SHEREHE YA EKARISTI TAKATIFU-MAANA HALISI NI MAANDAMANO




Sherehe ya  Ekaristi Takatifu – maana halisi ni maandamano
Tunaadhimisha Sherehe ya Mwili na Damu Takatifu ya Bwana wetu Yesu Kristo kila mwaka siku ya Alhamisi inayofuata baada ya kuadhimisha Sherehe ya Utatu Mtakatifu. Kwa kuwa Sherehe hiyo ni  Sikukuu ya amri, Kanisa imeruhusu kuiadhimisha  siku ya Dominika inayofuata ili  Wakristo wote waweze kutimiza wajibu wao wa kusali .
 Kuanza na Kuenea
 Kihistoria Sherehe hiyo ilianza huko Ufaransa kutokana na maono ya mtawa Juliana aliyoanza kuyapata mnamo mwaka 1209. Baada ya juhudi kubwa ya kumwomba Askofu wake kuanzisha Sherehe hiyo, hatimaye  ombi la sista Juliana lilipokelwa. Mwaka 1246 iliadhimishwa kwa mara ya kwanza huko Lie’ge  nchini Ufaransa.
Mwaka 1264 Papa Urban IV (wa nne) aliitangaza Sherehe hiyo iadhimishwe popote katika Kanisa. Kumbe kabla ya kuteuliwa kuwa Papa,  Urban alikuwa shemasi na baadaye padri wa jimbo hilo la Liege, alishaifahamu historia ya sikukuu hiyo.  Papa Urban IV alimwomba Mt.Thomaso wa Akwino(1224-1274) ambaye alikuwa mtaalamu sana katika elimu ya Mungu kuandika sala na tenzi zote za Sherehe hiyo. Tunaona utaalamu wake hasa katika Sekwensia ndefu ya Sherehe hiyo.
Kwa bahati mbaya  Papa Urban IV alifariki mwaka huohuo na kufanya agizo lake kutotekelezwa kwa miaka kadhaa. Alikuwa Papa Klementi V (1264-1314, ambaye alikuwa Papa kuanzia 1305 katika Mtaguso wa Vienna(1311-1312) aliagiza kwa mkazo kwamba Sherehe hiyo iadhimishwe potepote katika Kanisa Katoliki. Pamoja naye, baadaye Papa Yohane XXII (ishirini na mbili) naye alisisitiza jambo hilo. Sherehe hiyo mpaka miaka ya karibuni ilikuwa ikiitwa: Sherehe ya Mwili wa Kristo (Corpus Christi).  Ni dhahiri  kuwa mwelekeo wa Sherehe ulikuwa hasa kumwabudu Kristu katika Mwili wake kama jina la Sherehe lilivyosimama. Basi mnamo mwaka 1849 Papa Pius wa tisa aliweka Sikukuu ya Damu Takatifu ya Yesu ambayo iliadhimishwa Julai 1. Kwa hiyo kulikuwa na sikukuu mbili: Sherehe ya Mwili wa Bwana na Sikukuu ya Damu Takatifu ya Bwana.
 Marekebisho ya Mtaguso
Katika marekebisho yaliyofanywa na Mtaguso Mkuu wa pili wa Vatikano ni pamoja na kurekebisha Sherehe hiyo. Katika Katekisimu ndogo tunasoma: Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya Mwili na Damu takatifu ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mungu - mtu, katika maumbo ya mkate na divai.  Mkate na divai ni alama za Sakramenti.
Kwa vile Sikukuu hizo mbili zilikuwa na mwelekeo wa kuzitenga alama wazi za Sakramenti hiyo moja Mwili peke yake na Damu takatifu kuadhimishwa katika nafasi tofauti basi marekebisho ya Mtaguso mkuu yameziunganisha kuwa Sherehe moja. Sasa Sherehe hii inaitwa: Sherehe ya Mwili na Damu Takatifu ya Bwana wetu Yesu Kristo. Ni dhahiri kuelewa kwamba mwili ulio hai ni pamoja na damu yake hai pia. Jina hilo ndefu hufupishwa kwa kusema: Sherehe ya Ekaristi Takatifu.
Maandamano  ya Kuabudu
Tangu Sherehe hiyo ilipoanza imekuwa na utaratibu wa kufanya maandamano pamoja na Sakramenti ya Ekaristi ikichukuliwa katika chombo maalum kiitwacho monstransi ili kumwabudu Bwana wetu Yesu Kristo hadharani. Maandamano hayo yamekuwa yakipambwa na bendera nyeupe na hata rangi nyingine zenye kuvutia pamoja na maandishi ya kumtukuza Yesu katika Ekaristi. Bendera na vipeperushi hivyo vinapamba sehemu mbalimbali ya maandamano hayo; yaani sehemu ya watoto, vijana, akinababa na hata akinamama. Wasichana au pengine akinamama wachache walioandaliwa huwa mbele ya Ekaristi na kumwaga maua kama ishara ya heshima kubwa kwa Bwana wetu Yesu Kristo.
Kwa kawaida katika maandamano hayo huandaliwa kituo kimoja au viwili na hata zaidi kutegemea urefu wa njia ya maandamano. Katika vituo hivyo Ekaristi itawekwa juu ya meza iliyopambwa vizuri na waamini husimama au hupiga magoti ili kusali kwa kitambo. Hata iwapo maandamano siyo marefu inashauriwa sana kuwa na kituo angalau kimoja kusudi tendo hilo la kuandamana hadharani liimarishwe na sala zinazotolewa na Wakristo wote kama jumuiya moja inayoabudu. Katika vituo hivyo kuhani huongoza sala kuombea parokia, Jimbo, taifa na serikali  au  shida za jamii kwa jumla.
Sote Tumwabudu
Maandamano hayo na Ekaristi yasiwe tu kama tendo la haraka kwani ni tendo la kuabudu. Tuandamane kwa heshima mbele ya Bwana wetu Yesu Kristo. Inasisitizwa sana kuwepo na kituo angalau kimoja ambapo waamini wote kwa pamoja watatulia wakiabudu.
Tunawapongeza sana waamini wote wanaoshiriki maandamano hayo kwa moyo wa ibada na uchaji, wakishiriki kuimba nyimbo za Ekaristi na  nyingine zinazofaa. Wanaonyesha mfano mzuri wa kudhihirisha imani hadharani. Iwapo kuna Misa mbili baadhi ya Wakristo walioshiriki Misa ya kwanza huja  mwishoni mwa misa ya pili ili wapate kushiriki maandamano hayo muhimu ya kumwabudu Yesu. Hongera sana kwa kuonyesha uhai wa imani namna hiyo.
Kwa upande mwingine lakini tumeshuhudia baadhi ya waamini waliokuwa wakisimama pembeni mwa njia ya maandano na kuongea bila kushiriki maandamano. Huwaangalia wenzao wanapoandamana na wengine huendelea na biashara zao. Hilo si jambo zuri kamwe! Ni mara moja tu kwa mwaka mzima Liturujia imeweka utaratibu wa kumwabudu Yesu kwa namna hiyo. Wakristo wanapaswa kuvumilia adha ya kuandamana na kujitoa muda wao kwa ajili ya Liturujia hiyo maalum ya kumwabudu Yesu na  kukiri imani hadharani.
Tendo hilo la kuandamana ni tendo la kumwabudu Yesu Kristo na kukiri kwa dhati kwamba yeye Mungu - mtu yumo katika Sakramenti hiyo ya Mwili na Damu yake takatifu. Pamoja na hilo, ni tendo la  kumshukuru kwa  kudumu na waamini katika Sakramenti hiyo. Anakaa  katika Sakramenti hiyo usiku na mchana pamoja nasi.  Wakristo wangapi huenda  pale kanisani kumwabudu?  
Kumpokea Yesu kwa uchaji
Yesu tunayemwabudu ni pia chakula chetu cha uzima wa milele.  Kwa nafasi hii inafaa kukumbuka utaratibu wa kupokea Komunyo kwa heshima stahiki. Wakristo wajiandae vizuri kiroho na hata kuwa safi kimwili kwa kupokea Ekaristi takatifu. Mahali wanapopokea Ekaristi wakiwa wamesimama mstari wakumbuke kuonyesha tendo la heshima kama vile kuinama kabla ya kupokea Ekaristi.
Wanaopokea Ekaristi mkononi wakumbuke kuwa  mikono yote miwili iwe tayari kwa tendo hilo kuu la kumpokea Bwana . Isiwe, kwa mfano,  mkono moja unashika leso au simu. Inawapasa kusafisha kwa ulimi kwenye kiganja pale ilipowekwa Ekaristi takatifu kwa sababu mara nyingi hubaki chembechembe  ambazo zisiposafishwa kwa ulimi huanguka sakafuni na kukanyagwa. Kumbe chembechembe hizo ni sehemu ya Mwili wa Bwana.
 Mkristo akishampokea Yesu katika Sakramenti haitakiwi kuinama tena bali hurejea mahali pake kwa uchaji na kuabudu kimya kwa kitambo. Halafu aungane na wenzake katika kuimba. Tendo hili hutendeka mara nyingi basi lifanyike kwa heshima na uchaji.


Comments

  1. Asanteni sna kwa maelezo mazuri na yenye ufafanuzi wa kina yananisaidia hata mimi katika kuelezea katika vipindi redioni Mungu awabariki sana.

    ReplyDelete

Post a Comment

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU