Wingi wa maji si hoja katika ubatizo

Katibu Mkuu wa Jimbo Katoliki Morogoro Padri Luitfrid Makseyo amesema, Sakramenti ya Ubatizo wa Roho Mtakatifu ni sakramenti ambayo inamuondolea mtu dhambi ya asili na kumtayarisha kupokea sakramenti nyingine za Kanisa ili kupata uzima wa milele.
“Kama tukifikiri wingi wa maji ndiyo unaomtakasa mwanadamu maana yake tunaiweka akili yetu kuamini kwamba dhambi ya mwanadamu imekaa kwenye ngozi yake, na ndiyo maana wengine wanazamishwa kwenye maji ili wingi wa maji uweze kuwatakasa na kuwasafisha, dhambi si kama matope.”
Padri Makseyo amesema hayo hivi karibuni katika adhimisho la Misa Takatifu sherehe ya Ubatizo wa Bwana katika Kanisa la Bikira Maria mkingiwa dhambi ya asili iliyopo Jimboni humo. 
Padri Makseyo amesema kuwa, Ubatizo wa Roho Mtakatifu ni tofauti kabisa na ubatizo wa Yohane ambao ni ubatizo wa toba unaomwezesha mtu kutambua kuwa yeye ni mdhambi na anaweka makusudio ya kutokutenda dhambi tena.
Aidha amesema kuwa ubatizo huo wa Yohane wako watu wengi katika madhehebu yao bado wanaufuata mpaka leo hii, wanapohitaji kubatiza  watu lazima wabatizwa wapelekwe mtoni kwenye mabwawa au kuwapeleka katika visima vyenye maji mengi, akisema kuwa wingi wa maji si kigezo cha kumuondolea mtu dhambi.
Ameeleza kuwa, wingi wa maji siyo hoja ya msingi katika ubatizo, isipokuwa nguvu ya Roho Mtakatifu ndiyo kigezo katika utaratibu wa ubatizo wenyewe.
 Nguvu ya Roho Mtakatifu ndiyo inayoshuka na kumuondolea mtu dhambi zake kupitia sala inayotolewa na mbatizaji, ambapo maji ni ishara wazi inayoonekana katika tukio la ubatizo ili kuleta utakaso wa mbatizwa.
Hata hivyo padri Makseyo amewaasa waamini kuondokana na dhana ya kudhani kwamba wingi wa maji ndiyo unaomtakasa mwanadamu, maana yake inamfanya mwanadamu aweze kuamini kwamba dhambi zake ziko kwenye ngozi au mwili wake, kumbe dhambi si kama matope na wingi wa maji si hoja katika ubatizo
 Amewaasa waamini kutambua dhana nzima ya maana ya ubatizo kwamba Kanisa linasisitiza kuwa wazazi wanapaswa kuwabatiza watoto wao mapema zaidi mara baada ya kuzaliwa ili kumuondolea mtoto dhambi ya asili, hivyo wasimezwe na mafundisho ya mkopo yatolewayo na makanisa mengine kwamba mwanadamu anapaswa kubatizwa akiwa katika umri mkubwa
“Ubatizo ni wakati wowote mtu anapoomba kupata ubatizo hakuna kipimo cha wakati, kama sisi wakatoliki tukiwaacha watoto wanakaa muda mrefu bila kubatizwa ni makosa. Kanisa halijafundisha hivyo, Kanisa linamtaka mtoto hata mara baada ya siku ya tatu za kuzaliwa anaweza kubatizwa, ni vyema zaidi mtoto aondolewe dhambi ya asili mapema” amesema.



Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU