Askofu Chengula: Padri bora hanywi pombe kilabuni
WITO umetolewa kwa
viongozi wote wa kiroho hususani mapadri kutambua kuwa kunywa pombe kilabuni
siyo tabia za padri mzuri ambaye anamuwakilisha Kristo Duniani.
Wito
huo umetolewa na Askofu wa Jimbo Katoliki Mbeya Mhashamu Evaristo Chengula
wakati wa Ibada ya Misa Takatifu ya Daraja ya upadri kwa Shemasi Jacob
Machibya, iliyofanyika Parokia ya Chunya Jimboni Humo.
Katika
homilia yake Askofu Chengula amebainisha kuwa yapo mambo mengi ambayo
yanawezesha kujua kiongozi bora na muadilifu mbele za watu, lakini kipimo
ambacho pia kitaimarisha zaidi nafasi ya
kiongozi kama padri muwakilishi wa Kristo ni pamoja na kufanya mambo sahihi na
kwa wakati.
“Sidhani
kama litakuwa jambo la busara kwa padri kukaa kilabuni na kuanza kunywa pombe,
hapana hiyo siyo tabia njema” amesisitiza Askofu chengula.
Katika
hatua nyingine Askofu Chengula amewaasa viongozi wa Halmashauri Walei kuwa na
uwezo wa kuzungumza na mapadri wao bila ya kuwa na wasiwasi na jambo lolote, na
hiyo itakuwa na tija zaidi tofauti na kuzungumza wao binafsi bila ya
kumfikishia ujumbe muhusika, kwa kufanya hivyo ni wazi kuwa wanatenda dhami na
pia muafaka hautapatikana.
“Padri
siyo malaika naye anakosea lakini unakuta viongozi wa Halmashauri Walei
wanaogopa kumuambia wanakaa kimya. Hapana hiyo siyo sawa kwani kazi ya padri ni
pamoja na kukemea yaliyo mabaya, sasa kama ukiona na yeye anakosea ni laazima
utafute njia nzuri ya kumrudisha na siyo kukaa kimya” amesema Askofu Chengula
huku akiongeza kuwa katika mazungumzo mambo mengi yanafanikiwa.
Wakati
Askofu chengula akiwaasa walei kuwaombea mapadri na watawa pia amekumbusha kuwa
jukumu la kuombea miito mitakatifu nalo ni la kila mkristo, na itasaidia watoto
wengi zaidi kuwa na hamu ya kumtafuta Kristo kupitia Daraja Takatifu ya Upadri.
Katika
ibada hiyo ya misa iliyofanyika tarehe 16/08/2019 katika Parokia ya Chunya
jimbo la Mbeya, Shemasi Jacob Machibya
amepewa Daraja Takatifu ya Upadri na Askofu Evaristo Chengula huku akimuahidi
sala na maombi yake ili aweze kudumu vema katika nafasi yake ya upadri.
Comments
Post a Comment