Rais Magufuli: Ni wachache wanaoweza kutetea ukweli kama Ask. Chengula
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli amesema kuwa
ni viongozi wachache wanaoweza kujitokeza hadharani na kusema ukweli kama
alivyofanya marehemu Askofu Evaristo Chengula.
Amesema hayo katika Misa Takatifu ya kumuombea na
kuaga mwili wa Askofu Chengula, iliyofanyika Novemba 26 katika Kikanisa cha
Bikira Maria Mkingiwa dhambi ya asili katika Baraza la Maaskofu Katoliki
Tanzania (TEC), Kurasini jijini Dar es salaam.
Akitoa salamu za rambirambi katika misa hiyo Dkt.
Magufuli ametoa pole kwa Kanisa kwa kuondokewa na mmoja wa viongozi wa kiroho
ambaye daima alithubutu kusema na kusimamia ukweli.
“Amemaliza kazi yake salama, ameitangaza Injili na
amekuwa mkweli daima. Hakusita kuzungumza ukweli. Hivi karibuni alijitokeza na
kupinga vitendo vya ushoga vinavyoshamiri katika jamii yetu. Ni viongozi
wachache wanaoweza kujitokeza hadharani na kutangaza ukweli wa Injili” amesema
Dkt. Magufuli.
Akitoa homilia katika misa hiyo Askofu Mkuu Mwandamizi
wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es salaam Mhashamu Yuda Thadei Ruwaich amesema kuwa
kila mbatizwa hana budi kuishi wito wa kumshuhudia Kristo kiaminifu kwa kila hilo ni jukumu la kila
mkristo. Amebainisha kuwa utumishi wa Askofu Chengula ulijaa uaminifu, furaha,
ushujaa na uadilifu.
“Hakuogopa kusema ukweli kama ilivyompasa, Mungu
alimpa uthubutu katika kuushuhudia ukweli wake. Nasi hatuna budi kuishi
kiaminifu wito wetu wa kumshuhudia Kristo, hili ni jukumu la kila mbatizwa,
haidhuru ni nani” ameeleza.
Comments
Post a Comment