HOTUBA YA PAPA JUU YA WANAWAKE MASHEMASHI:VATICAN YATAHADHARISHA


Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya habari ya Vatican na Jimbo Takatifu  kwa Ujumla, Padre Federico Lombardi, ametoa ufafanuzi juu ya hotuba ya Papa Francisko wakati akikutana na Wakuu wa Mashirika ya Kike , akisema , Papa Francisko hajasema kama analenga kuanzisha utaratibu wa kutoa daraja la ushemasi au ukuhani kwa wanawake bali alikubaliana na Masista kuunda Tume ya kuchunguza zaidi majukumu yaliyofanywa na Mashemasi wanawake katika kanisa la mwanzo.  
Padre Lombardi ametoa maelezo haya kufuatia  taarifa nyingi za vyombo vya habari, baada ya Papa kukutana na Wakuu wa Mashirika na Taasisi za Watawa wa Kike, wakati wa kipindi cha maswali na majibu , Alhamisi iliyopita, katika ukumbi wa mjini Vatican, ambamo kati ya mengine pia , alijibu swali  lililouliza juu ya   uwezekano wa Kanisa kuwa na  mashemasi wa kike.   Masista  Mama Wakuu wapatao 900, walikutana na Papa, kama sehemu ya  Mkutano wao  Mkuu wa  Umoja wao wa Kimataifa, uliokuwa ukiendelea  hapa Roma.  
Mkutano wa Baba Mtakatifu  Francisko na Masista ulidumu kwa muda wa saa moja na nusu, ambamo walizungumzia maswala mbalim mbali  juu ya utume na majukumu ya wanawake katika maisha yao kidini. Na  Papa alijibu maswali kadhaa nyeti , ikiwemo nini kinachozuia hasa Kanisa kuwapa wanawake hata daraja la Ushemasi wa  kudumu , kama ilivyokuwa katika maisha ya  Kanisa la mwanzo. Katika jibu lake, Papa alisema,  uelewa juu ya jukumu la mashemasi wa kike katika Kanisa la Mwanzo  si bayana na hivyo walikubaliana na Masista kwamba , itafaa kuunda Tume ya kuchunguza zaidi juu ya  suala hili.
Padre Federico Lombardi ametaja  Mkutano huu wa  Papa na Masista toka duniani kote, kwamba yalikuwa ni mazungumzo mazuri yenye  kutia  moyo  kuhusu  uwepo wa wanawake katika utume wa Kanisa na hasa maisha ya wanawake waliotolea maisha yao huduma  ya Kanisa ikiwa ni pamoja na wajibu wao katika nafasi muhimu ndani ya  Idara mbalimbali za Kanisa ambako  wakfu wa kikuhani hauhitajiki.
Akizungumzia juu ya maoni mengi yaliyotolewa juu ya maelezo ya Papa kuhusu kuunda Tume ya kuchunguza  suala la mashemasi wa kike, Padre Lombardi amesema , suala hili limekuwa likiongelewa  ndani ya Kanisa hata katika siku za nyuma, kutokana na ukweli kwamba wakati wa  Kanisa la mwanzo, kulikuwa na wanawake  wanaotajwa kama Mashemasi ambao walifanya kazi fulani ndani ya jamii ya kikristo, lakini majukumu hayo hayakutajwa bayana.
Padre Lombardi anasema kuna haja ya kuwa waaminifu katika jambo hili, wakati tunatoa maoni juu ya maneno ya Papa  Francisko, ambamo alitaja juu ya kuanzisha Tume ya kutazama  tena  suala hili kwa uwazi zaidi, majukumu yaliyofanywa na Mashemasi wanawake wakati wa kanisa la mwanzo . Papa hakusema yeye anakusudia kuanzisha  utaratibu wa kuweka  mashemasi wa kike na wala  hakuzungumzia juu ya  Daraja la Ukuhani kwa  wanawake. Na kwamba,  Papa katika mahubiri yake ya wakati wa maadhimisho ya Ibada ya Ekaristi , aliweka wazi kwamba suala hili liko nje ya fikra zake.  
Padre Lombardi pia amesema ni makosa kupuuzia mengine yote muhimu yaliyozungumzwa na Papa Francisko wakati akikutana na Masista ,  na kung’ang’ania  hoja moja tu ya uwezekani wa Ukuhani  kwa wanawake kama  vile hapakuwa na mengine hayakuzungumzwa. 

Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU