Kanisa kujitoa rasmi kuchukua Hospitali ya Rufaa Kwangwa Musoma

Modest na Bertha Mayayi Musoma.
Imeelezwa kuwa kukosekana kwa hati miliki, thamani kubwa ya fidia, pamoja na kukosekana kwa wahisani wa ufadhili zimetajwa kuwa ni miongoni mwa sababu zilizosababisha Kanisa Jimbo Katoliki Musoma kujitoa rasmi kimaandishi juu ya ombi la kuchukua na kuendeleza Hospitali ya Rufaa Kwangwa ambayo kwa sasa inasimamiwa na serikali.          
Hayo yamebainishwa na Askofu wa jimbo hilo Mhashamu Michael Msonganzila hivi karibuni wakati akichangia hoja katika kikao cha kamati ya ushauri ya Mkoa wa Mara (RCC) ambapo alikieleza kikao kuwa maazimio mengi ya kikao hicho kuhusu Kanisa kuendelea na ujenzi wa Hospital hiyo, yameshawasilishwa kwa maandishi katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara.
Askofu Msonganzila amesema kuwa, Kanisa lilifuatilia vielelezo muhimu vya umiliki halali wa hospitali hiyo ya rufaa kwa muda wa miaka miwili bila mafanikio yeyote ikiwa ni pamoja na kukosekana kwa hati miliki ya eneo husika kama ilivyoahidiwa na kutolewa January 20 mwaka 2008.
Pia baada ya kufahamika kuwa Kanisa Katoliki linachukua na kuendeleza hospitali hiyo walijitokeza watu wengi wanaodai fidia yenye thamani ya shilingi milioni thelathini na nane jambo ambalo Kanisa halikuelewa.
“Tulijiuliza ni kwa nini   madai hayo ya fidia yanakuja   tena yenye gharama kubwa hivyo? Je, ni kwa sababu ya Kanisa Katoliki kuchukua eneo au laa! Nalo halikupata majibu na mbali zaidi Kanisa lilifanya jitihada za kupata wahisani wa kufadhili upatikanaji wa fedha zilizohitajika kwa wakati huo lakini lilikwama,”amesema Askofu Msonganzila.    
  Hata hivyo Kanisa limepokea barua kutoka katika ofisi ya Mkoa iliyotoa muda wa miezi sita vinginevyo serikali ichukue eneo lake ndipo Kanisa kupitia kikao hichohicho cha kamati ya ushauri, likaridhia kujitoa rasmi kimaandishi kati yamwaka 2010 na mwaka 2011.                       
Akizungumzia mchango wa Kanisa kwa Serikali katika utoaji huduma za jamii, Askofu Msonganzila amesema jitihada za kanisa Katoliki zimeonekana tangu  mwaka 1911  ambapo limejenga makanisa, vituo vya afya na shule ambazo baadaye zilitaifishwa na Serikali takribani shule kumi na sita na hivyo  Kanisa kukosa chochote, ingawa halikukata tamaa na kwamba mpaka sasa jimbo la Musoma lina  shule kumi zinazomilikiwa na Kanisa kwa ajili ya kusaidia jamii si tu kwa kufundisha bali hata kimalezi pamoja na kiimani.       
 Aidha amesema Kanisa pia linatetea haki za binadamu na amani ya mtu mmoja mmoja hususani akina mama na watoto wa kike ili wasinyanyaswena kutendewa ukatili kwa kuwatunza na kuwalea katika vituo vya Masanga, Rogolo na kituo cha Terminal Female Genital Multilation (TFGM) ambao wamekimbia mila potofu ya ukeketaji.         
Hata hivyo ameeleza chamgamoto kubwa kuwa ni baadhi ya wazazi kupinga hatua hiyo lakini Kanisa halijakata tamaa na badala yake litakuwa na uvumilivu wa hali ya juu dhidi ya mapambano hayo.
Kanisa halivumilii ukatili huo hivyo litamkeketa mtoto wa kike kielimu na kumuandaa kiakili aweze kuwa na nafasi kubwa kwa jamii ya kutwaa madaraka si ya kimila pekee bali madaraka ya taifa na ulimwengu mzima.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mara ambaye ndiye mwenyekiti wa kikao hicho Adam Malima amewataka wajumbe wa kikao hicho kujadili namna ya kukamilisha ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kwangwa ambayo imeshindwa kukamilika kwa muda wa zaidi ya miaka hamsini sasa.


Comments

Popular posts from this blog

SALA YA ASUBUHI:SALI HIVI..

Ujio wa Wamisionari wa Kwanza Tanzania Bara (2)

HISTORIA YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU