‘Jubilei ni azimio la kuanza upya wa maisha, siyo idadi ya miaka’
IMEELEZWA kuwa jubilei
siyo tu idadi ya miaka fulani, bali ni azimio la kuanza upya wa maisha katika
kuelekea ukamilifu na utakatifu. Hayo yamesemwa na Abate wa Abasia ya
Hanga-Songea, Abate Octavian Masingo wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu ya
uzinduzi wa Jubilei ya Miaka 50 ya Shirika la Masista wa Mtakatifu
Agnes-Chipole, Nyumba ya Mtakatifu Getrude Imiliwaha.
|
Akitoa
homilia katika adhimisho hilo Abate Octavian amesema kuwa katika kipindi cha
jubilei masista hao hawana budi kuweka mikazo na mikakati thabiti kuelekea
katika kilele huku mkazo ukiwekwa katika kutathmini hali halisi ya wito wao
badala ya kujikita katika kuhangaikia vitu.
“Mnapoizindua
jubilei hii mnaazimia kuanza upya maisha yenu ya kiroho. Inawapasa kunuia
kuelekea katika utakatifu na ukamilifu” ameeleza.
Aidha
ameongeza kuwa maandalizi ya kuelekea kilele cha jubilei hiyo hayapaswi
kujikita katika vitu kwani kufanya hivyo ni kupotosha dhamira ya kumshukuru
Mungu. Badala yake ameshauri kuwa maandalizi hayo yaendane na uwajibikaji na
utendaji mpya katika kumshukuru Mungu.
“Tendo
la uzinduzi huashiria shukrani kuelekea katika utimilifu. Mumtegemee Mungu kwa
sababu amewabeba na kuwasaidia hata sasa na hata kufikia utimilifu wa maisha
yenu na kazi yenu ya uinjilishaji” ameongeza.
Misa
ya uzinduzi wa Jubilei hiyo imeongozwa na Askofu wa Jimbo Katoliki Njombe
Mhashamu Alfred Maluma katika nyumba ya Mtakatifu Getrude Imiliwaha.
Comments
Post a Comment