‘Mwanakwaya mwenye vikwazo vinavyomtenga na ekaristi hataruhusiwa kuimba’
WITO umetolewa kwa wanakwaya wote wa
Parokia ya Bikira Maria Mama wa Fatima Geita kuhakikisha wanakuwa mfano hai wa
kupokea masakramenti, ambapo hadi kufika juma la kwanza la majilio kila
mwanakwaya ambaye atakuwa hajarekebisha ndoa au kuondoa kikwazo chochote
kinachomtenga na sakramenti za Kanisa hataruhusiwa kuimba.
Wito huo umetolewa na
Padri Gerald Singu Paroko wa Parokia ya Bikira Maria Mama wa Fatima Geita
wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu akiwa anaongea na waamini wa Parokia hiyo
katika mahubiri yaliyoenda sambamba na maadhimisho ya Siku ya Vijana Kijimbo.
Padri Singu mesema kuwa
haiwezekani mwanakwaya ahamasishe waamini katika nyimbo kwenda kukomunika
wakati yeye anabaki amekaa kwenye kiti.
Pia ametoa rai kwa viongozi wa ngazi
mbalimbali za kanisa katika parokia hiyo kuanzia ngazi ya jumuiya kuwafikia
waamini wote wasiopokea masakramenti kuwafikia na kuwashauri kurudia
masakramenti, wawape miongozo itakayowafanya waone ni jambo jema kwao kurudia
masakaramenti na kwamba asiwepo kiongozi wa kuwakatisha tamaa.
Wakati huo huo paroko
huyo ametoa wito kwa wanaume katika familia kutowakwamisha wake zao wenye nia
ya kurudia masakramenti kwa kuwawekea vikwazo visivyo na msingi na badala yake
wanandoa wote wafanye bidii ya pamoja kurudia masakramenti waliyojifungia wao
wenyewe.
Padri Singu amesema
kuwa inavyoonekana akina mama wengi wanayo nia na hamu kubwa ya kutaka kurudia
masakramenti lakini wanakutana na vikwazo kutoka kwa waume zao na hivyo
kuwafanya waendelee kujitenga naYesu wa ekaristi kitu alichosema kuwa si chema
kwa mkristo anayejitambua.
“Akina baba acheni
kuwawekea vikwazo akina mama wanapotaka kurudia masakramenti, inavyoonekana
akina mama wanayo hamu kubwa ya kutaka kurudia masakramenti lakini
wanapowashirikisha ninyi akina baba mnakuwa na vikwazo vikiwemo kuwa
hamjajipanga. Mnajipanga nini? rudieni fungeni ndoa hata bila sherehe, sherehe
yenu kubwa iwe ni kumpokea Yesu katika Ekaristi Takatifu” amesema.
Akihimiza zaidi juu ya
jambo hilo muhimu kiroho amesema kuwa waamini wote waliojifungia kupokea
sakramenti za kanisa waache ukaidi na waone kujitenga na sakramenti hizo
wanapungukiwa na kitu cha maana.
Comments
Post a Comment