Ufahamu juu ya tatizo la homa ya ini

Na Josephat Wangwe

TUNGALIKUA na mazoea ya kujali afya zetu na kujituma kwa moyo mkuu katika kuzitunza na kuziboresha kama tunavyotunza vitu vyetu vya thamani (Majumba, magari, simu, nk), basi gharama za matibabu tuzipatazo kila mwaka katika taifa letu zingepungua kwa kiasi kikubwa.
Lakini kutokana na muitikio hafifu tulionao katika mambo yahusuyo afya basi tumejikuta tukilazimika kuishi na magonjwa mbalimbali ndani ya miili yetu, mengine yanaoneka waziwazi na mengine huwa yamejificha ndani ya miili yetu yakitumaliza kidogo kidogo.
Homa ya ini (hepatitis) ni hali ya kuwepo kwa uvimbe (Inflammation) katika ini. Homa ya ini hutokana na sababu mbalimbali, Virusi vya homa ya ini ndio sababu kubwa kati ya sababu zinazopelekea kutokea kwa tatizo la homa ya ini. kuna aina tano (5) za ugonjwa wa homa ya ini zinazotambulika duniani yaani A,B,C,D na E ( Hepatitis A,B,C,D pamoja na E).
Utofauti huu unatokana na aina ya kirusi kilichomuingia mtu husika (Hepatitis A virus-HAV, Hepatitis B virus-HBV, Hepatitis C virus-HCV, Hepatitis D virus-HDV, pamoja na Hepatitis E virus-HEV). Sababu nyinginezo kama ugonjwa kutokana na hali ya mfumo wa mwili (Autoimmune diseases), matumizi ya pombe, nk zitatajwa katika makala hii.
“..., Kwa ujumla homa ya ini aina B pamoja na aina C (Hepatitis B na Hepatitis C) imewapata watu takribani milioni 325, lakini kati ya hawa wote ni mtu mmoja tu (1) kati ya watu kumi (10) aliyepimwa homa ya ini, vile vile ni mtu mmoja tu (1) kati ya watu watano (5) aliyepimwa na kutibiwa ipasavyo, ugonjwa wa homa ya ini hudhohofisha afya ya mtu taratibu bila kujionyesha kwa nje, hali hii hupelekea kutokea kwa tatizo la saratani ya ini (Liver cancer) na tatizo la kusinyaa kwa ini na kushindwa kufanya kazi (Cirrhosis), hii hupelekea kutokea kwa vifo takribani milioni 1.3 kila mwaka...”.
Hii ni tafsiri isiyo rasmi kutoka katika ujumbe wa shirika la afya duniani (World health organization-WHO) uliosemwa na Mkurugenzi mkuu wa shirika hilo Dr. Tedros A Ghebreyesus. Taarifa hiyo iliyotolewa siku ya homa ya ini duniani tarehe 28 julai mwaka huu, ilionyesha uwepo wa matumaini ya kutibiwa homa ya ini aina C (Hepatitis C) kutokana na uwepo wa dawa mpya zinazotibu aina hiyo ya homa ya ini ndani ya kipindi cha miezi mitatu kwa mtu yeyote mwenye umri kuanzia miaka 12 na kuendelea.
Homa ya ini kama yalivyo magonjwa mengine, huambukizwa/husambazwa kwa njia mbalimbali. Kirusi kinachosambaza homa ya ini aina B (HBV) kina uwezo mkubwa wa kuimili hali ya hewa ya nje ya mwili hivyo kinaweza kubaki nje ya mwili kwa takribani wiki nzima bila kupata madhara, zifuatazo ni njia zinazopelekea maambukizi ya tatizo la homa ya ini kati ya mtu mmoja na mwingine;
Kuchangia vitu vyenye ncha kali kama sindano, nyembe, kisu, nk ambavyo huweza kujeruhi mwili na kutoa damu/majimaji, damu/majimaji hayo huweza kumuingia mtu mwingine na kumuambukiza endapo ndani yake kutakuwepo virusi hivi vya kueneza homa ya ini.
Utumiaji wa madawa ya kulevya kwa njia ya kujidunga sindano. Ini hufanya kazi nyingi ndani ya mwili, moja ya kazi zake ni kuchuja usumu kutoka katika mfumo wa damu ndani ya mwili, madawa ya kulevya huongeza usumu huo ndani ya mwili hivyo kulifanya ini kuwa na kazi ya ziada kitu kinachoweza kupelekea ini kushindwa kufanya kazi yake, licha ya usumu huo wengi wanaotumia madawa ya kulevya kwa njia ya kujidunga huchangia sindano kitu kinachowaweka watumiaji hawa katika hatari ya kuambukizana virusi vya homa ya ini.
Mgusano wa majimaji ya mgonjwa na mtu mwingine kwa njia mbalimbali kama mgusano wa vidonda, macho, mdomoni, nk. Kundi la wale wanaowahudumia wagonjwa ndio lipo katika hatari ya kuambukizwa virusi vya homa ya ini kwa njia hii ya mgusano, siyo tu wanao wahudumia wagonjwa bali na wale walio katika hatari ya kugusanisha sehemu za miili zenye majimaji. Umakini unahitajika wakati wa muingiliano kati ya mtu na mtu ili kuepukana migusano maeneo yenye michubuko mwilini.
Maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto. Maambukizi haya huweza kutokea wakati wa kujifungua endapo shughuli nzima ya kujifungua itafanyika chini ya uangalizi mdogo, hii ni moja ya sababu inayowafanya wataalamu wa afya kuishauri jamii kuwapeleka kina mama kujifungulia kliniki pamoja na kuzingatia ratiba ya kliniki ya wajawazito katika kipindi chote cha ujauzito, hii itasaidia kutunza na kuboresha hali ya afya ya mtoto ajae.
Matumizi ya dawa kiholela. Dawa zote kwa ujumla wake zimetengenezwa katika kwa minajili ya kutumika katika kiwango maalumu ambacho hakiwezi kuleta madhara katika mwili wa binadamu, maelekezo yatolewayo juu ya matumizi ya dawa hizi yasipozingatiwa huongeza kiwango kikubwa cha usumu ndani ya mwili kiasi cha kulifanya ini kuzongwa na kazi ya kutoa sumu mwilini. Hali hii hulichosha ini na kulipunguzia ufanisi wa utendaji wake wa kazi na hatimaye kuliweka ini katika hatari ya kupatwa na maambukizi ya homa ya ini kwa urahisi zaidi.
Njia ya tendo la ndoa. Wanandoa wanaposhauriwa kwamba wanapaswa kuwa waaminifu katika ndoa haiishi tu katika kutunza na kusimamia misingi ya imani katika kanisa bali pia ushauri huu una lengo la dhati la kutunza afya zao. Imezoeleka kwa wengi kuwaza kuwa Ukimwi ndio unasambazwa kwa njia ya tendo la ndoa, ukweli ni kwamba magonjwa mengineyo kama homa ya ini husambazwa pia kwa njia hii kwani pia inahusisha migusano ya majimaji katika mwili, hivyo ni vyema kwa wanandoa kuwa waaminifu katika ndoa zao na wengineo walio katika mahusiano(Uchumba) kujitahidi kuepuka swala hili.
Si rahisi kutambua endapo mtu analo tatizo la homa ya ini katika hatua za mwanzo za tatizo hili, pengine mtu anaweza kukaa zaidi ya mwaka mmoja bila kuonyesha dalili zote za tatizo la homa ya ini katika mwili wake, lakini ifikapo hufika wakati dalili hizi zikajionyesha kwa nje aidha moja baada ya nyingine au pengine kwa makundi. Uonapo dalili zifuatazo wahi kituo cha afya kwa uchunguzi pamoja na dalili zifuata kwani hizi ni dalili/viashiria vya homa ya ini;
Kubadilika kwa rangi ya ngozi pamoja na rangi ya macho kuwa rangi ya njano.
Kujisaidia haja ndogo(Mkojo) yenye rangi nyeusi.
Kupatwa na homa, mafua pamoja na kuumwa kichwa.
Kupatwa na tatizo la kukosa nguvu.
Kuhisi kichefuchefu na pengine kutapika.
Kupatwa na maumivu ya tumbo upande wa juu kulia.
Kupungua uzito wa mwili.
Tiba dhidi ya tatizo la homa ya ini zinapatikana katika vituo vya afya, lakini gharama za matibabu ya ugonjwa wa homa ya ini ni kubwa kwa kiasi fulani, hivyo ni vyema jamii ikajifunza juu ya njia za kujikinga dhidi ya homa ya ini ili kuepuka gharama za maisha zisizo za lazima. Zifuatazo ni njia za kujikinga dhidi ya kuambukizwa tatizo hili;
Kupata chanjo ambayo hukinga homa ya ini aina B.
Chanjo kwa watoto wachanga kulingana na ratiba ya chanjo katika kliniki ya watoto.
Epuka kujidunga dawa za kulevya.
Epuka kuchangia sindano na vitu vingine vyenye ncha kali.
Kutembelea vituo vya afya mara kwa mara kwa lengo la kupima afya na kupata msaada wa kitabibu mara uonapo hali ya afya inabadilika.
Maono ya shirika la afya duniani(WHO) ni kutokomeza tatizo la homa ya ini ifikapo mwaka 2030, kauli mbiu ya mwaka huu inayosema “Pima, tibu homa ya ini” inawakumbusha watu wote juu ya lengo la kutokomeza homa ya ini kwa kutoa mualiko maalumu kwa kila mtu kuijali afya yake, ni wazi kuwa sauti ya pamoja inaweza kufanikisha lengo hili la kutokomeza tatizo la homa ya ini na hatimaye kumaliza pia tatizo la saratani ya ini. 


Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

MJUE MTAKATIFU MARIA GORETTI