KUELEKEA KILELE CHA JUBILEI KUU – ARI YA KICHUNGAJI MUHIMU
Katika kuadhimisha
Jubilei ya miaka mia moja na hamsini ya Uinjilishaji, Kanisa Katoliki Tanzania
linamshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kuwatuma Wamisionari kuja kutangaza Injili
Tanzania. Kwa kuzingatia jinsi Wamisionari walivyojitoa katika kutangaza
Injili, na kupambana na changamoto mbalimbali, Kanisa la Tanzania linapaswa
kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa Uinjilishaji wa miaka hiyo mia na hamsini.
|
Awamu za Uinjilishaji
Wataalamu wa historia hutueleza kwamba katika Afrika ya Mashariki,
Uinjilishaji wa kwanza ulifanywa na Wamisionari wa shirika la Mtakatifu
Agustino mnamo mwishoni mwa karne ya kumi na tano. Wamisionari hao walifuatana
na mvumbuzi mashuhuri aitwaye Vasco da Gama, na walifika Zanzibari 1499 na
lengo lake lilikuwa kutafuta njia ya kwenda India na mashariki ya mbali.
Katika kuinjilisha, wamisionari hao walipata upinzani mkubwa kutoka kwa
Waarabu. Walijitahidi kuendelea lakini
mnamo mwaka 1698 Uinjilishaji huo ni kama ulififia. Sababu kubwa ya kushindwa
ni kutokana na uvamizi wa Waarabu kutoka
Omani. Waarabu hao walikuwa na nguvu na kuweza kutawala sehemu hizo za pwani.
Uinjilishaji wa awamu ya pili ndio ulioanza katika karne ya kumi na
tisa. Wamisionari wa shirika la Roho Mtakatifu walifika kwanza Zanzibari mwaka
1863. Licha ya kupata upinzani mkali, Wamisionari hao hawakukata tamaa. Mwaka
1868 walifika Bagamoyo na kuanza Uinjilishaji Tanganyika. Kama tulivyoona
katika mada nyingine, walihubiri Bagamoyo na ujirani wake baadaye waliendelea
kaskazini mwa Tanganyika mpaka kufika sehemu za Moshi na Arusha. Licha ya
kupata changamoto ya hali ya hewa na maradhi mbalimbali na wengine wao
kufariki, hawakukata tamaa hata kidogo. Waliendelea kufika na kuhubiri Injili.
Baadhi ya watumwa waliokuwa huru na kuwa Wakristo, waliwasaidia wamisionari hao kama
makatekista.
Miaka kumi baadaye, mwaka 1878 shirika la Mababa Weupe lilifika Zanzibari na baadaye Bagamoyo.
Kutoka hapo Bagamoyo waliamua kuelekea
upande wa magharibi mwa Tanganyika mpaka kufika sehemu za Tabora. Hapo
waligawanyika katika makundi mawili. Kundi moja lilielekea kaskazini mpaka sehemu
za ziwa Viktoria, na kundi jingine liliendelea kwenda magharibi mpaka ziwa Tanganyika.
Wamisionari walioelekea kaskazini waliweza kuinjilisha sehemu za
Mwanza na ujirani, kumbe wale
walioelekea magharibi waliweza
kuinjilisha Kigoma na ujirani wake; baadaye walielekea kusini mpaka sehemu za
Mbeya. Hata hao walipata changamoto za kuumwa na hali ya hewa iliyowaletea adha
mbalimbali. Hata hivi Mwenyezi Mungu aliwajalia uvumilivu, waliendelea kuhubiri
Injili bila kukata tamaa; katika bidii na ari yao waliweza kwenda hata nchi jirani za Rwanda na
Burundi na sehemu ya mashariki ya Kongo.
Kama tulivyokwishasema kwa nafasi nyingine, shirika la tatu katika awamu
hii ya pili ya Uinjilishaji walikuwa wamisionari wa Mtakatifu Benedikto kutoka
Ujerumani. Hao walifika Dar es Salaam mwaka 1887, miaka kumi baada ya kufika
wamisionari wa shirika la Mababa au Mapadri Weupe. Shirika hilo, baada ya
kufika Dar es Salaam waliweka kituo chao Pugu. Kutoka Pugu walielekea kusini
wakipitia sehemu za Dodoma na Mahenge.
Vituo vikuu huko kusini mwa Tanganyika vilikuwa Tosamaganga karibu na Iringa, Ndanda karibu na Masasi na Peramiho karibu na mji wa Songea.
Walichagua kuweka vituo vikuu nje ya mji ili kutojihusisha na mambo ya kisiasa,
watu waone tofauti kati yao na wazungu
wa serikali.
Ari ya Wamisionari
Hapana shaka wamisionari walikuwa na ari kubwa ya kichungaji. Walitoka
nchi za mbali kuja Tanzania na kupambana na changamoto mbalimbali siyo kwa
ajili ya kutalii bali kwa ajili ya kazi
moja tu ya kuhubiri Injili. Kwa sababu hiyo walitafuta njia mbalimbali kuifikisha
imani ya Kikristo kwa watu. Kwa mfano walianzisha shule za awali vijijini na kuwafundisha watoto kusoma na
kuandika, lakini waliwafundisha pia imani, namna ya kusali na mafundisho ya
katekisimu.
Wamisionari wa Mtakatifu Benedikto walioinjilisha kusini mwa Tanzania,
kwa mfano, walifika katika timu au umoja na kila mmoja akiwa na majukumu yake.
Walikuwa mapadri, masista na pia watawa wakiume walioitwa mabradha au mabruda.
Neno bruda linatokana na neno la kijerumani
der bruder maana yake kaka. Bruda alikuwa mtawa mwanamume asiye padri.
Mapadri walijishughulisha na uchungaji, yaani: kufundisha katekisimu
mashuleni, kuadhimisha sakramenti na kutembelea vijiji kuadhimisha Ekaristi.
Walikuwa na ratiba katika kuhakikisha wanavitembelea vijiji au vigango vyote katika uchungaji.
Masista kwa upande wao waliweza kufundisha pia mashuleni, na kuwafundisha
wasichana kwa kazi za nyumbani. Sista mmoja aliangalia usafi wa kanisa na
maandalizi ya mavazi ya misa. Mwingine alikuwa mpishi na kuwa na bustani; huyo
alihakikisha chakula kinapatikana kwa
wakati wake kwa ajili ya jumuiya yote.
Mabradha walikuwa na kazi za nje kama ujenzi, ufugaji na useremala. Hao
pia walikuwa na wafanyakazi, kabla ya kuanza kazi wafanyakazi walipata katekesi
fupi kisha walisali pamoja ndipo kila mmoja alielekea sehemu yake ya kazi na
kuanza kazi. Mchana walipofunga kazi ilitolewa alama na wote walikusanyika ili
kusali pamoja kisha kuondoka. Kila mmoja alitimiza wajibu wake ili wawe na afya
njema.
Utaratibu wa kusali na wafanyakazi wao kabla ya kuanza kazi ulikuwa ni
sehemu ya Uinjilishaji ambao hata
masista waliutumia. Sista mpishi alisali na wasichana waliomsaidia jikoni kabla
ya kuanza rasmi kazi za jikoni. Walipokwenda shambani au bustanini sista
alianzisha sala fupi kabla ya kuanza kazi.
Kama kaulimbiu yao inavyosema: Ora et Labora yaani Sala na Kazi ndivyo
wamisionari walivyowafundisha wafanya kazi wao kuwa na bidii katika kusali na
kufanya kazi. Kwa njia hiyo masista na mabradha waliungana na padri katika
uchungaji; kuwahimiza waamini kusali na
kumtegemea Mungu katika maisha.
Ari ya Uwajibikaji
Kuadhimisha Jubilei kuwe fursa ya kuamsha ari ya kichungaji. Kutokana na
mazingira tofauti, kuhani au katekista hushawishika kufanya mambo muhimu tu
katika uchungaji, kama vile kuadhimisha Ekaristi na kuwahudumia wagonjwa katika
hatari ya kufa. Hutumia muda mwingi kati ya juma kufanya kazi za kimaendeleo
kama vile mashambani au miradi mingine
ili wapate fedha ya kujikimu.
Katika parokia nyingine, hata hivi jambo hilo linatekelezwa; waamini
wanahakikisha kuhani anapata chombo cha usafiri, chakula na mahitaji muhimu
pamoja na pesa kwa matumizi yake binafsi. Wakristo huhakikisha pia makatekista
wanapata mahitaji yote muhimu. Katika mazingira hayo wachungaji inawapasa
kutumia muda mwingi kufanya uchungaji ili kuwaimarisha waamini katika imani.
Ari na bidii waliyokuwa nayo wamisionari, iwahimize waamini, kwa nafasi
hii, kuhakikisha wachungaji wao wanapata chakula na mahitaji muhimu ili watumie
muda wao zaidi kwa ajili ya
Uinjilishaji. Wachungaji nao wakisukumwa na ari ya Wamisionari wawajibike
katika Uinjilishaji, tena Uinjilishaji wa kina.
Comments
Post a Comment