‘Ukristo ni vita’ Ask. Amani

Na Erick Paschal, Moshi
WAKRISTO wakatoliki nchini wametakiwa kutambua kuwa ukristo ni vita na mapambano ambapo maisha ya hapa duniani ni ya muda kwa ajili ya kujiandaa na maisha ya milele.
Rai hiyo imetolewa na Askofu Mkuu Isaac Amani wa Jimbo Kuu Katoliki Arusha wakati akitoa homilia yake kwenye adhimisho la Misa Takatifu ya kilele cha Jubilei ya miaka 150 ya Uinjilishaji Tanzania Bara kanda ya kaskazini, Misa iliyoambatana na sherehe ya Bikira Maria mpalizwa mbinguni.
Askofu Amani amesema kuwa mpango wa Mungu mara zote ni kumuokoa mwanadamu, na maovu anayoyatenda mwanadamu yanakwenda kinyume na mpango wa Mungu, kwa kuwa Mungu anashughulikia wokovu kwa sababu binadamu ana thamani mbele yake.
Askofu Amani amesisitiza kuwa kila mwanadamu hana budi kujitathmini na kujichunguza kwani mpango wa Mungu siku zote ni wokovu hivyo kila mmoja ana wajibu wa kujiuliza kama ni wakala wa Mungu ama wa shetani kwa matendo.
Vijana ni zamu yenu kuwa wamisionari
Wakati huo huo vijana na watoto wakatoliki nchini wametakiwa kuienzi roho ya kimisionari, ili siku moja wote wakutane mbinguni.
Wito huo umetolewa na Askofu Rogath Kimaryo wa Jimbo Katoliki Same wakati akitoa salamu katika Misa ya Kilele cha miaka 150 ya Ukristo Tanzania Bara kanda ya Kaskazini.
Askofu Kimaryo amesema kuwa roho ya kimisionari ni roho ya kanisa na ni asili yake, hivyo ameomba roho hiyo iwaguse vijana wote wa kike na wa kiume ili wazaliwe wamisionari wapya.
Katika hatua nyingine Askofu Kimaryo amewataka mapadri hasa wa majimbo nao kujenga roho ya kimisionari akisema kuwa lazima mapadri wawapende wamisionari, vijana, masista ili wazidi kuieneza habari njema ya wokovu kwani hiyo ndiyo furaha ya injili.
Naye Msimamizi wa Kitume  wa Jimbo Katoliki Moshi Padri Deogratias Matika ametoa rai kwa waamini  kuzingatia sakramenti zote saba walizopewa na Kristo hasa zile zinazowahusu na kuacha kuutafuta unafuu.
Padri Matika amesema kuwa kila mmoja akisimama kwa kile alichofundishwa akiwa kama mklero, muumini mkatoliki na mtawa basi ufalme wa Mbinguni ni juu ya kila mmoja.
Misa ya Kilele ya miaka 150 ya Uinjilishaji Tanzania Bara, kanda ya Kaskazini imefanyika katika Parokia watakatifu Malaika wakuu Himo, Jimbo Katoliki la Moshi na imeongozwa na Askofu Mkuu Isaac Amani wa Arusha, Askofu Rogath Kimaryo wa Same, Askofu Antony Lagwen wa Mbulu na Msimamizi wa Kitume wa Jimbo Katoliki la Moshi Padri Deogratias Matika.


Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU