Ask. Chengula azikwa Mbeya






Na Pascal Mwanache, Mbeya
WAZIRI wa Fedha na Mipango nchini Dkt. Philip Mpango amesema kuwa ni jukumu la viongozi wa dini kukemea uovu uliopo katika jamii na hata viongozi wa serikali wanaposhindwa kutimiza wajibu wao wa kuwatumikia watanzania.
Ameeleza hayo katika Misa Takatifu ya maziko ya marehemu Askofu Evaristo Chengula wa Jimbo Katoliki Mbeya iliyofanyika kwenye Kanisa la Hija Parokia ya Mwanjelwa, ambapo Dkt. Mpango amemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Ponge Magufuli.
Dkt. Mpango amesema kuwa marehemu Askofu Chengula alikuwa na uthubutu wa kukemea uovu katika jamii ya Tanzania, jambo ambalo viongozi wa dini hawana budi kuliendeleza. Amebainisha kuwa Askofu Chengula alikuwa ni kiongozi wa mfano kwa waamini wa Mbeya na watu wote.
“Waamini wa Jimbo Katoliki la Mbeya na wanachi wa Mbeya Mungu aliwapa zawadi kubwa, aliyoihamisha kutoka Iringa akawaleteeni ninyi. Huyu alikuwa ni kiongozi wa mfano. Aliwaelekeza watu kwa Mungu. Alithamini kazi kwa malengo, sikuzoea sana kusikia mpango mkakati kanisani, lakini yeye katika jimbo lake aliratibu mpango mkakati. Hii inaashiria ukweli kwamba ni lazima kazi ifanywe kwa malengo”.
Aidha Dkt. Mpango amesema kuwa wananchi wa Mbeya watamkumbuka Askofu Chengula kwa namna alivyojitola katika kuwapatia wananchi huduma nzuri za afya na elimu bila kubagua.

Rais TEC: Muda uliyopangwa na Mungu ndiyo muda mwafaka
Akitoa homilia katika misa hiyo Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzana (TEC) ambaye pia ni Askofu wa Jimbo Katoliki Mpanda Mhashamu Gervas Nyaisonga amesema kuwa muda uliopangwa na Mungu ndiyo muda mwafaka na kwamba huzuni ya mkristo ni huzuni ya kiimani, siyo huzuni ya kukata tama.
“Huzuni yetu ina chembe chembe za furaha ndani yake. Marehemu alikuwa na dira yake ambayo ni ‘Mungu dira yangu’. Hiyo ndiyo ilikuwa ndoto yake, kumfikia Mungu ndiyo utimilifu wa matarajio yake. Ili kufikia lengo hilo aliyatenda mambo makubwa mazuri kama wasifu wake ulivyoyataja” ameeleza.
Aidha Askofu Nyaisonga amesema kuwa marehemu Askofu Chengula alijiweka na kufanikisha mikakati ya kielimu, afya, miito na taasisi mbalimbali ili afikie dira yake, na hivyo ameikamilisha dira yake. “Tunahuzunika lakini huzuni takatifu” amesema.

Salamu za TEC
Akitoa salamu kwa niaba ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Makamu wa Rais wa TEC ambaye pia ni Askofu wa Jimbo Katoliki Geita Mhashamu Flavian Kassala amesema kuwa katika maisha yake marehemu Askofu Chengula amejidhihirisha kuwa baba mwenye moyo wa kutumikia na moyo mkuu wa mapendo ambapo historia yake inabaisha hayo wazi.
Ameeleza kuwa Askofu Chengula amekuwa chanzo cha furaha katika kila jumuiya aliyoishi huku akidhihirisha upendo na huruma hata kwa wale waliokuwa wanyonge ambapo hakusita kumgawia yeyote aliyehitaji upendo huo.
“Tutamkumbuka kwa malezi yake kwa vijana, kuwavuta waliopotoka warudi kundini na kuungana na walio wema. Alivuta miito mingi katika upadri na utawa. Alikuwa mwanga kwa wale waliotaka kuingia katika masiha ya ndoa. Matunda yake sisi sote tunayashuhudia leo” ameeleza.
Aidha ameongeza kuwa aliweza kutoa matamko mazito kwa lugha nyepesi na kusaidia kuwarudisha wengi, na kamba kuondoka kwake kumeacha pengo kubwa TEC kwani alikuwa chombo muhimu kwa umoja wa baraza. “Alikuwa tunu na hazina ya busara kwetu sisi maaskofu” amesema.

Naibu Spika atoa ombi kwa maaskofu
Akitoa salamu za rambi rambi Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Tulia Ackson amesema kuwa alichojifunza kutoka kwa Askofu Chengula ni kuwa na Upendo usio na mipaka.
“Alinipenda, nitajitahidi na nitamuomba Mungu anisaidie ili niweze kuwapenda watu wote bila mipaka. Alikipenda sana Kituo cha Afya cha Chewa, lakini pia sehemu ya kulelea watoto yatima, yeye alikuwa baba yao. Ninawaomba ili watoto wale na sehemu ile iendelee kuwa kimbilio kama ambavyo Askofu Chengula alivyopafanya kuwa kimbilio” ameeleza.

Msimamizi wa Jimbo
Wakati huo huo Baba Mtakatifu Fransisko amemteua Padri Francis Magalla kuwa Msimamizi wa Jimbo Katoliki la Mbeya, baada ya aliyekuwa Askofu wa Jimbo hilo Mhashamu Evaristo Chengula kufariki Dunia Novemba 21 mwaka huu.
Barua ya uteuzi huo imesomwa katika misa hiyo na Balozi wa Baba Mtakatifu nchini Askofu Mkuu Marek Solczyński ambaye pia aliongoza adhimisho hilo la Misa Takatifu.

Maziko ya Askofu Chengula
Mara baada ya mwili wa Askofu Chengula kuagwa TEC Novemba 26, 2018 ulisindikizwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere na kusafirishwa hadi Mbeya. Misa Takatifu kwa ajili ya kumwombea Marehemu Askofu Evaristo Chengula wa Jimbo Katoliki la Mbeya aliyefariki dunia Novemba 21, 2018 umezikwa kwenye Kanisa Kuu la Mtakatifu Anthony wa Padua, Jimbo Katoliki Mbeya, Novemba 27, 2018.
Askofu Evaristo Chengula alizaliwa Januari Mosi 1941, huko Mdabulo, Mufindi, Mkoani Iringa. Baada ya masomo na majiundo yake ya kitawa na kipadri, tarehe 15 Oktoba 1970 akapewa Daraja Takatifu ya Upadri.
Tarehe 8 Novemba 1996, Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Mbeya na kuwekwa wakfu kama Askofu tarehe 2 Februari 1997. Askofu Evaristo Marcus Chengula Amefariki dunia tarehe 21 Novemba 2018 kwenye Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar es Salaam.
Raha ya Milele umpe ee Bwana, na Mwanga wa milele umuangazie, apumzike kwa amani, AMINA.


Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU