Askofu Kinyaiya aonya vijana kuhusu mavazi yenye tamaduni za nje
Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki
Dodoma Mhashamu Beatus Kinyaiya amewataka vijana kuvaa mavazi yanayositiri
miili yao wakizingatia tamaduni za kiafrika na imani yao.
Askofu Mkuu Kinyaiya amesema hayo
hivi karibuni katika Parokia ya
Mtakatifu Petro Swaswa jimboni humo alipokuwa anatoa Sakramenti ya
Kipaimara kwa vijana 75 na kuzindua duka la Jimbo la kuuza visakaramenti vya
Kanisa.
Amewataka vijana walioimarishwa
kwa sakramenti hiyo kutokuiga tamaduni ambazo zinaaibisha utu wao na imani yao
hasa mavazi kwani sio kila tamaduni inapaswa kuigwa.
“Vijana ninawaombeni tena sana
msikubali kufuata tamaduni ambazo zinakwenda kinyume na maadili yetu ya
kitanzania fuateni tamaduni zetu zenye maadili ,” amesema Askofu Mkuu Kinyaiya
Kwa upande wa suala la Utandawazi
Askofu Mkuu Kinyaiya pia amewataka vijana kuwa
makini katika suala la utandawazi maana hilo ndilo linalowasababisha
watu kuacha tamaduni zao na kuanza kuishi tamaduni za kigeni ambazo matokeo
yake yanakuwa sio mazuri katika jamii.
Sambamba na hayo pia amewakumbusha
wakristo wote kukataa kuyumbishwa kiimani na kitamaduni kwani karne ya sasa ina
makelele na sauti nyingi. Kuzitambua zauti zilizo sahihi kunahitahi hekima na
werevu.
Aidha
amelipandisha hadhi na kuzindua duka la visakramenti la Parokia kuwa la
jimbo lililogharimu zaidi ya shilingi milioni 30.2.
Akitoa taarifa ya ujenzi wa duka hilo la visakramenti Paroko wa
Parokia ya Mtakatifu Petro Swaswa Padri
Antipas Shayo amesema kuwa duka hilo linategemea kuuza bidhaa mbalimbali
kulingana na imani ya Kanisa Katoliki, na bidhaa hizo ni pamoja na vitabu,
rozari, vitenge vya wawata, Pete, misalaba, sanamu na vinginevyo vyenye nia ya
kuueneza ukristo.
Padri Shayo amesema duka hilo
litaendeshwa na Halmashauri ya walei kwa niaba ya waamini chini ya usimamizi wa
Paroko ambapo kiasi cha fedha kitakachopatikana kitawezesha waamini kuhudumiwa
huduma mbalimbali za kiimani na kijamii.
Hata hivyo amesema kuwa kamati ya
fedha, uchumi na mipango itahusika na utendaji wa shughuli za kila siku na
itawajibika kufahamu kiasi cha mali kilichoingizwa na kupokelewa kwenye vitabu.
Aidha Padri Shayo amesema mpango
wa baadae wa Parokia hiyo ni kujipanga na kuhakikisha kuwa mafundisho ya dini
yanapewa kipaumbele katika jumuiya, shuleni na nyumbani.
Comments
Post a Comment