‘Mwanakwaya mwenye vikwazo vinavyomtenga na ekaristi hataruhusiwa kuimba’

Na Marco Kanani, Geita
WITO umetolewa kwa wanakwaya wote wa Parokia ya Bikira Maria Mama wa Fatima Geita kuhakikisha wanakuwa mfano hai wa kupokea masakramenti, ambapo hadi kufika juma la kwanza la majilio kila mwanakwaya ambaye atakuwa hajarekebisha ndoa au kuondoa kikwazo chochote kinachomtenga na sakramenti za Kanisa hataruhusiwa kuimba.
Wito huo umetolewa na Padri Gerald Singu Paroko wa Parokia ya Bikira Maria Mama wa Fatima Geita wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu akiwa anaongea na waamini wa Parokia hiyo katika mahubiri yaliyoenda sambamba na maadhimisho ya Siku ya Vijana Kijimbo.
Padri Singu mesema kuwa haiwezekani mwanakwaya ahamasishe waamini katika nyimbo kwenda kukomunika wakati yeye anabaki amekaa kwenye kiti.
 Pia ametoa rai kwa viongozi wa ngazi mbalimbali za kanisa katika parokia hiyo kuanzia ngazi ya jumuiya kuwafikia waamini wote wasiopokea masakramenti kuwafikia na kuwashauri kurudia masakramenti, wawape miongozo itakayowafanya waone ni jambo jema kwao kurudia masakaramenti na kwamba asiwepo kiongozi wa kuwakatisha tamaa.
Wakati huo huo paroko huyo ametoa wito kwa wanaume katika familia kutowakwamisha wake zao wenye nia ya kurudia masakramenti kwa kuwawekea vikwazo visivyo na msingi na badala yake wanandoa wote wafanye bidii ya pamoja kurudia masakramenti waliyojifungia wao wenyewe.
Padri Singu amesema kuwa inavyoonekana akina mama wengi wanayo nia na hamu kubwa ya kutaka kurudia masakramenti lakini wanakutana na vikwazo kutoka kwa waume zao na hivyo kuwafanya waendelee kujitenga naYesu wa ekaristi kitu alichosema kuwa si chema kwa mkristo anayejitambua.
“Akina baba acheni kuwawekea vikwazo akina mama wanapotaka kurudia masakramenti, inavyoonekana akina mama wanayo hamu kubwa ya kutaka kurudia masakramenti lakini wanapowashirikisha ninyi akina baba mnakuwa na vikwazo vikiwemo kuwa hamjajipanga. Mnajipanga nini? rudieni fungeni ndoa hata bila sherehe, sherehe yenu kubwa iwe ni kumpokea Yesu katika Ekaristi Takatifu” amesema.
Akihimiza zaidi juu ya jambo hilo muhimu kiroho amesema kuwa waamini wote waliojifungia kupokea sakramenti za kanisa waache ukaidi na waone kujitenga na sakramenti hizo wanapungukiwa na kitu cha maana.


Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU