Heri tufe kwa njaa kuliko misaada yenye shinikizo la ushoga-Kard. Pengo
ASKOFU Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki
Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo amepongeza na kufurahia
msimamo wa serikali dhidi ya kauli ya baadhi ya mataifa ya Magharibi kutishia
kusitisha misaada kwa Tanzania kwa kuwa nchi inapinga ushoga.
Ametoa msimamo huo hivi karibuni katika maadhimisho ya Misa Takatifu ya
Mavuno iliyofanyika kijimbo katika Viwanja vya Msimbazi Centre, vilivyopo Jimbo
Kuu Katoliki Dar es Salaam.
Kardinali Pengo amesema kuwa yapo baaadhi ya mataifa yanayotishia kukata
misaada kwa nchi zinazopinga ushoga na mahusiano ya watu wa jinsia moja hivyo
Kardinali Pengo amesisitiza kuwa, ni heri kufa kwa njaa kuliko kupokea misaada
yenye shinikizo la kufanya mambo machafu yaliyo kinyume na Mungu.
Kiongozi huyo wa kiroho amesema kuwa, uchafu wa mahusiano ya watu wa
jinsia moja ndio uliosababisha Sodoma na Gomora kuangamizwa na kwamba, mambo
hayo ni kinyume na mpango wa Mungu katika uumbaji, hivyo hayawezi kukubalilika.
“Tunaishukuru Serikali kwa msimamo wake kuhusu jambo hili, na sisi kama
Watanzania hatuwezi kuyakubali mambo hayo yasiyompendeza Mungu; na kama ni kufa
na njaa basi tufe na Mungu wetu,” amesema Kardinali.
“Tunalolifanya tunasema kitu
kimoja kwa Mungu kwamba, kama tutakufa kwa njaa
tutakufa na wewe, kama wanataka tuwe na ndege zisizo na marubani katika
mambo machafu, basi sisi tutabaki na wewe na si ndege wala magari ya kifahari,
kwa sababu kumpuuza Mwenyezi Mungu ni kujipuuza wenyewe,” amesema Kadinali
Pengo.
Ikumbukwe kuwa hivi karibuni, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi
Lugola, alisema kamwe vitendo vya ushoga haviruhusiwi na kila kiungo
kilichoumbwa na Mungu katika mwili wa mwanadamu kina kazi yake hivyo, Serikali
ya Tanzania haitakubali vibadilishiwe matumizi.
Waziri Lugola alitoa kauli bungeni Dodoma baada ya Mbunge wa Konde,
Khatibu Saidi Haji, kutaka msimamo wa Serikali kuhusu vitendo vya ushoga.
Akasema: “Serikali yetu kamwe haitaruhusu mwanadamu yeyote kubadili
matumizi ya kiungo ambacho kimekusudiwa kwa ajili ya kutolea haja, kitumike
katika matumizi mengine ambayo Mungu hakuyakusudia.”
Kauli hiyo imeridhisha Maaskofu wa Kanisa Katoliki na Mwadhama Kardinali
Pengo ambaye anakuwa Askofu wa pili kupinga ushoga hadharani huku Marehemu
Askofu Evaristo Chengula aliyekuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Mbeya akiwa wa kwanza kupinga vitendo vya
ushoga hadharani siku kadhaa kabla hajafikwa na mauti.
Pia katika Ibada ya Misa Takatifu ya
kumwaga Marehemu Askofu Chengula iliyofanyika Baraza la Maaskofu
Katoliki Tanzania (TEC) Kurasini Dar es Salaam Novemba 29 mwaka huu kabla ya
kusafirishwa kwenda Mbeya kwa maziko, Rais John Magufuli alimtaja Mhashamu
Chengula kama mtu wa Mungu aliyekemea ushoga hadharani.
Comments
Post a Comment