Mapadri msiburuze Misa Takatifu, Ekaristi ndiyo maisha yenu-Ask. Lebulu
Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu
Katoliki Arusha Mhasham Josaphat Lebulu amewataka Mapadri kuenzi
Ekaristi Takatifu huku akiwaonya wanaokimbiza Misa Takatifu kwa kisingizio cha
kujali muda.
Askofu Lebulu ameyasema hayo hivi karibuni katika adhimisho la Ibada
ya Misa Takatifu ambayo ilikuwa ni
maalumu kwa ajili ya Bikira Maria Nyota ya Uinjilishaji Tanzania katika
maadhimisho ya miaka 150 ya uinjilishaji Tanzania bara ambayo yalifanyika
Bagamoyo ulipo mlango wa Imani.
Ametaka Maadhimisho ya Ekaristi Takatifu yafanywe kwa maandalizi ya
kutosha ili yaadhimishwe kwa imani.
“Tuenzi Neno la Mungu, Ekaristi Takatifu na Mama yake. Mimi kama
padri nikisahau Injili, nitaleta balaa na kasoro kubwa katika Kanisa, endapo
tutamdharau na kumuweka pembeni Mama Maria tutashindwa.
Wajibu wa kwanza wa padri ni kuishi na kuheshimu Neno la Mungu,
kuadhimisha Ekaristi Takatifu na kufungamana na Maria Mama wa Kanisa maana huyu
Mama ndiye anayetubeba mgongoni na kutufikisha mahali salama,” Amesisitiza
Askofu Lebulu.
Aidha amewataka wakristo wote kutambua kuwa urithi pekee wa
Uinjilishaji ni Neno la Mungu, Ekaristi Takatifu pamoja na Mama Bikira Maria.
‘Nimekuwa nikijiuliza ni kitu gani kiliwasukuma wamisionari waje
kwetu? Ndipo nikafungua maandiko Matakatifu ambayo yalinipa jibu moja,’Nimekuja
ili wawe na uzima tena uzima tele.’
Mungu akaniambia kupitia Neno lakwe kwamba, Yesu aliacha zawadi ya
neno la Mungu yaani Yeye mwenyewe ambaye ni Neno la Mungu aliyefanyika mwili.
Yesu hakuacha picha yake wala mchoro wake ili wafuasi wake wamkumbuke
la hasha aliacha Neno lake na Ekaristi Takatifu ambayo ni mwili wake na alisema
twaeni mle, twaeni mnywe.. fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu.
Alipopokea msalaba wake mama yake alifuata nyuma wakati hakuweza
kuelewa lolote lakini alikubuka maneno ya Simeoni ‘Upanga utapenya moyo wako’
alienda mpaka chini ya msalaba na Yesu
alituachia mama yake.
Alimtazama Mwanafunzi aliyempenda akasema ‘Tazama mama yako na Mama
tazama mwanao. Mwanafunzi aliyependwa na Yesu
ni mimi na wewe. Hiyo ni zawadi
ya tatu,” ameeelza Askofu Lebulu.
Amesema zawadi hizo Tatu yaani Neno la Mungu, Ekaristi Takatifu na
Mama Bikira Maria ndizo zilizowajaa
Wamisionari wakazibeba kila walipotaka kwenda huku wakiongozwa na maneno
ya Yesu, ‘Enendeni ulimwenguni mwote… Historia kama tuijuavyo hawa wamisionari
waliozikwa hapo kati ya umri wa miaka 20-40 ni Neno la Mungu, Ekaristi Takatifu
na Mama Bikira Maria viliwapa nguvu ya kufanya uinjlishaji.
Kuadhimisha Jubilei yetu ya 150 hapa Tanzania tunaona majitoleo ya
wamisionari na waamini watakaposahau
chanzo cha majitoleo yao ambayo ni Neno … watakuwa tumekosea mno maana walileta
kile kilichoachwa na Kristo wakakieneza kwetu.
“Walipokuja wamisionari
hawakujali kupata taabu maana hata Kristo hakujali kifo maana ni katika
kifo tunapata uzima wa milele. Sisi watanzania maneno hayo yanatuhimiza kuzama kutafuta kiini cha yale
Yesu aliyasia katika mioyo ya wamiaionari,”ameeleza.
Ameliasa Kanisa kufanya tathmini ili limshikuru Mungu pale
lilipofanikiwa na kuomba kupata mafanikio zaidi lakini pia kukubali pale
lilipoanguka ili kuomba toba na kusimama tena.
“Yesu amefanya kazi kupitia wamisionari ni zamu yenu waamini wa
Tanzania na anatutahadharisha kuwa yupo mwizi na mawakala zake. Kuna changamoto
ya imani na kuna hatari za waamini
wanaochanganya imani,
Kuna kushindwa na kuanguka na tusikose kusema ukweli hapa nimeshindwa
na hapa lazima tusimame ila hatutasimama bila kuomba toba.
Tusiangalie kuanguka tu na kukata tamaa bali tupige goti tumwambie
Mungu tumekosea atusimamishe maana Mungu anatuambia Moyo uliovunjika na
kupondeka hataudharau. Tumwambie Mungu tuhurumie tuweze kuendelea mbele,”
amesisitiza.
Ameliasa Kanisa katika kipindi kipya cha uinjilishaji kusia mbegu ya
imani kwa watoto na vijana ili wakue katika maisha mfungamano.
“Mwaka 1948 nilifika Kanisani nikafurahishwa na maua nilifikiri ni
Mbinguni nikaona masista wa Damu Takatifu na mapadri walivyokuwa wanafanya
misa. Nikasikia Neno, waacheni watoto wadogo waonje ukristo na kuanzia hapo
nikasema lazima niimbe nikajiingiza kwenye masuala ya imani baadaye nikawa
padri.
Sasa msiwache watoto na vijana nyumbani, washirikisheni imani, waende
Kanisani, washiriki mafundisho na semina mbalimbali za imani. Ninasisitiza malezi mfungamano.Watoto waachwe waelekezwe
ni marafiki wa Yesu,” amesema.
Aidha ameliasa Kanisa kuwekeza imani kwenye familia kwani ni jambo la msingi familia kuwa Kanisa dogo lenye watu wacha
Mungu na kuwa kitu kimoja na mapadri, watawa na maaskofu chini chini ya Yesu
Kristo na Nyota ya uinjilishaji ambaye ni Mama Maria .
Katika kilele cha maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 150 ya Uinjilishaji
nchini Tanzania Novemba 3 mwaka huu Askofu Mkuu Mstaafu Josaphat Lebulu wa
Jimbo Kuu Katoliki Arusha alijumuika pamoja na Askofu Mstaafu Damian Kyaruzi wa
Jimbo Katoliki Sumbawanga kumshukuru Mungu kwa miaka 50 tangu walipopewa Daraja
Takatifu ya Upadri, huku akisema kama wangekatiswa tamaa katika wito wao tangia
wakiwa wadogo wasingelikuwa mapadri na hatimae Maaskofu.
Comments
Post a Comment