Askofu Chengula: Padri bora hanywi pombe kilabuni

Na Izack Mwacha, Mbeya
WITO umetolewa kwa viongozi wote wa kiroho hususani mapadri kutambua kuwa kunywa pombe kilabuni siyo tabia za padri mzuri ambaye anamuwakilisha Kristo Duniani.
Wito huo umetolewa na Askofu wa Jimbo Katoliki Mbeya Mhashamu Evaristo Chengula wakati wa Ibada ya Misa Takatifu ya Daraja ya upadri kwa Shemasi Jacob Machibya, iliyofanyika Parokia ya Chunya Jimboni Humo.
Katika homilia yake Askofu Chengula amebainisha kuwa yapo mambo mengi ambayo yanawezesha kujua kiongozi bora na muadilifu mbele za watu, lakini kipimo ambacho pia kitaimarisha zaidi  nafasi ya kiongozi kama padri muwakilishi wa Kristo ni pamoja na kufanya mambo sahihi na kwa wakati.
“Sidhani kama litakuwa jambo la busara kwa padri kukaa kilabuni na kuanza kunywa pombe, hapana hiyo siyo tabia njema” amesisitiza Askofu chengula.
Katika hatua nyingine Askofu Chengula amewaasa viongozi wa Halmashauri Walei kuwa na uwezo wa kuzungumza na mapadri wao bila ya kuwa na wasiwasi na jambo lolote, na hiyo itakuwa na tija zaidi tofauti na kuzungumza wao binafsi bila ya kumfikishia ujumbe muhusika, kwa kufanya hivyo ni wazi kuwa wanatenda dhami na pia muafaka hautapatikana.
“Padri siyo malaika naye anakosea lakini unakuta viongozi wa Halmashauri Walei wanaogopa kumuambia wanakaa kimya. Hapana hiyo siyo sawa kwani kazi ya padri ni pamoja na kukemea yaliyo mabaya, sasa kama ukiona na yeye anakosea ni laazima utafute njia nzuri ya kumrudisha na siyo kukaa kimya” amesema Askofu Chengula huku akiongeza kuwa katika mazungumzo mambo mengi yanafanikiwa.
Wakati Askofu chengula akiwaasa walei kuwaombea mapadri na watawa pia amekumbusha kuwa jukumu la kuombea miito mitakatifu nalo ni la kila mkristo, na itasaidia watoto wengi zaidi kuwa na hamu ya kumtafuta Kristo kupitia Daraja Takatifu ya Upadri.
Katika ibada hiyo ya misa iliyofanyika tarehe 16/08/2019 katika Parokia ya Chunya jimbo la Mbeya,  Shemasi Jacob Machibya amepewa Daraja Takatifu ya Upadri na Askofu Evaristo Chengula huku akimuahidi sala na maombi yake ili aweze kudumu vema katika nafasi yake ya upadri.


Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU