TEC yawasilisha rai kwa serikali
Yasisitiza kujenga jukwaa la majadiliano katika ukweli na uwazi
Na Sarah
Pelaji, Dar es Salaam
RAis John Pombe Magufuli wa Tanzania,
Agosti 7, 2018 amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa Jumuiya ya
Wakristo Tanzania, CCT pamoja na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania TEC,
walioomba kukutana naye na kujitambulisha, Ikulu, Jijini Dar es Salaam.
Ujumbe wa Jumuiya ya Wakristo Tanzania umeongozwa na
Askofu Anikilisa Cheyo, Mwenyekiti na kwa upande wa Baraza la Maaskofu Katoliki
Tanzania, ujumbe umeongozwa na Askofu Gervas John Nyaisonga, Rais wa Baraza la
Maaskofu Katoliki Tanzania.
Kwa upande wake, Rais Magufuli amewahakikishia
viongozi wa Makanisa kwamba, yuko pamoja nao na kuwataka kufanya kazi kwa
kujiamini na kwa uhuru na ikiwa kama wanalo jambo lolote lile, wamjulishe na
kwamba, atalishughulikia. Amewataka viongozi wa Makanisa kuwahubiria Watanzania
amani, upendo na mshikamano pamoja na kuipenda nchi yao!
Akizungumza na gazeti hili, Makamu Rais wa Baraza la
Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) Askofu
Flavian Kassala, amesema kuwa, katika mkutano huo, mambo makuu manne
yamejadiliwa kwa kina na mapana: Kwanza kabisa ilikuwa ni nafasi ya
kujitambulisha kama viongozi wapya wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania;
Pili kumshukuru kwa kuendelea kujenga mahusiano mema na Kanisa, tatu kumpongeza
kwa ujasiri, ari na mwamko wa maendeleo nchini Tanzania na hatimaye,
kuwasilisha rai ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania.
Askofu Kassala amempongeza Rais Magufuli kwa moyo wake
wa uzalendo, ari na moyo mkuu wa kutaka kuwaletea watanzania maendeleo endelevu
ambayo kwa namna ya pekee kabisa yanajionesha katika ujenzi wa miundo mbinu ya
barabara, vyombo vya usafiri pamoja na majengo ya huduma.
Kanisa
linampongeza Rais kwa kukuza na kudumisha nidhamu katika utumishi wa umma;
mapambano kwa vitendo dhidi ya rushwa, ufisadi na wizi wa mali ya umma, mambo
ambayo yalianza kulitumbukiza taifa katika utovu wa nidhamu na kumong’onyoka
kwa maadili na utu wema.
“Rais Magufuli amekuwa mstari wa mbele kusimamia
rasilimali za taifa na hasa madini ili faida inayopatikana, iwe ni kwa ajili ya
ustawi, maendeleo na mafao ya watanzania wote. Wameipongeza Serikali kwa kutoa
elimu bila malipo kwa shule za msingi na sekondari, jambo ambalo linatoa fursa
kwa watoto wengi kupata elimu, tayari kupambana na hali na mazingira yao.
Maaskofu wanaipongeza Serikali kwa maboresho makubwa katika huduma ya afya na
ustawi wa jamii. Serikali ya awamu ya tano imeendelea kusimama kidete katika
kutatua migogoro ya ardhi, ambayo ilikuwa ni kero kubwa ya kitaifa. Ikumbukwe
kwamba, ardhi ni mtaji wa maskini, unaoweza kuwasaidia watanzania wengi kuwa na
uhakika wa usalama wa maisha yao, kwa kuwekeza katika kilimo na makazi.
Askofu Kassala anasema, Baraza la Maaskofu Katoliki
Tanzania limewasilisha rai kwa serikali, ili kujenga jukwaa la majadiliano
katika ukweli na uwazi kuhusiana na masuala ya elimu, afya na ustawi wa jamii,
ambayo, kwa hakika Kanisa limekuwa ni mdau mkuu.
Kumbe, kabla ya Serikali haijatoa maamuzi ambayo
yanaweza kuwa athari kwa huduma zinazotolewa na Kanisa, ni vyema, kukawa na
utamaduni wa kujadiliana, ili kupima: matatizo, changamoto na mafanikio ya sera
na mikakati kama hiyo. Lengo ni kuliwezesha Kanisa kutoa huduma bora na makini
kwa familia ya Mungu nchini Tanzania. Pale ambapo kuna maridhiano ya pande zote
zinazohusika, kwa hakika hata utekelezaji wake utakuwa na ufanisi mkubwa.
Askofu Kassala anakaza kusema, uhusiano kati ya
Serikali na Kanisa unazingatiwa katika huduma za kijamii, hususani afya, elimu na ustawi wa jamii. Ndiyo maana,
leo hii, Kanisa linaadhimisha Jubilei ya Miaka 150 ya mfumo rasmi wa elimu
ulioanzishwa mjini Bagamoyo na Shirika la Roho Mtakatifu na matunda yake
yakaanza kuonekana miaka mia moja baadaye, kwa shule za Kanisa kutoa viongozi
wazalendo, waliojisadaka kwa ajili ya uhuru, ustawi na maendeleo ya watanzania
wengi! Kati yao ni Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Askofu Kassala anasema, mazungumzo yao na Rais
Magufuli yalikuwa katika hali ya utulivu, amani na maelewano kwani lengo ni
kudumisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi: kiroho na kimwili. Umekuwa ni
muda wa kusikilizana na kuondoa shaka pale ilipojitokeza. Rais Magufuli
amewashukuru na kuwapongeza Maaskofu na kuwataka kujenga na kudumisha utamaduni
wa kukutana na kujadiliana katika ukweli na uwazi. Anasema, si rahisi sana
kuona mafanikio na kwamba, bado anahitaji watanzania kumsindikiza katika sala,
ili daima aweze kumtanguliza Mungu katika maisha na maamuzi yake, kwani
yanagusa watu wengi na hata wakati mwingine, yanabeba changamoto kubwa kwake
binafsi na kwa taifa katika ujumla wake. Amesema, Serikali itaendelea
kushirikiana na Makanisa pamoja na taasisi zake katika sekta ya elimu na afya,
kwa kutoa ruzuku kadiri ya Mkataba wa PPP “Public Private Partinership, yaani
Mkataba wa Mahusiano Kati ya Taasisi za Umma na Sekta Binafsi.
Comments
Post a Comment