Ask. Chengula mshumaa uliozima
Kanisa Katoliki Tanzania limepata pigo
baada ya kuondokewa na Askofu wa Jimbo Katoliki Mbeya Mhashamu Evaristo
Chengula aliyefariki kwa ugonjwa wa moyo
Novemba 21 mwaka huu katika hospitali ya
Moyo ya Jakaya Kikwete katika hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es
Salaam alipokuwa anapata matibabu.
Taarifa kutoka Ofisi ya Katibu Mkuu Baraza la
Maaskofu Katoliki Tanzania Padri.Dr. Charles Kitima zinasema kuwa, Marehemu
Askofu Chengula ameaga dunia akiwa na umri wa miaka 77 ya kuzaliwa ambapo
amezaliwa January I mwaka 1941.
Atazikwa
Novemba 27 mwaka huu saa nne asubuhi katika Kanisa la Kiaskofu la Mtakatifu
Antoni wa Padua Jimbo Katoliki Mbeya.
Akizungumza na
Gazeti hili, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania Mhashamu Gervas
Nyaisonga amesema kuwa, Kanisa limepoteza Askofu mwenye fadhila mbalimbali
ikiwemo ya uvumilivu, ucheshi, mpenda watu, mpole na msahimivu.
“Ninawapa pole
Maaskofu wote wa Kanisa Katoliki kwa kuondokewa na mmoja wa wachungaji wakuu
katika Kanisa la Tanzania.
Pia ninawapa
pole wanakanisa wa Tanzania, Mapadri, watawa na walei wote hususani mapadri wa
Jimbo Katoliki Mbeya, watawa wa kiume na kike, waamini waamini, viongozi
mbalimbali wa dini na serikali jimboni Mbeya.
Ninawaasa
tuiombee roho ya marehemu iweze kupokelewa Mbinguni na kupokea msiba huu kwa
imani tukijua kuwa, sisi wakristo njia yetu ya kwenda kwa Baba ni kifo, ni
katika kufa ndipo tunapata uzima wa milele,” amesema Askofu Nyaisonga.
Aidha amesema
kuwa Marehemu Askofu Chengula alikuwa baba mwema, mpenda watu na mcheshi ndiyo
maana hata picha zake zinazosambaa kwenye mitandao anaonekana anatabasamu kwa
sura ya upendo.
Ni mtumishi
mwaminifu mwenye busara ambaye amefanya kazi ya kulitumikia Kanisa la Mungu kwa
uaminifu, amemaliza mwendo, amemaliza kazi yake maana katika umri alionao
amefanya mengi.
“Sisi mapadri
wa jimbo lake la Mbeya tulifurahia na kuridhishwa na utendaji kazi wake kwani
alikuwa baba anayeendeleza maisha ya mapadri, wengi tulijiendeleza kielimu
katika fani mbalimbali na amekubali kututoa kufanya kazi katika taasisi za
Kanisa .
Hiyo inaonesha
moyo wake wa kujitolea kwa Kanisa. Kuna mapadri wanafanya kazi AMECEA, Walimu
katika vyuo vikuu, Baraza la Maaskofu, kuna mapadri madaktari wa binadamu na fani
mbalimbali. Hayo yote ni matunda ya kazi yake,” amesema.
Amewataka
waamini, mapadri na Kanisa kwa ujumla kuendelea kumuenzi husuani katika fadhila
ya upole, uvumilivu, upendo, uthubutu, ukarimu na ucheshi ili kujenga jumuiya
yenye amani na furaha.
Katibu mkuu wa
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania amesema Padri Dr. Charles Kitima ameeleza
kuwa, Marehemu Askofu Chengula aliwasili Jijini Dar es Salaam, Novemba 20 mwaka
huu akiwa anasumbuliwa na ugonjwa wa moyo.
Alipelekwa
kwenye Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete katika Hospitali ya Taifa ya
Muhimbili, na kulazwa ili aendelee na matibabu.
Jitihada za Madaktari kutaka kuokoa maisha
yake, hazikufanikiwa ndipo majira ya saa
tatu asubuhi ya Novemba 21 mwaka huu aliaga dunia.
Baadhi ya
wanaharakati wa uhai (Pro-life) wamesema kuwa Askofu Chengula ameacha alama
katika taifa hili kwani ni hivi karibuni tu amewataka wananchi na serikali
kukemea na kupinga ushoga kwa nguvu zote.
Ikumbukwe
kuwa, wiki moja iliyopita Marehemu Askofu Chengula alisikika sana kwenye vyombo
vya habari Tanzania huku akipongezwa kauli yake aliyosema kuwa Ushoga ni
ushetani.
Kuhusu suala
la Ushoga Askofu Chengula alisema kuwa licha
ya Vitabu Vitakatifu kuelezea
kuwa ushoga ni dhambi pia siyo utamaduni
wa watanzania.
Hivyo aliwataka watanzania kuwa makini na watu wasiolitakia taifa mema na wanaotaka
kuliingiza Taifa katika matendo maovu ya aibu yasiyompendeza Mungu.
“Hawa watu wa
haki za binadamu wajikite katika masuala
ya kupiga vita utoaji wa mimba na kuuwa
watoto wasio na hatia na siyo mambo ya
ushoga, ni dhambi kubwa.
Nimependezwa
sana na kauli ya ya huyu Waziri wa mambo
ya ndani alipoonyesha msimamo bungeni
kuwa Tanzania ni hekalu la Roho Mtakatifu na hivi haipaswi kuchezewa chezewa
kwa vitendo visivyompendeza Mungu ukiwemo ushoga,”alisema enzi za uhai wake
wiki moja iliyopita.
Kwa wanachuo
wote Askofu Chengula aliwapa wosia wa kuzingatia taaluma akiwakataza kujiingiza
kwenye siasa.
Alisema Kanisa
lingependa kuona wahitimu watakaomaliza
wanaopata elimu katika vyuo vya Kanisa ni wahudumu wa jamii wanaotoa huduma
wakizingatia weledi na haki bila ubaguzi wa
itikadi zao vya vyama wala imani za dini zao.
“Hatutavumilia
wanafunzi wanaojihusisha na siasa kwa kutumiwa na vyama vya siasa kuingiza
masuala hayo vyuoni hasa vyuo vya
Kanisa hali ambayo inaweza kuleta
mgawanyiko miongoni mwa wanafunzi. Someni kwanza mkimaliza ndipo mshikamane na
mambo mengine nje ya taaluma.
Lengo la
wanafunzi kwenda shule ama vyuo vya Kanisa ni kuwajengea uelewa,
kuwaimarisha na kuwaendeleza watanzania
kitaaluma wapate maarifa waweze kulitumia Taifa . Siasa ni nje ya lengo na
zinawapotezea muda.
Tusingependa kuona wala kusikia wanafunzi wakijihusisha na CCM, Chadema, Cuf
na vyama vingine vyovyote. Nasema siasa ni marufuku,” amesema wiki moja
iliyopita akiwa hai huko SAUT Mbeya.
Alitahadharisha
juu ua uchaguzi unaokuja ambapo siku ya Injumaa Kuu mwaka huu aliwaasa waamini na wananchi kuchagua viongozi sahihi
na watakaokidhi mahitaji yao badala ya kufanya makosa kwa kuchagua viongozi
wasiofaa na kuanza kulalamika baada ya uchaguzi.
Amesema
imekuwa ni kawaida kwa maaskofu na wadau wengine kuanza kukosoa viongozi baada
ya uchaguzi, jambo ambalo halina faida sana, na hivyo wao kama maaskofu mwaka
huu wameamua kuwataka waumini wao kuwapima kwa umakini watu wote
watakaojitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika chaguzi zijazo kwa
kuanzia na uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika mwakani.
Wasifu mfupi wa marehemu
Askofu
Evaristo Marcus Chengula alizaliwa tarehe Mosi Januari 1941, huko Mdabulo,
Wilaya ya Mufindi, Mkoani Iringa. Baada ya masomo ya utawa na upadri, Oktoba 15
mwaka 1970 alipewa Daraja Takatifu ya Upadri.
Novemba 8
mwaka 1996, Mtakatifu Yohane Paulo II alimteuwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki
Mbeya na kuwekwa wakfu kama Askofu Februari 2 mwaka 1997.
Amefariki
dunia akiwa amelitumikia Kanisa kama Padri kwa muda wa miaka 48 na Askofu kwa
muda wa miaka 21.
Raha ya milele
umpe ee Bwana na Mwanga wa milele umwangazie apumzike kwa amani, Amina.
Comments
Post a Comment