juni Sherehe ya  Moyo Mtakatifu wa Yesu. Mapadri watumie nafasi hiyo kuadhimisha huruma ya Mungu na kujipatanisha na Mungu. Basi tutumie nafasi hii kutafakari kuhusu Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu.
Msingi wa Sherehe
Sherehe hiyo huadhimishwa siku ya Ijumaa baada ya Dominika ya  Sherehe ya Mwili na Damu takatifu ya Bwana wetu Yesu Kristo. Imechaguliwa siku ya Ijumaa, ni siku aliyouawa Bwana wetu Yesu Kristo alipoonyesha kilele cha upendo wake kwetu kama yeye mwenyewe alivyosema. “Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake”(Yn 15:13).
Tunapotafakari na kufuatia historia ya  Sherehe yenyewe tunaona  inatokana na kuwa na Ibada  kubwa kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu. Kutokana na Wakristo kumheshimu Bwana wetu Yesu Kristo, Mungu mtu, kwa ajili ya upendo wake mkuu kwetu wanadamu, upendo ambao ishara yake ni moyo wake mtakatifu, hatimaye tunayo
 Sherehe hiyo.
Mababa wa Kanisa
Tayari katika karne za kwanza enzi za Mababa wa Kanisa waliziona sehemu fulani katika Injili kama ishara ya upendo mkuu wa Yesu kwetu wanadamu. Kwa mfano Yesu anapowaalika wale wanaoelemewa na mizigo wamwendee: “Njoni kwangu ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jitieni nira yangu... nanyi mtapata raha nafsini mwenu”.(Mt 11;28-30).  Katika Injili ya Yohane Yesu huwaalika wanaoona kiu waende kwake: “Mtu akiona kiu, na aje kwangu anywe” (Yn 7:37). 
Tena, Mababa hao wa Kanisa walitafsiri tendo la Yesu kuchomwa ubavu wake kwa mkuki na kutokwa damu na maji kuwa ishara ya upendo wake mkuu kwetu wanadamu(Yn 19:34). Kujibu  upendo mkuu wa Yesu kwetu wanadamu walianza kuwa na sala maalum kuonyesha kwamba wanampenda Yesu. Kwa kuwa moyo ni kielelezo cha upendo basi mpango huo wa sala ukapata jina Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu.  Baadhi ya watakatifu  wa karne ya kumi na mbili kama Anselmo wa Canterbury(1033-1109) na Bernardo wa Kleovoo Abate (1090-1153) walikuwa na  Ibada kubwa kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu.
Kadiri miaka ilivyoendelea Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu ilipata nguvu na kuenea. Katika karne ya kumi na tatu tunaona watakatifu wengi waliadhimisha Ibada hiyo. Baadhi yao walijaliwa kutafakari upendo wa Mungu  na kusali kwa namna ya pekee na hata kujaliwa maono. Katika karne ya kumi na sita Shirika la Wajesuiti waliieneza Ibada hiyo na kuwahimiza watu kusali.
Katika karne ya kumi na saba watawa wa huko Ufaransa kama Mt.Yohane Eudes (alifariki 1680) waliiimarisha kwa dhati na kuieneza Ibada kwa Moyo  Mtakatifu wa Yesu. Kwa ruhusa ya Askofu wake Mt.Yohane Eudes alikuwa kuhani wa kwanza kuadhimisha sikukuu ya Moyo Mtakatifu wa Yesu. Aliruhusiwa kuadhimisha sikukuu hiyo 20.10.1672 lakini katika makanisa ya utawa wake tu kwani mpaka hapo sikukuu hiyo ilikuwa haijatangazwa.
  Mt Margareti Alakoki
Historia ya Sherehe hiyo hatimaye ilifikia kilele chake katika maono aliyopata Mt.Margareti Maria Alakoki (Alacoque) kati ya miaka 1673 mpaka 1675. Yeye alikuwa mtawa wa Shirika la Maonano (Visitation Sisters) huko Ufaransa na alipata kutokewa na Yesu Kristo mara kadhaa akimtaka aombe kuanzishwa kwa sikukuu ya Moyo mtakatifu wa Yesu. Katika maono hayo alielekezwa sikukuu iadhimishwe Ijumaa ya oktava ya sikukuu ya Mwili wa Kristo ambayo sasa inaitwa Sherehe ya Mwili na Damu takatifu ya Yesu. Pamoja na Sikukuu hiyo Mt. Maria Margareti Alakoki aliambiwa kuhusu kusali na kupokea Ekaristi siku za Ijumaa na pia kuabudu Ekaristi kwa saa moja.
Taarifa hiyo ya Mt.Margareti Maria Alakoki ilipofika katika uongozi wa Kanisa huko Roma, haikupokeleka mara. Ilichukua karibu miaka mia mpaka Papa Klementi wa kumi na tatu(XIII) alipoanza kuonyesha dalili za kukubali.  Wakati huo wote watu waliendelea kuwa na Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu. Mwaka 1765 Papa Klementi aliwaruhusu Maaskofu wa Poland na Wakuu wa  Undugu wa Moyo Mtakatifu wa Yesu kuadhimisha sikukuu hiyo. Ulikuwa mwaka 1856 Papa Pius wa tisa (IX) aliitangaza sikukuu ya Moyo mtakatifu wa Yesu  iadhimishwe popote katika Kanisa.
 Baadaye kidogo mwaka 1899 Papa Leo wa kumi na tatu (XIII) aliipandisha hadhi yake  na kuagiza kila nchi iwekwe chini ya ulinzi wa Moyo Mtakatifu wa Yesu. Papa  Pius wa kumi na moja (XI) mwaka 1928 aliipandisha tena hadhi ya sikukuu hiyo baada ya kuifanyia marekebisho. Aliiweka kuwa sherehe  ingawa ilibaki kuwa  sikukuu ya hiari  na wala si ya amri, yaani haiwalazimu waamini wote kushiriki kusali siku hiyo.
Kwa hiyo tunaona Sherehe hiyo ilivyopitia hatua mbalimbali kihistoria mpaka kufikia hatua iliyopo sasa tunapoiadhimisha. Mapapa mbalimbali wamekuwa wakiipa heshima sikukuu hiyo kadiri miaka ilivyokuwa ikienda. Miaka mia moja baada ya Papa Pius wa tisa kuitangaza iadhimishwe pote katika Kanisa, yaani 1956 halifa wake Pius wa kumi na mbili (XII) aliandika waraka maalum kusahihisha mawazo ya wapinzani wa sikukuu hiyo. Waraka huo  unajulikana kwa jina lake katika lugha ya kilatini: Haurietis aquas yaani Mtachota maji. Papa anapinga mawazo potovu ya wale waliokuwa wanaibeza Sherehe hiyo.
Liturujia ya Sherehe
Katika marekebisho ya Mtaguso mkuu wa pili wa Vatikano matini  yamekuwa hasa yale ambayo yaliidhinishwa na Papa Pius wa kumi na moja (XI). Kabla yake mkazo ulikuwa katika mateso ya Bwana kumbe sasa mkazo ni mapendo makubwa ya Kristo kwetu ambayo yamejidhihirisha katika kutukomboa na kutuondolea dhambi zetu.
Mpango wa masomo ya Misa ni kama Sherehe nyingine yaani masomo matatu katika  miaka mitatu. Masomo yanasisitiza mapendo aliyokuwa nayo Mungu kwetu sisi wanadamu. Katika Agano la Kale Mwenyezi Mungu alionyesha mapendo hayo kwa taifa lake la Israeli.Kumbe katika Agano Jipya mapendo ya Mungu yamefikia kilele na kuonekana kwa njia ya Mwanae Yesu Kristo alipokubali kujitoa kuteswa na hatimaye kuuawa kwa ajili yetu. Mwinjili Yohane anaelezea kilele cha mapendo ya Mungu kwetu anaposema: “Kwa maana jinsi hii  Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu  amwaminiye asipotee bali awe na uzima wa milele”(Yn 3:16).
Katika kuadhimisha Sherehe hii mwaka huu tunaadhimisha pia Jubilei maalum ya Huruma ya Mungu kwa Mapadri. Basi waamini wote wanapaswa kuwaombea  Mapadri ili waweze kutenda vema utume wao. Wanapowahubiria wengine  wenyewe  wajitakatifuze, wawe watakatifu. 

Comments

Post a Comment

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI