Maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo iwe ni fursa ya kuendelea kuimarisha uhusiano, umoja wa Wakristo pamoja kuwanufaisha binadamu wote. Ni nafasi ya kukumbuka ushuhuda wa pamoja uliofanywa na viongozi wa Kanisa la Kiorthodox na Kanisa Katoliki kwa ajili ya wakimbizi na wahamiaji huko Lesvos, nchini Ugiriki. Wote hawa wanahitaji kuhakikishiwa usalama wa maisha yao, amani na utulivu na kwamba, wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji ni changamoto kubwa kuwahi kutokea baada ya vita kuu ya pili ya dunia. Kuna watu wengi wanaoendelea kuteseka na kunyanyasika, wengi wao wakiwa ni wale wanaotoka huko Mashariki ya Kati. Ni wajibu wa Makanisa kusikiliza kilio cha wale wanaoteseka na kupondeka moyo; wahanga wa vitendo vya misimamo mikali ya kidini, ubaguzi, dhuluma, ukosefu wa haki jamii, umaskini na baa la njaa duniani. Wote hawa wanapaswa kuoneshwa mwanga wa matumaini katika maisha yao kwa kutambua kwamba, hawa ni binadamu na maisha yao ni matakatifu. Hii n...