KUELEKEA KILELE CHA JUBILEI KUU – ARI YA KICHUNGAJI MUHIMU

Katika kuadhimisha Jubilei ya miaka mia moja na hamsini ya Uinjilishaji, Kanisa Katoliki Tanzania linamshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kuwatuma Wamisionari kuja kutangaza Injili Tanzania. Kwa kuzingatia jinsi Wamisionari walivyojitoa katika kutangaza Injili, na kupambana na changamoto mbalimbali, Kanisa la Tanzania linapaswa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa Uinjilishaji wa miaka hiyo mia na hamsini.

Awamu za Uinjilishaji
Wataalamu wa historia hutueleza kwamba katika Afrika ya Mashariki, Uinjilishaji wa kwanza ulifanywa na Wamisionari wa shirika la Mtakatifu Agustino mnamo mwishoni mwa karne ya kumi na tano. Wamisionari hao walifuatana na mvumbuzi mashuhuri aitwaye Vasco da Gama, na walifika Zanzibari 1499 na lengo lake lilikuwa kutafuta njia ya kwenda India na mashariki ya mbali.
Katika kuinjilisha, wamisionari hao walipata upinzani mkubwa kutoka kwa Waarabu.  Walijitahidi kuendelea lakini mnamo mwaka 1698 Uinjilishaji huo ni kama ulififia. Sababu kubwa ya kushindwa ni  kutokana na uvamizi wa Waarabu kutoka Omani. Waarabu hao walikuwa na nguvu na kuweza kutawala sehemu hizo za pwani.
Uinjilishaji wa awamu ya pili ndio ulioanza katika karne ya kumi na tisa. Wamisionari wa shirika la Roho Mtakatifu walifika kwanza Zanzibari mwaka 1863. Licha ya kupata upinzani mkali, Wamisionari hao hawakukata tamaa. Mwaka 1868 walifika Bagamoyo na kuanza Uinjilishaji Tanganyika. Kama tulivyoona katika mada nyingine, walihubiri Bagamoyo na ujirani wake baadaye waliendelea kaskazini mwa Tanganyika mpaka kufika sehemu za Moshi na Arusha. Licha ya kupata changamoto ya hali ya hewa na maradhi mbalimbali na wengine wao kufariki, hawakukata tamaa hata kidogo. Waliendelea kufika na kuhubiri Injili. Baadhi ya watumwa waliokuwa huru na kuwa Wakristo,  waliwasaidia wamisionari hao kama makatekista.
Miaka kumi baadaye, mwaka 1878 shirika la Mababa Weupe  lilifika Zanzibari na baadaye Bagamoyo. Kutoka hapo  Bagamoyo waliamua kuelekea upande wa magharibi mwa Tanganyika mpaka kufika sehemu za Tabora. Hapo waligawanyika katika makundi mawili. Kundi moja lilielekea kaskazini mpaka sehemu za ziwa Viktoria, na kundi jingine liliendelea kwenda magharibi mpaka  ziwa Tanganyika.
Wamisionari walioelekea kaskazini waliweza kuinjilisha sehemu za Mwanza  na ujirani, kumbe wale walioelekea magharibi  waliweza kuinjilisha Kigoma na ujirani wake; baadaye walielekea kusini mpaka sehemu za Mbeya. Hata hao walipata changamoto za kuumwa na hali ya hewa iliyowaletea adha mbalimbali. Hata hivi Mwenyezi Mungu aliwajalia uvumilivu, waliendelea kuhubiri Injili bila kukata tamaa;  katika  bidii na ari yao  waliweza kwenda hata nchi jirani za Rwanda na Burundi na sehemu ya mashariki ya Kongo.
Kama tulivyokwishasema kwa nafasi nyingine, shirika la tatu katika awamu hii ya pili ya Uinjilishaji walikuwa wamisionari wa Mtakatifu Benedikto kutoka Ujerumani. Hao walifika Dar es Salaam mwaka 1887, miaka kumi baada ya kufika wamisionari wa shirika la Mababa au Mapadri Weupe. Shirika hilo, baada ya kufika Dar es Salaam waliweka kituo chao Pugu. Kutoka Pugu walielekea kusini wakipitia sehemu za Dodoma na  Mahenge. Vituo vikuu huko kusini mwa Tanganyika vilikuwa Tosamaganga karibu na  Iringa, Ndanda karibu na  Masasi na Peramiho karibu na mji wa Songea. Walichagua kuweka vituo vikuu nje ya mji ili kutojihusisha na mambo ya kisiasa, watu waone  tofauti kati yao na wazungu wa serikali.

Ari ya Wamisionari
Hapana shaka wamisionari walikuwa na ari kubwa ya kichungaji. Walitoka nchi za mbali kuja Tanzania na kupambana na changamoto mbalimbali siyo kwa ajili ya  kutalii bali kwa ajili ya kazi moja tu ya kuhubiri Injili. Kwa sababu hiyo walitafuta njia mbalimbali kuifikisha imani ya Kikristo kwa watu. Kwa mfano walianzisha shule za awali  vijijini na kuwafundisha watoto kusoma na kuandika, lakini waliwafundisha pia imani, namna ya kusali na mafundisho ya katekisimu.
Wamisionari wa Mtakatifu Benedikto walioinjilisha kusini mwa Tanzania, kwa mfano, walifika katika timu au umoja na kila mmoja akiwa na majukumu yake. Walikuwa mapadri, masista na pia watawa wakiume walioitwa mabradha au mabruda. Neno bruda linatokana na neno la kijerumani  der bruder maana yake kaka. Bruda alikuwa mtawa mwanamume asiye padri.
Mapadri walijishughulisha na uchungaji, yaani: kufundisha katekisimu mashuleni, kuadhimisha sakramenti na kutembelea vijiji kuadhimisha Ekaristi. Walikuwa na ratiba katika kuhakikisha wanavitembelea  vijiji au vigango vyote katika uchungaji. Masista kwa upande wao waliweza kufundisha pia mashuleni, na kuwafundisha wasichana kwa kazi za nyumbani. Sista mmoja aliangalia usafi wa kanisa na maandalizi ya mavazi ya misa. Mwingine alikuwa mpishi na kuwa na bustani; huyo alihakikisha chakula  kinapatikana kwa wakati wake kwa ajili ya jumuiya yote.
Mabradha walikuwa na kazi za nje kama ujenzi, ufugaji na useremala. Hao pia walikuwa na wafanyakazi, kabla ya kuanza kazi wafanyakazi walipata katekesi fupi kisha walisali pamoja ndipo kila mmoja alielekea sehemu yake ya kazi na kuanza kazi. Mchana walipofunga kazi ilitolewa alama na wote walikusanyika ili kusali pamoja kisha kuondoka. Kila mmoja alitimiza wajibu wake ili wawe na afya njema.
Utaratibu wa kusali na wafanyakazi wao kabla ya kuanza kazi ulikuwa ni sehemu ya  Uinjilishaji ambao hata masista waliutumia. Sista mpishi alisali na wasichana waliomsaidia jikoni kabla ya kuanza rasmi kazi za jikoni. Walipokwenda shambani au bustanini sista alianzisha  sala fupi kabla ya kuanza kazi. Kama kaulimbiu yao inavyosema: Ora et Labora yaani Sala na Kazi ndivyo wamisionari walivyowafundisha wafanya kazi wao kuwa na bidii katika kusali na kufanya kazi. Kwa njia hiyo masista na mabradha waliungana na padri katika uchungaji; kuwahimiza waamini kusali na  kumtegemea Mungu katika maisha.

Ari ya Uwajibikaji
Kuadhimisha Jubilei kuwe fursa ya kuamsha ari ya kichungaji. Kutokana na mazingira tofauti, kuhani au katekista hushawishika kufanya mambo muhimu tu katika uchungaji, kama vile kuadhimisha Ekaristi na kuwahudumia wagonjwa katika hatari ya kufa. Hutumia muda mwingi kati ya juma kufanya kazi za kimaendeleo kama vile mashambani  au miradi mingine ili wapate fedha ya kujikimu.
Katika parokia nyingine, hata hivi jambo hilo linatekelezwa; waamini wanahakikisha kuhani anapata chombo cha usafiri, chakula na mahitaji muhimu pamoja na pesa kwa matumizi yake binafsi. Wakristo huhakikisha pia makatekista wanapata mahitaji yote muhimu. Katika mazingira hayo wachungaji inawapasa kutumia muda mwingi kufanya uchungaji ili kuwaimarisha waamini katika imani. Ari na bidii waliyokuwa nayo wamisionari, iwahimize waamini, kwa nafasi hii,  kuhakikisha wachungaji wao  wanapata chakula na mahitaji muhimu ili watumie muda wao zaidi kwa  ajili ya Uinjilishaji. Wachungaji nao wakisukumwa na ari ya Wamisionari wawajibike katika Uinjilishaji, tena Uinjilishaji wa kina.


Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU