Mahari yatajwa kuchangia unyanyasaji kijinsia Dodoma
IMEELEZWA kuwa changamoto ya wazazi kupenda mahari na
kuwaoza watoto wao wakiwa wadogo ni moja
ya sababu inayochangia kukithiri kwa ukatili wa kijinsia na mimba za utotoni
wilayani Chamwino.
Hayo yameelezwa na baadhi ya
viongozi wa vikundi mbalimbali vya uelimishaji rika kupitia mradi unaosimamiwa na shirika
lisilokuwa la kiserikali (WOWAP) chini ya ufadhili wa The faoundation for civil
soceity ukiwa na lengo la kutokomeza
ukatili wa kijinsia na mimba za utotono
wilayani humo.
Mmoja wa viongozi hao wa uelimishaji rika Nyamwanji Nyamwanji
akizungumzia suala hilo amesema kuwa ijapokuwa serikali imesema elimu ni bure
kuanzia shule ya msingi hadi sekondari lakini jamii bado haioni umuhimu wa
elimu na kuthamini mahari na kuoza watoto wao wakiwa wadogo.
Amesema kuwa tatizo lililopo
hivi sasa wazazi wengi hawaoni umuhimu wa elimu jambo ambalo inafika wakati
hata kuwashawishi watoto wao wafanye vibaya katika mitihani yao ili wasifaulu
na baadaye waweze kuwaoza.
“Kwa kweli changamoto ya mahari
katika jambo hili tunalopambana nao bado ni kubwa kwani wazazi wengi
wanathamini mahari kuliko elimu ya watoto wao wa kike jambo ambalo kwa kweli
tunaiomba serikali nayo iliangalie jambo hili kwani watoto wengi wanakatisha
masomo.” amesema
Aidha amesema kuwa kwa hali ya
sasa wao kama viongozi wa vikundi wamebaini kuwa lipo tatizo la wazazi wengi
kutowajibika pia kwa watoto wao katika matumizi ya watoto jambo ambalo nalo
linachangioa watoto kujiingiza katika mambo yasiyofaa na kujikuta wakiingia
katika vishawishi.
Hata hivyo amesema kuwa lipo
tatizo lingine ambalo bado linawakwamisha pindi wanapotaka kushughulikia suala
la kutokomeza ukatili huo wa kijinsia na mimba za utotoni nalo ni suala la kukosa ushirikiano kutoka kwa viongozi wa
serikali za vijiji, kata na hata mahakamani.
Amebainisha kuwa suala la rushwa
nalo ni kikwazo kwani sheria ingefuatwa na baadhi ya watu wanaowaoa hao watoto
au kuwapa mimba wangehukumiwa kwenda jela ingeweza kuwa funzo kwa wengine na
kuacha kuwachezea watoto hao wadogo.
Vile vile amesema kuwa
changamoto nyingine kwenye jamii ni pamoja na wivu, rushwa, kukosa ushirikiano,
waelimishaji kuonekana wabaya kwenye jamii pamoja na kuogopa kutishiwa.
Kwa upande wake Mratibu wa Mradi
huo kutoka WOWAP, Nasra Suleimani amesema kuwa wao kama shirika wanaendelea
kuwafuatilia viongozi hao katika kuwakumbusha majukumu yao ya kutoa elimu kwa
jamii ili jambo hilo liweze kutokomezwa.
Amesema kuwa wao kama shirika wanaendea na kuhamasisha jamii
kupitia vikundi hivyo kwa njia ya ngoma, wakulima, wafugaji, wasanii lengo
likiwa ni kufikia malengo ya suala hilo kuisha kabisa.
Comments
Post a Comment