Miaka 150 tuendeleze jumuiya ndogo ndogo, elimu, uongofu wa ndani
Askofu wa Jimbo Katoliki Morogoro
Mhashamu Telesphory Mkude amewahimiza waamini nchini Tanzania, kujikita katika
toba na wongofu wa ndani, huku wakiimarisha jumuiya ndogondogo.
Askofu Mkude ambaye alikuwa mwenyeji wa Maadhimisho ya Jubilei ya
Miaka 150 ya Uinjilishaji nchini Tanzania, Novemba Mosi 2018 wakati wa Ibada ya Misa Takatifu ya
ufunguzi wa Jubilei, sanjari na kuwakumbuka pamoja na kuwaombea Wamisionari
marehemu waliojitoa sadaka kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia furaha ya
Injili.
Amewataka waamini kutambua uwepo na madhara ya dhambi katika maisha
yao, tayari kukimbilia huruma na upendo wa Mungu utakaowaimarisha zaidi katika
imani inayomwilishwa katika ushuhuda na matendo.
Askofu Mkude amewataka waamini kuendelea kuimarisha utume wa Jumuiya
Ndogo ndogo za Kikristo, kipaumbele cha kwanza katika sera na mikakati ya
shughuli za kichungaji zinazotolewa na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu
Katoliki Afrika Mashariki na Kati, yaani, AMECEA! Amewasihi waamini kudumisha Ibada ya Rozari
kwa Bikira Maria, muhtasari wa historia ya huruma ya Mungu katika maisha ya
mwanadamu! Wawe kweli ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa
jirani zao.
Bikira Maria, Mama wa Mungu na Malkia wa Rozari Takatifu, amebarikiwa
kuliko wanawake wote, ni sura ya Kanisa iliyovishwa mwanga wa Pasaka; Yeye ni
heshima ya watu wa Mungu; mshindi dhidi ya dhambi na ubaya wa moyo!
Padri Saba: Mlei Mkatoliki ana wajibu wa
kutakatifuza ulimwengu
Akitoa mada kuhusu ‘Mlei Mkatoliki katika Kuyatakatifuza Malimwengu’
Padri Raymond Saba wa Jimbo Katoliki
Kigoma, ambaye amewahi kuwa pia Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki
Tanzania amesema kuwa njia ya utakatifu wa maisha, Kanisa nchini Tanzania
linaweza kupyaisha ari ya maisha ya kiroho na utume wake. Mafuta ya utakatifu
yanaweza kulisaidia Kanisa kuganga na kutibu majeraha ya watoto wake na
walimwengu katika ujumla wao, kwa kuonesha utimilifu wa upendo unaobubujika
kutoka kwa Kristo Yesu.
Hivi ndivyo anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa
kitume “Gaudete et exsultate” yaani “Furahini na kushangilia, wito wa utakatifu
katika ulimwengu mamboleo.”
Ameitaka familia ya Mungu nchini Tanzania kuchuchumilia furaha ya
kweli katika maisha na kuondokana na tabia ya kutaka kuyakumbatia malimwengu na
raha zake!
Toba na wongofu wa ndani, uwasaidie waamini kuchuchumilia neema ya
utakaso waliyoipokea wakati wa Ubatizo na hivyo waendelee kupyaisha imani yao
kwa Kristo na Kanisa lake na kuendelea kutekeleza mapenzi ya Mungu hapa
duniani, ili hatimaye, waweze kupata maisha na uzima wa milele!
Padri Kitima: Lazima kuendeleza matunda ya
uinjilishaji katika sekta ya elimu
Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania Padri Charles
Kitima, amesema kwamba, elimu na mchakato wa uinjilishaji ni sehemu ya vinasaba
vya maisha na utume wa Kanisa na kamwe haviwezi kutenganishwa.
Tanzania haina budi kumshukuru Mungu kwa mchango mkubwa uliotolewa na
Kanisa katika sekta ya elimu na maendeleo ya jamii katika kipindi cha miaka 150
iliyopita.
Huu ni wakati wa kusimamia na kuendeleza matunda ya uinjilishaji
katika sekta ya elimu,kwa Kanisa kuendelea kuwekeza katika elimu bora zaidi,
itakayowasaidia watanzania kupambana na hali pamoja na mazingira yao, ili kweli
Tanzania iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Huu ni wakati muafaka kwa
Kanisa na Serikali kushikamana kwa dhati ili kudumisha: ustawi, maendeleo na
mafao ya watanzania wengi katika sekta ya elimu kwani Kanisa ni mdau mkubwa wa
maendeleo nchini Tanzania!
Kuna uhusiano mkubwa kati ya shule zinazomilikiwa na kuendeshwa na
Kanisa Katoliki pamoja na dhamana ya Uinjilishaji wa kina inayovaliwa njuga na
Mama Kanisa katika mapambazuko ya Uinjilishaji nchini Tanzania. Ili kutambua
umuhimu huu, kuna haja kwanza kwa walimu, walezi na wanafunzi wenyewe kufahamu
changamoto inayoletwa na Kanisa kwa wakati huu!
Shule na taasisi za elimu ya juu pamoja na vyuo vikuu vinavyomilikiwa
na kuendeshwa na Kanisa Katoliki, vimekuwa ni vituo vya majiundo makini ya
vijana: kiakili, kimaadili, kiroho na kiutu, kwa kuzingatia ubora na viwango
vya kitaifa na kimataifa, ukweli ambao kamwe hauwezi kufumbiwa macho nchini
Tanzania.
Shule, taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu vimekuwa ni vituo vya
majadiliano ya kidini na kiekumene; mahali pa kurithisha imani, maadili na utu
wema. Kutokana na dhamana hii, vijana wanapaswa kuwa kweli ni wadau wa
uinjilishaji kwa njia ya ushuhuda wa maisha na matendo yao adili. Jambo msingi
kwa walimu, wazazi na walezi ni kutambua dhamana na utume wa shule za
kikatoliki katika mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu
mzima: kiroho na kimwili, ili waweze kushiriki kikamilifu katika kuwajengea
watoto na vijana msingi wa imani, maadili na utu wema.
Hapa ni mahali pa kujenga na kuimarisha upendo kwa Mungu na jirani,
ili wanafunzi wanaohitimu kutoka katika shule za Kikristo waweze kuwa kweli ni
wadau katika kuyatakatifuza malimwengu. Dunia inawahitaji vijana watakaotoka
kifua mbele kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili, kwa kutambua kwamba,
shule na taasisi hizi ni vyombo makini vya mchakato wa uinjilishaji na
utamadunisho!
Comments
Post a Comment